SHARE

NA EZEKIEL TENDWA,

HAKUNA aliyeamini kile kilichotokea katika Uwanja wa Nou Camp, Machi 8, mwaka huu, pale Barcelona walipoibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya PSG ya nchini Ufaransa.

Ajabu ya mchezo huo ilitokana na ukweli kwamba, katika mchezo wa kwanza Barcelona walijikuta wakifungwa mabao 4-0 na kwa matokeo hayo kila mmoja akaamini kuwa miamba hiyo ya Hispania safari yao imeiva.

Hata wenyewe mashabiki wa Barcelona waliingia na kuujaza uwanja wao huo katika mchezo wa marudio, lakini hakuna aliyekuwa na uhakika wa kikosi chao kusonga mbele, ikizingatiwa kuwa PSG ni moja ya timu zenye uwezo mkubwa.

Mabao 4-0 waliyokuwa nayo kibindoni yalitosha kabisa kuwaaminisha mashabiki wao kwamba lazima watasonga mbele, lakini mawazo yao yakakomeshwa baada ya kukubali kuruhusu mabao hayo 6-1 ugenini, wakishindwa kulinda ile akiba waliyokuwa nayo.

Leo hii Barcelona watakuwa tena uwanja wao wa nyumbani kuwakabili Juventus ya nchini Italia, ambapo itabidi tena wafanye kazi ya ziada kupata ushindi mnono kama walivyofanya dhidi ya PSG.

Barcelona wanayo kazi kubwa ya kupindua tena matokeo, kwani katika mchezo wa kwanza wakiwa ugenini nchini Italia, walijikuta wakibamizwa mabao 3-0 na sasa wanatakiwa tena kuwafurahisha mashabiki wao pale Nou Camp.

Kitu kimoja tu kinaweza kuwasaidia Barcelona, nacho ni kupambana kama walivyofanya dhidi ya PSG na kwa kawaida yao wanapokuwa uwanja wao huo wa nyumbani ni wazi wanatumia kila njia kuhakikisha wanawazidi ujanja wapinzani wao.

Kama Barcelona wangekuwa Afrika, ni wazi wangefananishwa na timu za Kiarabu ambazo zinapokuwa uwanja wao wa nyumbani iwe jua au mvua watakuadhibu tu, labda itokee bahati mbaya tu.

Ni kweli kwamba Barcelona wanacheza soka la kuvutia sana, lakini ni moja ya timu zinazolalamikiwa kuwa mara kadhaa zimekuwa zikibebwa na baadhi ya waamuzi, hasa katika mchezo wao dhidi ya PSG, walipoibuka na ushindi wa mabao hayo 6-1.

Mwamuzi alilalamikiwa kuruhusu baadhi ya mabao ya Barcelona yaliyoonekana wazi yalikuwa si halali, huku akiwanyima PSG fursa kama hiyo, ndiyo maana hata mashabiki wa Juventus wanahofia hali kama hiyo.

Yote kwa yote, kama Barcelona wataweza kuupanda tena mlima huu mrefu dhidi ya Juventus kama walivyofanya dhidi ya PSG, ni wazi watakuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Kama Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Luiz Enrique atawapa kazi maalumu vijana wake na kupindua matokeo ya Juve ya mabao 3-0 waliyoyapata nyumbani kwao, basi apewe sifa zake na kombe liwekwe tayari kwa ajili yake.

Taarifa kutoka nchini Hispania zinadai kuwa, msimu huu ukimalizika Kocha huyo atafuta mavumbi na kutimka zake na heshima kubwa ambayo atakumbukwa nayo ni kutwaa ubingwa wa UEFA msimu huu.

Katika ubingwa huo, kama watafanikiwa kuutwaa, moja ya mambo atakayokumbukwa nayo ni kupinduapindua matokeo ya wenzake, akianzia na PSG, baada ya kikosi chake kufungwa mabao 4-0, akashinda 6-1, na shughuli ya leo itakavyomalizika.

Hakuna shaka kwamba shughuli ya yeo ni nzito, lakini Barcelona wanaweza wakafanya kitu kingine cha ajabu wakiwa na jeuri ya uwezo wa akina Lionel Messi, Luiz Suarez pamoja na Neymar JR.

Licha ya kwamba Juventus wana mabao 4-0, ni wazi watakuwa na wasiwasi wa kile kilichowapata PSG, lakini pia hata mashabiki wa Barcelona kuna uwezekano mkubwa kwamba wanao wasiwasi kwamba kifurushi walichokuwa nacho dhidi ya PSG, kinaweza kikachacha leo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here