SHARE

NA NIHZRATH NTANI JNR

Jioni moja, umbali wa maili 14 kutoka kusini mwa mji wa Bijeljina. Mwanaume mmoja aitwaye Tomislav Milisevic alikuwa miongoni mwa maelfu ya watazamaji waliosimama pembezoni mwa uwanja.

Tomislav alikuwa mahala hapo kushuhudia mashindano ya vijana ya Bosnian City of Bijeljina. Mashindano hayo kwa siku hiyo yalikuwa yanafanyika ndani ya ardhi ya kijiji kidogo cha Batar karibu na Bijeljina. Simulizi kuhusu mtoto mmoja wa ajabu ikaanza jioni hiyo.

Dakika kumi zilikuwa zimepita tangu Tomislav Milisevic angali akiwa amepigwa na butwaa.

Ni kama mtu asiyeamini kitu ama anayeshuhudia kitu fulani kikitendeka kwa mara ya pili huku akiwa haamini.

Ni kama angali yupo ndotoni. Ndoto iliyokuja kugeuka kuwa kweli miaka mingi baadae.

Ulikuwa uamuzi wa ghafla, uamuzi asiotarajia. Uamuzi bora kabisa ambao amewahi kuufanya maishani,Tomislav.

Tomislav ,alichukua kijidaftari chake kidogo na kufungua ukurasa wa kwanza kabisa. Kisha akachukua peni yake nyekundu na akaandika maneno mawili tu kwa herufi kubwa “LUKA JOVIC.” Ni miaka 13 imepita tangu kutokea kwa tukio hili.

NI NANI TOMISLAV MILICEVIC ?

Mwanaume huyu alipata kuwa msaka vipaji wa klabu ya Red Star Belgrade. Huku pia akiwa kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 12 ya klabu hiyo.

Miaka 13 iliyopita. Ni jioni hiyo. Tomislav alikuwa amemuona kwa macho yake Gerd Muller (aliyepata kuwa mshambuliaji hatari Duniani)katika mwili wa mvulana mdogo wa miaka 8 kwa wakati huo.

Tomislav alipata mshuhudia Muller na jioni hiyo akakiona kivuli cha Gerd Muller katika miguu ya mtoto huyu. Mtoto huyu ni Luka Jovic.

Aliondoka na jina la Jovic na siku chache baadae.Luka Jovic alikuwa ndani ya academy ya Red Star Belgrade. Hakuwepo hapo kwa bahati mbaya tu ama kwa sababu ya nguvu ya Tomislav. Alikuwa hapo kwa sababu ya maajabu yake.

“Namna alivyokuwa akiuamrisha mpira.lilikuwa jambo lililonistaajabisha mno. Alikuwa bora kwa kila kitu. Uwezo wake wa kuwatambuka walinzi na kufunga magoli mazuri ni tukio lililonifanya nibakie nikiduwaa. Kitu kingine alikuwa na uwezo wa kutumia miguu yote miwili kwa uwiano sawa.”

“Nilimuona kijana mwenye kipaji cha ajabu. Kipaji ambacho kwa zaidi ya miaka 20 ya kazi yangu sikuwahi kukiona kamwe. Nikajiambia sihitaji muda zaidi kumtazama. “

“Sekunde kumi zilitosha kulipitisha jina lake. Niliamini kuwa ; Muda tu utazungumza” Tomislav Milicevic akimzungumzia Luka Jovic.

Akiwa na miaka 21 hivi sasa. Historia kuhusu Luka Jovic inasisimua kwa upande mwingine.

NI NANI LUKA JOVIC?

Ni mfalme mdogo ndani ya dimba la “Commerzbank-Arena. Dimba linalomilikiwa na klabu ya Eintracht Frantfurt nchini Ujerumani.

Pamoja na wachezaji wengi mahiri kupita mahala hapo. Jovic anatajwa kuwa ndiye mchezaji mwenye kipaji zaidi aliyepata kuichezea klabu ya Eintracht.

Ndani ya ligi ya Bundesliga. Jovic ana rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga goli 5 ndani ya mechi moja katika historia ya ligi hiyo.

Nchini kwao Serbia. Jovic ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza “Eternal Derby” moja ya pambano la timu za mji mmoja yenye upinzani mkubwa zaidi Duniani.

Kiwango chake cha msimu uliopita. Kimekuwa habari kubwa Barani Ulaya. Miguu yake ikaipeleka klabu ya Eintracht Fankfurt hatua ya nusu fainali ya kombe la Europa ,mbali na kuifanya klabu hiyo kushika nafasi ya saba ndani ya Bundesliga.

Umahiri wake umewashangaza wengi. Magoli yake 17 na akitoa pasi za mwisho 6 katika mechi 32 za ligi. Huku akifanikiwa kutupia magoli 10 katika mechi 14 za Europa.

TUTAMSHUHUDIA NDANI YA SANTIAGO BERNABEU.

Kufanya vibaya kwa Real Madrid msimu uliopita kumewapa hasira kubwa wahafidhina wa Real Madrid. Mpaka sasa kuna majina kadhaa yameshatua kunako viunga vya Charmatin.

Mbali na Eden Hazard ambaye ni jina kubwa. Mtu mwingine ambaye anapaswa kutupiwa jicho ni huyu Luka Jovic.

Wakati mashabiki wengi wa Real Madrid wakihuzunika kuondoka kwa Cristiano Ronaldo msimu uliopita, aliyekuwa tegemeo kubwa klabuni hapo. Wakati wakijiuliza ni mchezaji yupi angeweza kuvaa viatu vyake.

Inakuchukua dakika chache kujua kuwa Luka Jovic ndiye mchezaji anayetazamiwa kuwa mrithi wake. Wanafanana karibu vitu vingi.

Luka Jovic ni mzuri wa kutumia miguu yote miwili kwa uwiano sawa. Akiwa mzuri pia kwa mipira ya juu.

Haikushangaza kwa Real Madrid kuamua kulipa ada ya euro 60 milioni ambayo ni rekodi klabuni Eintrach Frankfurt kupata huduma yake.

Bila shaka, msimu ujao. Mshambuliaji huyu anapaswa kutazamwa kwa jicho la kipekee. Muda utatupa majibu wakati utakapofika.Tusubiri

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here