Home Habari LWANDAMINA AAGA YANGA, AACHA UJUMBE MZITO

LWANDAMINA AAGA YANGA, AACHA UJUMBE MZITO

3557
0
SHARE

NA SAADA SALIM

KOCHA Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina, kesho anatarajia kuondoka nchini na kuelekea kwao Zambia, kutokana na matatizo ya kifamilia.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwassa, ameliambia DIMBA kwamba, wamepokea barua kutoka kwa Lwandamina ya kuomba ruhusa ya wiki moja kwenda kwao kwa ajili ya kuweka sawa mambo ya kifamilia na wao wamebariki safari hiyo.

“Kocha ataondoka kesho kutwa (kesho), kuelekea kwao Zambia, kwani hivi karibuni alipata msiba wa mpwa wake ambapo hakwenda katika mazishi, hivyo kipindi hiki tumeona aende kwa muda huu alioomba,” alisema.

Mkwassa alisema mara baada ya muda huo waliompa atarejea na kuendelea na majukumu yake ya kukinoa kikosi chao kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa.

Wakati Lwandamina akiondoka, ameacha ripoti nzito kwa Katibu Mkuu wa Yanga kuhusiana na usajili ambao klabu hiyo inatarajiwa kuufanya hivi karibuni, dirisha dogo litakapofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.

Yanga, ambao wataiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hapo mwakani, wanataka kuhakikisha hawaishii hatua za awali na badala yake mikakati yao ni kufika hata fainali, ndiyo maana wanataka kujipanga kisawasawa.

Tayari wapo baadhi ya wachezaji ambao wameshaingia katika rada za Wanajangwani hao, akiwamo kiungo fundi, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ kutoka Mtibwa Sugar, huku pia wakifikiria kuongeza straika mmoja na beki mmoja wa kati.

Katibu Mkuu wa Yanga, Mkwassa, alisema moja ya mikakati yao ni kuhakikisha wanafanya usajili wa nguvu kwa kuchukua wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu ili wajiimarishe zaidi.

“Kama unavyoona timu yetu imeandamwa na baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi, hivyo lazima tufanye usajili dirisha dogo, ikizingatiwa kuwa, moja ya malengo yetu ni kuhakikisha tunafika mbali kwenye michuano ya kimataifa,” alisema.

Mkwassa alisema watahakikisha usajili unaofanywa unakuwa kwa ajili ya kuboresha mapungufu yaliyopo katika kikosi chao kwa kuzingatia mapendekezo ya kocha wao, George Lwandamina na si vinginevyo.

Hata hivyo, licha ya katibu huyo kutoweka wazi mikakati yao, lakini DIMBA lina taarifa kwamba, Lwandamina ameshakabidhi mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji na sasa anayesubiriwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika.

“Kocha ameshaleta mapendekezo yake na anayesubiriwa ni mwenyekiti wa usajili, Hussein Nyika na kwa taarifa yako tu ni kwamba, ndani ya siku chache benchi la ufundi litakaa naye ili kuweka mambo sawa,” alisema kigogo mmoja ndani ya Yanga.

SHARE
Previous articleANAONDOKA
Next articleDONALD NGOMA ALIKOROGA YANGA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here