Home Habari LYON MIKONONI MWA GSM

LYON MIKONONI MWA GSM

450
0
SHARE

HUSSEIN OMAR NA CLARA ALPHONCE

KUNA msemo wa Kiswahili unasema ‘lisemwalo lipo’, baada ya hivi karibuni uongozi wa African Lyon kukubali kuiachia timu hiyo mikononi mwa Kampuni ya GSM kwa Sh bilioni moja za Tanzania.

Tetesi za timu hizo kuuzwa zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki mbili zilizopita, japo Mkurugenzi wa timu hiyo, Rahimu Kangezi ‘Zamunda’ amekuwa akikanusha, akidai taarifa hizo si za kweli.

Lakini DIMBA ilipata taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa Kangezi akithibitisha kuuzwa kwa timu hiyo kwenda GSM. Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa, kampuni hiyo imeanza kuwekeza fedha ili kuhakikisha timu hiyo inabaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

“Timu ipo mikononi mwa GSM kwa sasa, wao wameanza kuwekeza fedha kwa ajili ya timu, wanagharamia kila kitu, lengo ni kuinusuru isishuke daraja, na sasa wameanza usajili wa kimya kimya kwa wachezaji wanaowahitaji msimu ujao.

“Wana mpango wa kuacha wachezaji wote na kubakiza wachezaji watatu, ambao ni Miraji Adam, Kipa Rostand Youthe na Hassan Isihaka, ambaye bado wapo naye kwenye mazungumzo ya kumwongeza mkataba na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, Charles Otieno,” kilieleza chanzo chetu.

Hata hivyo, DIMBA lilipomtafuta Meneja Mkuu wa Kampuni ya GSM, Hersi Said, alithibitisha kufanya mazungumzo na uongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuinunua, ila bado mazungumzo hayajamaliziki.

“Kweli tupo kwenye mazungumzo ya awali na African Lyon, nia ni kuinunua timu hiyo na mazungumzo yanaendelea vizuri na huenda msimu ujao timu ikawa mikononi mwetu,” alisema Said.

Alipotafutwa Kangezi ili aweze kuzungumzia suala hilo, simu yake haikupatakana na kuna taarifa kuwa, hayupo nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here