Home Makala Maajabu ya jezi nyota waliowahi kuvaa namba za kipekee uwanjani

Maajabu ya jezi nyota waliowahi kuvaa namba za kipekee uwanjani

643
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

ACHANA na uhamisho wa pesa nyingi uliofanywa na klabu za Ligi Kuu ya England msimu huu kiasi cha kuvunja rekodi yao wenyewe kwa kutumia zaidi ya Sh bilioni 1 kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Katika usajili wa msimu huu, kuna kiungo mmoja anaitwa Jonathan de Guzman aliyesajiliwa na Chievo Verona, ambapo aliibua mjadala mkubwa baada ya kuchagua kuvaa jezi namba 1.

Jezi hiyo iliyochaguliwa na Guzman iliibua mshangao mkubwa kwa vile mara nyingi imezoeleka kuvaliwa na walinda milango. Kwa maana hiyo, kiungo huyo analazimika kuingia kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kufanya hivyo kipindi cha nyuma.

0: Hicham Zerouali, Aberdeen
Zerouali, raia wa Morocco anayecheza nafasi ya ushambuliaji aliwahi kubadili jezi namba 10 na kuvaa jezi yenye namba 0, huku ikiwa imezoeleka kwamba mara nyingi mastraika hupenda kuvalia jezi namba 9, 10, 12, 14 na namba nyingine kama hizo, lakini yeye akapendekeza apewe jezi namba 0.
Mmorocco huyo alifanya hivyo mwaka 1999, wakati akisajiliwa na klabu ya Aberdeen akitokea Fus de Rabat na kuichezea klabu hiyo jumla ya mechi 37, akifanikiwa kufunga mabao 11, ikiwemo hat-trick dhidi ya Dundee.

1: Edgar Davids, Barnet
Mshindi wa zamani wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya akiwa na klabu ya Ajax, aliweka rekodi ya kuvaa jezi namba 1 alipohamia klabu ya Barnet. Baada ya tukio hilo alinukuliwa akisema huenda chaguo lake la jezi yake hiyo mpya ikawa na bahati ili kuepuka adhabu za kuonyeshwa kadi mara kwa mara na marefa.

2: Ossie Ardiles, Argentina
Ardiles ni raia wa Argentina aliyewahi kukipiga katika klabu ya Tottenham ya England. Aliamua kuvaa jezi mpya yenye namba mbili katika timu yake ya taifa kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.

10: William Gallas, Arsenal
Ni beki wa zamani Arsenal aliyesajiliwa na Washika mitutu hao wa London akitokea kwa mahasimu wao wa mji huo huo wa London, Chelsea mwaka 2006. Wakati wa kusajiliwa kwake aliomba klabu impatie jezi namba kumi, ingawa kwa kawaida jezi yenye namba hiyo kwa asilimia kubwa huvaliwa na wachezaji wanaocheza safu ya ushambuliaji.

16: Paulo Futre, West Ham
Futre ni nyota wa Ureno aliyetua West Ham msimu wa 1996-1997 na kuhitaji kuvaa jezi yenye namba 16 badala ya namba 10 aliyokuwa anaivaa katika klabu aliyotoka. Pia jezi yenye namba hiyo ilikuwa ikivaliwa na nyota mwingine klabuni hapo. Futre alianza kutumia jezi hiyo rasmi wakati timu yake ilipokutana na Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu.

52: Nicklas Bendtner, Arsenal
Ni straika wa zamani wa Arsenal aliyeingia kwenye orodha hii ya wabadilisha jezi za kushangaza mashabiki, baada ya michuano ya Euro kumalizika mwaka 2012. Alipotua Emirates alibadili kutoka kuvaa jezi yenye namba 26 na kuvaa 52.

69: Bixente Lizarazu, Bayern Munich
Akiichezea Bayern Munich mwaka 2005, katika nafasi ya beki wa kulia alionekana akivalia jezi yenye namba 69, ambayo ilikuwa namba kubwa sana katika namba ambazo zimeonekana zikitumiwa na wachezaji duniani kote.
Mfaransa huyo alichagua kuvaa jezi yenye namba hiyo 69 akichukua namba mbili za mwaka aliozaliwa ambapo alizaliwa mwaka 1969, huku pia uzito wake ukiwa kilo 69 na upande wa kimo chake ikiwa ni sentimita 169.

80: Ronaldinho, Milan
Ronaldinho wakati anapata uhamisho wa kutoka Barcelona kwanda AC Milan 2008, alibadili jezi ya awali aliyokuwa akiivaa akiwa Nou Camp alipotua katika viunga vya San Siro ambapo aliamua kutumia jezi yenye namba 80 badala ya namba 10 ya awali.

Akinukuliwa na vyombo vya habari, Makamu wa Rais wa Milan, Adriano Galliani Milan, alisema jezi hiyo namba 10 ilikuwa tayari inatumiwa na kiungo Mholanzi, Clarence Seedorf, ambaye pia alikuwa mchezaji wa daraja la juu. Hata hivyo, Ronaldinho hakuiomba jezi hiyo na badala yake aliomba apewe yenye namba 80, kwa mujibu wa Galliani.
Ronaldinho alichagua kupewa jezi hiyo yenye namba 80 kwa sababu ya kuzaliwa mwaka 1980 na kuungana na mastaa wengine wawili klabuni, wenye jezi zenye namba za kipekee, Mathieu Flamini (84) na Andriy Shevchenko (76).

1+8: Ivan Zamorano, Inter Milan
Straika huyu pia alibadili namba ya jezi yake kipindi anahama kutoka klabu ya Real Madrid kwenda Inter Milan mwaka 1996, hivyo akaamua kuachana na jezi namba 10 kutokana na jezi hiyo kutumiwa na Roberto Baggio klabuni hapo na yeye kuamua kutumia jezi namba tisa, ambayo ilikuwa ikisomeka 1+8.

88: Gianluigi Buffon, Parma
Mlinda mlango huyu mkongwe raia wa Italia anayekipiga katika klabu ya Juventus alianza kutumia jezi namba 88 akiwa na klabu yake ya zamani, Parma, kabla ya kubadilisha baadaye namba hiyo na kuanza kutumia jezi namba moja kama ilivyo sasa ndani ya viunga vya Turin.
Akizungumzia kitendo hicho cha kuvaa jezi yenye namb 88, Buffon alisema: “Nimechagua jezi hiyo kwa sababu inanikumbusha mipira minne, najua jamii nyingi ya Waitaliano wanajua ninachomaanisha.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here