Home Habari Mabadiliko makubwa Simba

Mabadiliko makubwa Simba

891
0
SHARE
Evans Aveva akijadiliana jambo na Hans Pope.
Evans Aveva akijadiliana jambo na Hans Pope.
Evans Aveva akijadiliana jambo na Hans Pope.

NA SAADA SALIM,

KAMA ni kujipanga Simba safari hii wameamua kujipanga vilivyo ili kuhakikisha wanarejesha heshima yao katika soka la Tanzania.

Uongozi wa klabu hiyo kwa kushirikiana na wadau wao wa karibu Jumapili iliyopita walikuwa na kikao kizito kilichotoka na maamuzi mazito ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kukiboresha kikosi chao kwani hali si nzuri na hawajafurahishwa na mambo yanayoendelea kutokea.

Uongozi huo ulikaa chini kwa saa sita katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam na kujiuliza maswali kadhaa kisha wakapata ufumbuzi kuhakikisha wanakuja na mabadiliko makubwa ili kuboresha zaidi mambo ndani ya klabu.

Wekundu hao wameshindwa kufanya vizuri kwa miaka minne na kushindwa kutwaa ubingwa na kushiriki michuano ya kimataifa hivyo hawataki hilo liendelee.

Kikao hicho kilichokutanisha watu wazito wa klabu hiyo kilijadili mada mbalimbali ikiwemo kurejesha mshikamano miongoni mwa wanachama huku ikiliangalia suala la usajili wa wachezaji na benchi la ufundi kwa mtazamo mwingine.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zilizothibitishwa na kigogo mmoja zinadai kuwa katika majadiliano hayo, kila mjumbe alitoa mawazo yake juu ya nini kifanyike na ndipo walipokuja na majibu sahihi.

Umoja

Kigogo mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho amelidokeza DIMBA Jumatano kuwa suala la umoja linapaswa kusimamiwa na Rais wa klabu Evance Aveva ambaye alitakiwa kushirikiana na wajumbe kadhaa katika kulimaliza.

“Unajua kuna misemo ambayo mababu zetu walitumia kwamba, tusigombee fito wakati tunajenga nyumba moja. Kwa kuliona hilo, kamati ya utendaji ilikutana na baadhi wa Wanasimba kwa ajili ya kuweka tofauti zao pembeni ili kurudisha umoja utakaotufanya kushirikiana kujenga timu yetu,” alisema.

Usajili

Kuhusu usajili, kigogo huyo alisema msimu uliopita walifanya makosa katika usajili, jambo ambalo hawapendi litokee tena msimu huu hivyo tayari wameamua kuurudisha mfumo wao wa zamani wa kusajili wachezaji uliokuwa ukitumika.

Katika mfumo huo wa zamani Simba ilikuwa ikiyaweka mezani majina kama matatu au manne ya wachezaji wanaocheza namba moja na kumtafuta mmoja wanayeona anafaa bila kujali kama wana uwezo wa kumnunua ama la.

“Zamani tulivyokuwa tukisajili ilikuwa ni tofauti na sasa ambapo mtu analeta jina lake tu. Tulikuwa tunaitisha majina mawili au matatu ya wachezaji wa timu tofauti tofauti kwenye nafasi moja na kisha tunayachambua na kupata jina moja tunalolisajili,” alisema kigogo huyo.

Alisema kwa hivi sasa tayari wamekwishayafanyia kazi baadhi ya majina kwani tayari Kamati ya Usajili imekwishapelekewa majina ya mabeki wa kulia watatu ambao ni Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Juma Abdul (Yanga) na Shomari Kapombe (Azam FC).

Alisema walitumia muda mrefu kuchambua wachezaji hao na mwisho wa siku jina la Kimenya limepita katika kamati hiyo na sasa linafanyiwa kazi ili asajiliwe katika kikosi cha timu hiyo.

Katika safu ya beki wa kushoto pia wameangalia wachezaji watano ambao ni kumrejesha mchezaji wao Adam Miraji, Nurdin Chona (Prisons), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Michael Aidan wa JKT Ruvu ambapo majina hayo yapo katika mikono ya kamati ya usajili kuangalia nani ni bora zaidi kati yao ambaye wana uwezekano wa kumpata.

“Pia katika nafasi nyingine kama kiungo tumewaangalia wachezaji kama Mohammed Ibrahim na Muzamiru Yasini (Mtibwa), Mbaraka Yusuf (Kagera Sugar) na Jamal Mnyate (Mwadui FC) ambao wanapaswa kusajiliwa.”

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, kigogo huyo alisema tayari kamati hiyo inayosimamiwa na Mwenyekiti wake, Zacharia Hanspope, imekwishapelekewa jina la kiungo Mzimbabwe, Knowledge Musona anayekipiga katika klabu ya K.V Oostend ya Afrika Kusini.

“Yako majina mengine ambayo bado tunayajadili lakini tayari hili la Musona (siyo anayetajwa na Yanga), ingawa kamati inaendelea kutafuta wachezaji wengine wakiwemo mastraika wawili kutoka nje na beki mmoja hatari kwa ajili ya kuboresha kikosi cha msimu ujao,” alisema.

Alisema beki ambaye anatafutwa nje ya nchi awe na uwezo wa kuzuia na kwenda mbele kuongeza mashambulizi kama ilivyo kwa Kelvin Yondani wa Yanga au David Mwantika na Pascal Wawa (Azam FC).

Kocha Mkuu

Katika nafasi ya nani atakuwa kocha mkuu, kwa mujibu wa kigogo huyo ni kwamba suala hilo bado halijafanyiwa maamuzi kwani mezani kwao yako majina ya makocha watatu, Kallisto Pasuwa (Zimbabwe), Joseph Omog, kocha aliyewahi kuifundisha Azam FC (Cameroon) na Sellas Tetteh kutoka Ghana ambaye aliwahi kufundisha klabu kubwa za nchini Rwanda na DR Congo.

“Suala la kocha hatukuweza kuzungumzia kwa vile tayari Pope (Zacharia Hanspope-Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili) yuko Zimbabwe analishughulikia hivyo tunasubiri kesho (leo) tukikutana tujue amefikia wapi,” alisema kigogo huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa vile si msemaji.

Alisema yote hayo yanafanywa kwa ajili ya kuirejesha klabu hiyo katika heshima yake ambapo msimu ujao wanahitaji kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali, hali inayowasukuma kujenga kikosi imara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here