Home Funguka/Mapenzi Mabadiliko nayo hayahitaji hasira

Mabadiliko nayo hayahitaji hasira

1253
0
SHARE

UNAWEZA kuchukizwa na tabia ya ulevi kwa mpenzi wako, pengine anakukera kwa kutokuwa na kauli nzuri, wapo baadhi wanachukizwa na jinsi wanavyopewa umuhimu wakati wa starahamu.

Yote haya yanakera na hayapendezi, maana mapenzi ni raha na maridhiano, kinyume na hapo maisha ndani ya nyumba hayawezi kunoga.

Lakini unajua kwamba baada ya kero zote hizo, unaweza kukuta zipo sababu zinazowafanya watu wakamaliza tofauti zao na kujikuta wamerudisha mapenzi tena yakawa ya moto zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.

Kufaulu huku kuna siri nyingi, lakini moja ni kubembelezana na kuwepo na mmoja anayejua jinsi ya kusuluhisha tatizo baina yao.

Waliofanikiwa katika hili ni wale walioamua kuweka hasira pembeni, wakajirudisha chini mpaka aliyemkosea mwenzake akajiona yupo juu na anathaminiwa.

Lakini siri ya yote haya ni kutaka kumaliza jambo kubwa linalokera kwa njia rahisi na isiyokera hata kidogo.

Unapoonyesha tabasamu katika jambo gumu, yaani pengine mke au mume amekosea, lakini mmoja akawa mpole anayeshauri badala ya kukemea, basi ujue suluhu katika maisha ya watu hawa huwa haiendi mbali.

Hili ni somo muhimu sana kwa wanaoishi pamoja au wenye malengo kama hayo, lakini kwa bahati mbaya wanakuwa na tabia zisizolingana.

Kinachoweza kufananisha tabia hapa si makelele, kukomoana au kila mtu kuwa mkali, endapo itatokea hivi basi hii itakuwa ni miongoni mwa zile nyumba zisizodumu au zinazokaribisha mke na mume kulala vitanda tofauti.

Tumeshuhudia baadhi ya ndoa au mahusiano yaliyodumu muda mrefu ambayo wenyewe wameyaachia yakajenga ufa na baadaye yakapasuka na kuyaacha vipande viwili.

Watu wa aina hii baadaye wanalazimika kuishi kwa mashinikizo au ya watoto au wengine kulinda rasilimali walizochuma pamoja, lakini kitu kinachoitwa mapenzi kwao unakuwa ni msamiati mgumu.

Wito wetu maalumu ni kubadili tabia na hasa kutotamani na wala usikaribishe kitu kinachoitwa kununiana, iwe na mume au mke na ikiwezekana hata jirani au rafiki yako.
Mazoea ya kusameheana kujenga furaha ya pamoja ndiyo yanayoweza kuiondoa chuki na mifarakano katika maisha na ndilo linalotakiwa liwe lengo la kila mmoja wetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here