Home Habari MABOSI SIMBA SC WAINGIA MAFICHONI

MABOSI SIMBA SC WAINGIA MAFICHONI

415
0
SHARE
  • Wafanya vikao usiku kucha

NA EZEKIEL TENDWA

MABOSI wa Simba chini ya kuimaliza AS Vita bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’, wanajua kwamba wakipata matokeo mazuri dhidi ya AS Vita Jumamosi ya wiki hii watatinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa wameamua kuingia mafichoni kuweka mambo sawa.

Mbali na kuweka rekodi kama wataweza kutinga hatua hiyo ya robo fainali, watavuna mamilioni ya fedha kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hivyo wameamua kuingia msituni kuhakikisha hawaipotezi nafasi kirahisi.

Licha ya kwamba Simba wanaburuza mkia kwenye kundi D, lakini wakiibuka na ushindi wa aina yoyote watafikisha pointi 9, zitakazowafanya kutinga robo fainali moja kwa moja.

Mpaka sasa Simba ina pointi 6 nafasi ya nne, huku JS Saoura ya Algeria wakiongoza kwa pointi 8, AS Vita nafasi ya pili wakiwa na pointi 7 sawa na Al Ahly ya Misri waliopo nafasi ya tatu, timu hizo zinapishana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa namna kundi hilo lilivyo, kila timu inaweza kutinga robo fainali kama ikipata matokeo ya ushindi, ndiyo maana Simba wanataka kumaliza biashara mapema.

Tangu juzi Jumatatu, vigogo wa Simba chini ya Mo Dewji, wameanza vikao vya mara kwa mara, lengo likiwa ni kutafuta mbinu za kuwaua wapinzani wao hao katika mchezo utakaochezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Kigogo mmoja ndani ya timu hiyo ameliambia DIMBA Jumatano kuwa, jana kulikuwa na vikao viwili vyote vikijadili namna kikosi chao kitakavyoweza kuwatoa kimasomaso Watanzania Jumamosi na kwa jinsi mambo yanavyokwenda, bila shaka Wacongo hao watarudi kwao vichwa chini.

“Mikakati ni mizito sana, timu imeingia leo (jana), lakini huku nyuma kuna vikao vizito kuweka mambo sawa, kwani kama unavyojua tukishinda tunaingia robo fainali, sasa hatutaki kupoteza nafasi hiyo.

“Tunafahamu kwamba mchezo utakuwa mgumu sana, lakini kama tuliweza tulipokutana na JS Saoura tukawafunga mabao 3-0, na tukaweza tena dhidi ya Al Ahly tukiwafunga bao 1-0, nadhani hata hawa AS Vita watakufa tu,” alisema.

Vikao hivyo vimekuwa vikifanyika maeneo mbalimbali, pia ofisini kwa Mo Dewji, lengo kubwa likiwa kuivusha salama timu yao ambayo iliwasili jana ikitokea Algeria ilikofungwa mabao 2-0 na Saoura.

Muda mfupi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege JK Nyerere, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alianza kuwaomba radhi mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla kufuatia timu yake kupoteza mchezo dhidi ya JS Saoura.

Licha ya kichapo hicho, Aussems aliahidi timu yake kupata ushindi katika mechi hiyo ya Jumamosi, akidai kwamba anafarijika kutokana na kikosi chake kutimia.

“Waliokuwa majeruhi katika kikosi change, Emmanuel Okwi na Erasto Nyoni nimeambiwa wako fiti na wanaweza kucheza, hivyo wameongeza nafasi ya kushinda kutokana na umuhimu wao.

Naye beki kisiki wa timu hiyo, Pascal Wawa, amewataka Watanzania kusubiri ushindi hiyo Jumamosi kutokana na jinsi walivyojipanga, lakini pia wakijivunia kucheza uwanja wa nyumbani.

“Hatutaweza kupoteza mechi katika uwanja wa nyumbani, tutafanya maajabu Taifa, Wanasimba msihofu,” alisema Wawa.

Kitita ambacho Simba watatia kibindoni endapo watashinda kinaweza kuwasukuma kufanya usajili wa nguvu msimu unaokuja.

Kama kwa bahati mbaya Simba wakifungwa na AS Vita au kutoka sare na kuishia hatua hiyo ya makundi, hawataondoka mikono mitupu, kwani timu yoyote inayoishia hapo inapata kitita cha Dola 550,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.2).

Wakifanikiwa kutinga na kuishia hatua ya robo fainali watalamba Dola 650,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.4), wakifika na kuishia nusu fainali watachukua Dola 875,000 (zaidi ya Sh bilioni 2), wakifungwa kwenye mchezo wa fainali watachukua Dola 1,250,000 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.8).

Wakipambana na kufanikiwa kutwaa ubingwa kama walivyoagizwa na Rais John Magufuli, wakati wakikabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watavuna Dola 250,000 (zaidi ya Sh bilioni 5.7), ndiyo maana vigogo wa timu hiyo hawataki kulala.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here