Home Michezo Kimataifa MADOGO Wa kuwaangalia msimu ujao England

MADOGO Wa kuwaangalia msimu ujao England

266
0
SHARE
Dominic Solanke

LONDON, England

KLABU zinazoshiriki Ligi Kuu ya England zimekuwa bize katika dirisha la usajili wa majira haya ya kiangazi, ambapo tayari wameshakamilisha uhamisho wa mastaa mbalimbali, wakiwemo Zlatan Ibrahimovic na Michy Batshuayi.

Hata hivyo, wachezaji chipukizi wanaokipiga katika klabu hizo kubwa hawatasahaulika pia katika mechi kadhaa za Ligi Kuu na chipukizi hao ndio hawa hapa ambao utawashuhudia katika mechi za michuano mbalimbali ambayo klabu hizi za ligi kuu zitacheza.

ARSENAL

Jeff Reine-Adelaide

Chipukizi huyu wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 18, alijiunga na Arsenal msimu uliopita akitokea Lens.

Ana uwezo wa kucheza kama kiungo wa kati na mara nyingine akitumika pembeni.

Alifanya vizuri katika michezo ya kirafiki msimu uliopita, na kiwango hicho kikampa nafasi ya kucheza michezo miwili ya Kombe la FA akiwa na kikosi cha kwanza.

Chris Willock

Kiungo mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 18, anatarajiwa kufuata nyayo za Alex Iwobi, Mnigeria aliyeonesha kiwango cha hali ya juu msimu uliopita.

Willock ameziwakilisha pia timu za taifa England mpaka ngazi ya umri chini ya miaka 17, na amefanya vizuri sana kwenye timu ya vijana ya Arsenal chini ya miaka 18.

CHELSEA

Dominic Solanke

Mchezaji huyu wa kimataifa wa England chini ya miaka 21, alifanya vizuri kiasi chake akiwa katika klabu ya Vitesse Arnhem kwa mkopo ambapo alifanikiwa kufunga mabao saba katika michezo 25 aliyoanza  msimu uliopita.

Ujio wa straika Michy Batshuayi unaweza kuwa ni nuksi kwake, kwani anataka kudhihirisha kwa kocha Antonio Conte kuwa na yeye ana uwezo wa kupambana katika kikosi cha kwanza.

Izzy Brown

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 alitokea West Brom mwaka 2013 na ameendelea kuonesha kiwango cha hali ya juu katika klabu ya Chelsea.

Na yeye pia alipelekwa kwa mkopo katika timu ya Vitesse msimu uliopita, na alifanikiwa kufunga bao moja tu, ila kutokana na kiwango chake hata kwenye timu ya taifa ni wazi kuwa dhahabu hii inangojewa kwa hamu msimu ujao.

LEICESTER CITY

Ben Chilwell

Beki huyu wa kushoto alipewa nafasi katika michezo mitatu ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa England msimu uliopita (miwili ya FA na mmoja wa Capital One).

Amehusishwa kwa kiasi kikubwa na Liverpool katika dirisha la usajili wa majira haya ya kiangazi, lakini Leicester haitaki kumwachia kinda wao huyo mwenye umri wa miaka 19 kwa sasa.

Hamza Choudhury

Kinda huyu mwenye umri wa miaka 18 anayejulikana kwa nywele zake aina ya Afro, alitolewa kwa mkopo kwenda timu ya Burton Albion msimu uliopita ambapo alicheza michezo 13 ya ligi na kuisaidia timu hiyo kupanda daraja na kutinga katika ligi ya Championship.

Kwa sasa anafanya mazoezi na kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za kirafiki na anaweza kupewa nafasi msimu ujao katika mechi za ligi na makombe mbalimbali.

LIVERPOOL

Ovie Ejaria

Kiungo huyu mwenye kipaji alinyakuliwa kutoka Arsenal na ameonesha kiwango kizuri katika timu za vijana za Liver.

Ameshacheza michezo miwili ya kirafiki akiwa na kikosi cha kwanza cha timu hiyo: dhidi ya Tranmere pamoja na dakika 45 dhidi ya Fleetwood Town mapema wiki hii.

Trent Alexander-Arnold

Kinda mwingine aliyefanya vizuri katika mchezo wa kirafiki baina ya timu yao na Tranmere, ambapo alitoa pasi ya bao pekee lililofungwa na Danny Ings.

Trent ana kasi na nguvu, na ndiyo vitu vitakavyombeba pindi atakapopewa nafasi na kocha Jurgen Klopp, anayehusudu soka la kasi na nguvu bila kuchoka.

MAN CITY

Tosin Adarabioyo

Mlinzi huyo amepitia ngazi zote za vijana England, ingawa bado hajapata nafasi ya kucheza katika mchezo wa ligi kuu.

Mabeki wote wa City hivi sasa ni wazee, na Adarabioyo huenda akapata faida kutokana na hilo, ingawa ujio unaotegemewa wa mlinzi John Stones unaweza kuwa kikwazo kwake kucheza timu ya wakubwa.

Chipukizi huyo wa miaka 18 alionesha kiwango kizuri katika kombe la vijana la FA msimu uliopita, na anaweza kupewa nafasi ya kuonesha uwezo wake katika kikosi cha kwanza pia.

Brandon Barker

Winga huo mwenye umri wa miaka 19 alicheza mchezo wake wa kwanza na timu ya wakubwa katika mchezo wa kombe la FA dhidi ya Chelsea msimu uliopita na kuna matumaini ya kumuona tena msimu ujao katika mchezo mkubwa wowote ule, lakini kutokana na City kuanza kuingia sokoni huenda akatolewa kwa mkopo.

MAN UNITED

James Weir

Weir alianza maisha yake ya soka katika timu ya Preston mahali alikozaliwa, kabla ya kujiunga na akademi ya United mwaka 2008, kipindi ambacho Sir Alex Ferguson alikuwepo kwenye benchi la ufundi.

Tangu ajiunge na timu hiyo, kiwango cha kiungo huyo mwenye uwezo mzuri wa kushambulia kimekuwa kikipanda siku hadi siku.

Ni nahodha wa timu ya vijana chini ya miaka 21 na kocha Jose Mourinho anasubiriwa kwa hamu kuonekana akimtumia chipukizi huyo ndani ya Old Trafford.

Donald Love

Kiwango cha hali ya juu alichokionesha katika kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 21, kilimwezesha apate nafasi ya kucheza katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Sunderland msimu uliopita.

Ana miaka 21 sasa na ni wakati mwafaka wa yeye kuanza katika michezo ya ligi kuu.

Beki huyu wa pembeni ambaye ana uwezo wa kucheza katikati pia, alicheza michezo nane akiwa Wigan kwa mkopo, na aliisaidia timu hiyo kucheza michezo minne mfululizo bila kufungwa bao msimu uliopita.

TOTTENHAM

Josh Onomah

Chipukizi huyu alionekana kwa mara ya kwanza msimu uliopita akiwa na kikosi cha kwanza cha Tottenham, ambapo kocha Mauricio Pochettino alimwamini na kumpa nafasi aliyoitumia vizuri.

Kutokana na soko la usajili linaloendelea hivi sasa, na Spurs ikitaka kuongeza mastaa kadhaa kwa ajili ya msimu ujao, huenda kinda huyu akatolewa kwa mkopo.

Kyle Walker-Peters

Beki huyu wa kulia ana jina linalofanana na Kyle Walker wa kikosi cha kwanza ambaye naye ni beki wa kulia.

Baada ya kinda Kieran Trippier kuonekana msimu uliopita akiwa na kikosi cha kwanza, huenda na huyu naye tukamwona msimu ujao katika michezo ya ligi kuu kama Pochettino apendavyo kuwapa nafasi chipukizi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here