SHARE

SAADA SALIM NA EZEKIEL TENDWA

AMEPONA kabisa. Winga wa Yanga, Juma Mahadhi ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha ameonyesha uwezo mkubwa katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani na kudhihirisha kuwa amepona kabisa.

Katika mazoezi hayo, Mahadhi alionyesha uwezo mkubwa sana kuanzia kuchezea mpira, kutoa pasi za uhakika na kuwasumbua mabeki kutokana na ujanja wake huku akifunga mabao ya uhakika.

Moja ya mambo yaliyowafanya mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo kufurahi ni kutokana na mabao aliyokuwa akiyafunga wakati wa mazoezi maalumu waliyokuwa wakipewa na kocha wao mkuu, Hans Van de Pluijm.

Mahadhi alifunga mabao mazuri manne katika mipira ya faulo katika zoezi maalumu walilokuwa wakipewa na kocha wao huyo huku beki wa kulia, Hassan Ramadhan ‘Kessy’ naye akionyesha umahiri wake.

Yanga wanajiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, dhidi ya Medeama ya Ghana utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mahadhi ambaye alisajiliwa na Yanga kutoka Coastal Union ya jijini Tanga, aliwaonyesha mashabiki kuwa hakusajiliwa kwa bahati mbaya baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu dhidi ya TP Mazembe.

Licha ya kwamba aliumia katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Yanga kulala kwa bao 1-0 na kushindwa kuumalizia, alikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here