SHARE

NA NIHZRATH NTANI


JIMBO la Basque lipo kaskazini mwa nchi Hispania, ambako ni karibu zaidi na nchi ya Ufaransa. Jimbo hili na lile la Catalan kwa miaka mingi yanapigania kujitenga kutoka mikononi mwa taifa la Hispania.

Kama ilivyo kwa nchi nzima ya Hispania, Jimbo la Basque limezungukwa na bahari kwa kiasi kikubwa, huku kukiwa na milima yenye kuvutia mno kwa wageni na hata wenyeji.

Katika Bara la Ulaya, Hispania ndilo taifa linaloongoza kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.

Jimbo hili la Basque, lenye wakazi wapatao 2,166,184 kwa mujibu ya sensa ya mwaka 2014, inaelezwa kuwa linaongoza kwa kuwa na ubaguzi sana tofauti na majimbo mengine.

Katika jimbo hili ndipo zinapotokea timu mbili za Athletic Bilbao na Real Sociedad, ambapo Athletic Bilbao ikionekana kuwa ni timu ya watu wa hali ya chini, huku Real Sociedad yenyewe ikiungwa mkono na watu wa hali ya kati na juu.

Sera za usajili zilikuwa zinafanana za kutosajili mchezaji anayetoka nje ya Jimbo la Basque hadi ilipofika mwaka 1989, Real Sociedad walipoachana na sera hiyo na kuweza kumsaini John Aldridge, raia wa Jamhuri wa Ireland, aliyetoka Liverpool na tangu hapo wageni wengi wamekuja na kuondoka.

Na timu hizo zinapokutana, mechi yao huwa imebatizwa jina la ‘Basque Derby,’ nyasi huwaka moto kwa muda wa dakika 90. Ni vita ya soka.

Ndani ya Jimbo la Basque ndipo ulipo mji mwingine wa pili kwa ukubwa baada ya mji wa Bilbao uitwao San Sebastian. Ni kusini mwa mji wa San Sebastian ndipo ulipo uwanja maarufu wa ‘Anoeta’, unaomilikiwa na Real Sociedad.

Kwa miaka ya karibuni uwanja huu umegeuka maarufu sana kwa wapenzi wa soka nchini Hispania na duniani kwa ujumla. Umaarufu wa uwanja huu haukuja kirahisi tu, bali kwa karibu miaka 10 sasa klabu ya Barcelona haijaweza kushinda uwanjani hapo.

Tangu utawala wa Mholanzi Frank Rijkaard klabuni Barcelona, wamepita makocha watatu hadi huyu wa nne Luis Enrique, hakuna aliyevunja rekodi hiyo. Si Pep Guardiola, wala Tata Martimo, hata hayati Tito Vilanova, hakuna aliyeibuka na ushindi uwanjani Anoeta.

Ilikuwa Mei 5, 2007 wakati tulipowashuhudia Andres Iniesta na Samuel Eto’o wakiiongoza Barcelona kuibuka na ushindi uwanjani hapo na tangu wakati huo Barcelona wamekwenda mara 8, wakipoteza mechi 5 na kutoa sare mechi 3. Ni rekodi ya kushangaza mno kwa klabu ya Barcelona.

 

KWANINI BARCELONA HAWASHINDI ANOETA?

Soka ni mchezo wenye matokeo matatu. Kuna kushinda, kufungwa na kutoa sare. Lakini kwa rekodi ya Barcelona dhidi ya Real Sociedad uwanjani Anoeta ni jambo la kushangaza mno. Ubora wa Barcelona na ubora wa Real Sociedad kuna tofauti kubwa mno baina ya hizo timu mbili.

Kitu kimoja ambacho watu wa Basque wanacho ni ile hali ya ujivuni. Kujiona wao ni bora kuliko watu wengine. Usishangae kuona watu wa Basque wakiiona Real Sociedad ni timu bora zaidi ya Barcelona au Real Madrid. Wanajiamini mno.

Si Barcelona tu wanaopata vichapo uwanjani hapo, hata Atletico Madrid nayo imeonja joto ya jiwe msimu huu, baada ya kuchapwa bao 2 kwa bila wiki chache zilizopita. Hata Real Madrid hupata shida kushinda uwanjani hapo.

Ile hali ya kucheza kwa nguvu na kujituma dhidi ya timu kubwa ni kama ambavyo ushindi dhidi ya timu hizo basi ni ushindi wa taifa zima la Basque. Na hujivunia sana jimbo lao pale wanapopata matokeo chanya dhidi ya klabu maarufu na kubwa.

Hata hivyo, Uwanja wa Anoeta, unachukua watazamaji 32,076, mara tatu ya idadi ya watazamaji wanaoingia uwanja wa FC Barcelona wa Nou Camp.

Miongoni mwa viwanja viwili vikubwa nchini Hispania katika eneo la kuchezea wachezaji ni Anoeta na Vicente Calderon pekee unaomilikiwa na Atletico Madrid.

Utofauti wa viwanja hivi huja katika vipimo. Viwanja hivi vina vipimo vya urefu wa mita 105 na upana ni mita 70. Vipimo vikubwa zaidi kuliko viwanja maarufu vya Santiago Bernabeu, San Mames, Nou Camp na Mestalla.

Kitu kingine kinacholeta tofauti uwanjani Anoeta ni ile hali ya umbali kati ya watazamaji wakiwa majukwaani na eneo la uwanja wanaochezea wachezaji. Hii inatokana na kuwepo kwa sehemu zinazotumika kwa michezo ya riadha. Hali hiyo huleta hali ya ubaridi sana uwanjani hapo. Huleta ugumu kwa wachezaji ambao hawajazoea hali hiyo.

Hali inayoikuta FC Barcelona mara zote wanapokutana na Real Sociedad ni hali ambayo iliwahi kuikuta Real Madrid dhidi ya Deportivo La Coruna.

Iliwachukua Real Madrid miaka 18 kuanzia 1991 -2010 kuweza kuibuka na ushindi katika dimba la Riazor, linalomilikiwa na Deportivo la Coruna.

Hata kile kikosi kilichoonekana bora cha ‘Galactico’s hakikuweza kuvunja rekodi hiyo.

Kuanzia 2007 hadi sasa FC Barcelona inasifika kwa kuwa na takwimu bora za umilikaji wa mpira, iwe wamefungwa, wameshinda au wametoa sare.

Lakini takwimu zao huwa tofauti inapokuja mechi dhidi ya Real Sociedad. Mara zote Real Sociedad huibuka na alama nyingi za kumiliki mpira (Ball Possession). Ni ajabu lakini ndio ukweli.

Ingawa wameweza kutawala ‘La Liga’ kwa miaka 8 iliyopita, huku wakiwa na rekodi bora ya kushinda katika viwanja vyenye timu zinazoonekana kuwa imara kama Vicente Calderon, Santiago Bernabeu, Mestalla, Juan Sanchez Pijuan, lakini hali huwa tofauti wanapokwenda Anoeta.

Wahenga walinena kila mtu na mbabe wake. Mbabe wa FC Barcelona ni Real Sociedad na katu usicheze kamari kuipa ushindi Barcelona wanapokutana na wanaume hawa wa Jimbo la Basque wakiwa uwanjani kwao Anoeta.

Wikiendi hii ni EL CLASICO. Dunia itasimama kwa dakika tisini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here