SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

VITA ya kuwania ufungaji bora imezidi kunoga huku wachezaji watatu; Heritier Makambo wa Yanga, Meddie Kagere wa Simba na Salim Aiyee, wakishikana mashati kisawasawa.

Katika msimamo wa wafungaji bora Makambo na Salim Aiyee wa Mwadui, ndio wanaoongoza kila mmoja akiwa na mabao 12 huku Kagere akifuatia na mabao yake 11.

Licha ya kwamba Kagere anayo mabao 11, lakini kasi yake inawatisha wapinzani wake hao kwani amekuwa na mfululizo mzuri wa kufunga karibu kila mchezo unaomjia mbele yake.

Kingine kinachowatisha zaidi wapinzani wake hao ni kwamba, Simba wamecheza michezo michache tofauti na timu nyingine na kama ataendelea kufunga hiyo inamaanisha anaweza akawaacha mbali zaidi.

Kagere alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Azam FC, mchezo uliochezwa Ijumaa ya wiki hii, mabao ambayo yalimsogeza na kuwapumulia Makambo na Aiyee.

Kama atafunga dhidi ya Lipuli Jumanne ya wiki ijayo Uwanja wa Samora mkoani Iringa, atawakuta wawili hao na huenda akawapita endapo atafunga zaidi ya bao moja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here