Home Makala MAKOCHA WALIOSEPA NA KURUDI KUZINOA KLABU ZAO ZA ZAMANI

MAKOCHA WALIOSEPA NA KURUDI KUZINOA KLABU ZAO ZA ZAMANI

524
0
SHARE

 

NA MAREGES NYAMAKA


MOJA kati ya vivutio vilivyoongeza chachu maradufu katika soka ni pale mchezaji anapotundika daluga na kufungua ukurasa mpya wa ukocha na baada ya muda fulani anarejea katika klabu yake aliyoichezea akiwa na majukumu mengine ya kuhudumu katika benchi la ufundi.

Pia katika kundi hilo kuna baadhi ya makocha ambao hawakucheza mahali hapo, bali waliajiriwa kama makocha moja kwa moja, ikatokea wakatupiwa virago, lakini baada ya muda fulani wanashawishiwa kurejea na kufanya kazi katika kitengo hicho hicho.

Miongoni mwa makocha walioula katika pande zote mbili hizo kucheza na kufundisha (nenda rudi), hususan katika Ligi Kuu England ni Kenny Dalglish, aliyewahi kuichezea Liverpool na baadaye kukalia benchi la ufundi kwa nyakati tofauti, ingawa aliporejea msimu wa 2011/12 hakufanya vizuri katika nafasi hiyo kama ilivyotarajiwa.

Ifuatayo ni orodha ya makocha walioondoka na kurejea mahali hapo hapo.

 

Kevin Keegan, Newcastle United

Miaka aliyofundisha 1992-1997 na 2008

Kevin Keegan aliiongoza vyema Newcastle katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya  England mwaka 1997, ingawa baadaye walijikuta wanafanya vibaya katika mechi za ugenini mzunguko wa pili, ambapo taji lilinyakuliwa na Arsenal.

Hata hivyo, msimu uliofuata Keegan aliachia ngazi na kutimkia Fulham, akidai utawala wa juu ambao ulikuwa ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi, Dennis Wise, ulikuwa ukiingilia majukumu yake, ikiwamo kufanya usajili bila kumshirikisha.

 

Kenny Dalglish, Liverpool

1985-1991 na 2011-2012

Dalglish aliwasili kwa mara ya kwanza katika viunga vya Anfield akiwa kama kocha mwaka 1985 na kufanikiwa kuiongoza Liverpool kutwaa taji la ubingwa wa Kombe la Ligi msimu huo na baadaye akafanya hivyo tena miaka ya 1988 na 1990.

Mscotland huyo alidumu kwa Majogoo hao wa Anfield kwa miaka sita kuanzia 1985 hadi 1991, kabla ya kurejea mahali hapo msimu wa 2011-12 kuchukua nafasi ya Roy Hodgson, ingawa kipindi hicho Dalglish hakufanya vizuri sana kama ilivyokuwa awali, hali iliyopelekea kutupiwa virago kutokana na timu kufanya vibaya, ikimaliza ligi kwa kushika nafasi ya nane kwenye msimamo.

 

Francesco Guidolin, Palermo

2004-05, 2006-07, 2007 na 2007-08

Francesco, kocha wa hivi sasa wa klabu ya Swansea City ya England, mara ya mwisho kuinoa timu yake ya zamani aliyoichezea, Palermo, ilikuwa ni 2007-08. Aliamua kujiuzulu mwenyewe kutokana na matokeo mabovu yaliyomwandama kwenye kikosi chake mfululizo.

Kocha huyo mwenye mapenzi makubwa na klabu yake hiyo, alinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema imetosha na hatarajii kwa mara nyingine kuajiriwa na Palermo kama  kocha, kwani anaangalia zaidi mbele kufundisha klabu nyingine.

 

Nigel Pearson, Leicester City

2008-2010 na 2011-2015

Pearson alibahatika kuinoa Leicester City mwaka 2008, kipindi hicho ikishiriki Ligi Daraja la Pili (League One) na kufanikiwa kuipandisha hadi katika Ligi Daraja la Kwanza (Championship).

Lakini kocha huyo 2010 alionyeshwa mlango wa kutokea, ambapo alichukiliwa na Hull City kabla ya kurejea King Power 2011- 2015.

 

Jose Mourinho, Chelsea

2004-2007 na 2013-2015

Jose Mourinho ni kocha mwingine katika Premier League aliyerejea kupiga mzigo ndani ya  klabu yake ya Chelsea, aliyowahi kufanya nayo kazi kipindi cha nyuma.

Mourinho aliiongoza The Blues 2004, akijipachika jina la ‘Special One’ , ikiwa ni miezi michache tu tangu aipe FC Porto taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Akiwa Stamford Bridge, Mourinho alifanikiwa kwa kasi ndani ya misimu miwili akiipa Chelsea Ubingwa wa Ligi Kuu England, kabla ya kuwepo tofauti kati yake na bosi wa klabu, Roman Abromovic, hatua iliyomfanya Mreno huyo mwaka 2008 kuamua kutimka na kuelekea viunga vya San Siro, kwa ajili ya kuinoa Inter Milan ya huko na baadaye Real Madrid.

Baada ya kuinoa Real Madrid kwa muda wa miaka mitatu, Mourinho aliamua kurejea tena jijini London kuwanoa The Blues mwaka 2013 na kuwaongoza vema kiasi cha kufanikiwa kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa mara nyingine.

Hata hivyo, baadaye alijikuta akikumbwa na upepo mbaya wa timu kufanya vibaya msimu uliofuata na kumfanya kutimuliwe, ambapo alipata ulaji katika jiji la Manchester, anapoinoa timu ya Manchester United hadi hivi sasa.

 

Fabio Capello, Real Madrid

1996-1997 na 2006-2007

Capello, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England, inaelezwa kuwa mapenzi yake makubwa hadi leo ni klabu ya Real Madrid ya Hispania, alikoondoka na kurejea kuifundisha kwa nyakati tofauti.

Kwa kifupi Capello ni miongoni mwa makocha waliopata mafanikio makubwa ndani ya dimba la Santiago Bernabeu.

Raia huyo wa Italia aliiwezesha Real Madrid kushinda Ligi Kuu Hispania, maarufu kama La Liga mwaka 1997, lakini mwaka 2007, huku akiwa amezungukwa na mastaa kibao kama akina Fabio Cannavaro, David Beckham na Ruud van Nistelrooy, alishindwa kufanya vizuri na nafasi yake kuchukuliwa na Bernhard Schuster Julai 9, mwaka huo.

Tony Pulis, Stoke City

2002-2005 na 2006-201

Tony Pulis mafanikio yake makubwa akiwa na kikosi cha Stoke City kwa misimu tofauti, ilikuwa ni mwaka 2011 alipoweza kufikia hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la FA, huku taji likienda Etihad, Manchester City ikiibuka na ushindi wa bao 1-0.

Awali Pulis akiwa na miaka mitatu klabuni hapo, timu hiyo ilifanya vibaya sana, huku mashabiki wakitupa lawama kwa uongozi wa klabu chini ya mmiliki Gunner Gilsons, kutokana na kuyumba kwa uchumi na kushindwa kufanya usajili wa kina, kabla ya hivi sasa uwepo wa kampuni ya Bet365.

 

 

Harry Redknapp, Portsmouth

2002-2004 na 2005-2008

Portsmouth ilikuwa klabu ya tatu kwa Harry Redknapp kuifundisha akitokea West Ham United na kuanza kazi rasmi katika viunga vya Frott Park na kudumu mahali hapo kwa misimu miwili, kabla ya kuvutwa kwa mara nyingine msimu wa 2005-2008, ambapo alifanikiwa kushinda Kombe la FA.

Katika mechi ya fainali ya michuano hiyo ya Kombe la FA, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cardiff City, kwenye Uwanja wa Wembley na nyota wa mchezo akiwa Nwanko Kanu.

 

Vittorio Pozzo, Italia

1912, 1921, 1924 na 1929-1948

Pozzo aliiongoza timu ya taifa ya Italia kwa vipindi vinne tofauti, mara ya mwisho kabisa ikiwa ni mwaka 1948.

Katika muda wote huo, kocha huyo anajivunia rekodi tamu ya kuwapa Waitaliano Kombe la Dunia pekee katika ardhi yao hiyo ya nyumbani, kwa kuibamiza Hungary 1938.

Muitaliano huyo hadi anaachana na masuala ya ukocha, hakuwahi kufundisha soka nje ya nchi yake, kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.

Kabla ya kupewa kibarua cha kuinoa timu ya taifa, Pozzo aliwahi pia kuzinoa timu za Torino na Inter Milan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here