Home Michezo Kimataifa MAKONDA UMEWASIKIA HAWA? WACHEZAJI 13 ENGLAND WANATUMIA DAWA ZA KULEVYA

MAKONDA UMEWASIKIA HAWA? WACHEZAJI 13 ENGLAND WANATUMIA DAWA ZA KULEVYA

588
0
SHARE

LONDON, England

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anawachukia sana wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya na kuthibitisha hilo, ameanza operesheni ya kutokomeza dawa hizo.

Wakati huu tukiendelea kuona majina ya vigogo yakiripoti Kituo Kikuu cha Polisi, makala haya yanakueleza namna dawa za kulevya zinavyoleta madhara kwenye mchezo wa soka.

Mpaka sasa wachezaji 13 wanaocheza kwenye Premier League wamebainika kutumia dawa za kulevya aina ya cocaine, japo Chama cha Soka nchini humo (FA) kimegoma kuweka majina yao hadharani.

Uamuzi huo wa FA umekuja ili kuwalinda wachezaji hao wasiathirike kisaikolojia wanapoanza kutumia dawa.

Hili limekuja baada ya hivi karibuni nyota wa Stoke City, Saido Berahino, kufungiwa wiki nane baada ya kugundulika akitumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Adhabu hii imekuja siku chache baada ya Stoke kukamilisha uhamisho wa Berahino kutoka West Bromwich Albion.

FA wamepewa dhamana hii ya kuendesha upimaji na Serikali ya England na wanaamini mpaka kufikia mwaka 2018,  watakuwa wameshawafanyia vipimo wachezaji 5,000.

Mpaka sasa mchezo wa soka ndio unaoongoza kwenye zoezi hili kuliko michezo mingine nchini England.

Matukio haya yanakumbusha nyota watano waliowahi kutuhumiwa kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Kolo Toure

Mwaka 2011, Kolo Toure, alifungiwa miezi sita kwa kosa la kutumia vidonge vya ‘diet’ alivyokuwa akitumia mkewe.

Beki huyu raia wa Ivory Coast, aliyewahi kukipiga katika klabu ya Liverpool, mwaka 2015 aliwahi pia kupimwa na kubainika anatumia dawa za kusisimua misuli.

Edgar Davids

Edgar ‘The Pitbull’ Davids, miongoni mwa viungo bora kuwahi kutokea duniani aliyewahi kukipiga kwenye klabu za Ajax, Milan, Juventus, Barcelona, Inter na Tottenham.

Alicheza pia mechi 74 akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Uholanzi.

Mwaka 2001 akiwa Juventus, aliwahi kufungiwa miezi minne baada ya kugundulika kuwa anatumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Pep Guardiola

Pep Guardiola alifungiwa miezi minne mwaka 2001, baada ya kugundulika kuwa anatumia madawa hayo.

Kocha huyu wa Man City na kiungo wa zamani wa Barcelona, alipinga kesi hii na miaka sita baadaye alishinda.

Lakini ajabu, miaka miwili baadaye, mwaka 2008 kesi hiyo ilifunguliwa tena kabla ya Pep kushinda tena mwaka 2009 na kusafisha jina lake.

Adrian Mutu

Historia si rafiki wa Adrian Mutu. Wengi wamemsahau nyota aliyefanya matumizi makubwa ya pesa kuingia kwenye mchezo wa soka.

Baada ya kufunga mabao 22 kwenye michezo 36 ya Seria A, nchini Italia akiwa na Parma msimu wa 2002/03, Mutu alitajwa kuwa kinda hatari zaidi duniani.

Agosti 2003, Chelsea waliilipa Parma zaidi ya dola milioni 25 kwa ajili ya kuipata saini ya mkali huyu kutoka Romania.

Ikiwa ni sehemu ya kuijenga upya Chelsea kama ilivyoazimiwa na bilionea wa klabu hiyo, Roman Abramovich, Mutu aligundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu mwaka 2004.

Kosa hilo likampelekea kukumbana na adhabu ya kifungo cha miezi saba. Baadaye alirejea nchini Italia ambapo mwaka 2010 tena alifanyiwa vipimo na kugundulika tena kutumia madawa.

Akiwa Italia, alifungiwa miezi sita na kushindwa kurejea tena kwenye ubora wake baada ya kumaliza kifungo hicho.

Tabia yake nje ya uwanja imekuwa chanzo kikubwa cha kumaliza kipaji kikubwa cha nyota huyu aliyewahi kutabiriwa makubwa wakati akichipukia kule Italia.

Diego Maradona

Mara tatu ambazo Diego Maradona alifanyiwa vipimo vya matumizi ya madawa yaliyopigwa marufuku michezoni, alikutwa na hatia.

Hakuna anayeweza kubisha, Maradona anabaki kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea ulimwenguni lakini ziko tabia ambazo kwa namna moja au nyingine zilikatisha safari yake kisoka haraka mno.

Machi, 1991 alipimwa na kugundulika, kitendo kilichopeleka kupewa adhabu ya kufungiwa miezi 15 na kumaliza ufalme wake katika ardhi ya Italia alioutengeneza akiwa na jezi ya Napoli.

Mwaka 1994, kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na Argentina alipimwa na kunaswa akiwa mtumiaji wa madawa hayo ambapo alipewa adhabu ya miaka 15 kutojihusisha kabisa na soka.

Kipimo cha mwisho Maradona kilikuwa mwaka 1997 na hapa ndipo alipomaliza rasmi mpira wake. Kwenye mahojiano aliyoyafanya mwaka 2008, Maradona alisema: “Hivi mnajua ningekuwa mchezaji wa aina gani kama nisingekuwa natumia cocaine (dawa za kulevya)? Tumepoteza mchezaji mkubwa sana na ninajutia siku zote kwa kuwa najua ningekuwa mkubwa zaidi ya hapa!”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here