SHARE

NA WINFRIDA MTOI

KITENDO cha kufanya majaribio katika timu ya Kuala Lumpur Rovers ya nchini Malaysia, kumempa mchongo mpya straika wa Lipuli FC, Paul Nonga ambaye tayari ameaga kikosini hapo.

Nonga alikwenda kufanya majaribio hayo ya wiki mbili za Januari mwaka huu, lakini alishindwa kujiunga moja kwa moja na timu hiyo kutokana na kubanwa na mkataba wa Lipuli.

Straika huyo anayefukuzana na Meddie Kagere katika ufungaji akiwa na mabao 11, licha ya kutoweka wazi kama anakwenda kujiunga na timu hiyo aliyofanya majaribio, lakini alikiri kuwa msimu ujao hatakuwepo Lipuli.

Akizungumza na DIMBA jana, Nonga, alisema  majaribio aliyofanya japo ni siku chache, yamemuongezea kitu katika kazi yake na kumfanya akue zaidi kisoka.

“Tangu nimeanza kucheza soka, nimekuwa nikizinguka tu katika klabu mbalimbali za hapa nchini, sikujua huko nje kuko vipi, lakini nilikwenda kufanya majaribio Malaysia nimeona kuna utofauti kubwa katika soka.

“Hali niliyokutana nayo kule, imenifanya niongeze kitu katika kazi zangu, kikubwa ni kupambana na kujiamini, naamini msimu ujao nitakuwa wa tofauti na sasa,”alisema.

Alieleza kuwa  tayari ameshawaaga  viongozi wa Lipuli na kuwaambia watafute straika mwingine wa kuziba pengo lake,  hata hivyo hajaweka wazi sehemu anayokwenda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here