Home Makala Malimi Busungu: Mwambusi ananichukia, naondoka

Malimi Busungu: Mwambusi ananichukia, naondoka

598
0
SHARE
Malimi Busungu

NA ZAINAB IDDY,

KUMEKUWAPO na maswali mengi kuhusu wapi alipo straika wa Yanga, Malimi Busungu na kama yupo kwanini hachezi. Mashabiki wa Yanga wanakumbuka uwezo wa kupachika mabao alionao Busungu na raha aliyowahi kuwapa msimu uliopita wakati timu hiyo ilipoifunga Simba mabao 2-0.

Busungu nyota wa zamani wa Mgambo Shooting kwa sasa ni mmoja ya wachezaji wenye wakati mgumu ndani ya kikosi cha Yanga, akiwa amewekwa kando baada ya kuingia katika mahusiano mabaya na benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na kocha Hans van Pluijm.

DIMBA limefanikiwa kukutana naye uso kwa uso na kuweza kuzungumza naye juu ya kinachomsibu kiasi cha kushindwa kupata nafasi ya kucheza wakati huu Yanga ikiwa katika vita ya kupambania kutetea taji lake la ligi kuu.

DIMBA: Pole na majeraha kwanza uliyoyapata wakati Yanga ikishiriki mashindano ya kimataifa.

Busungu: Asante, nashukuru kwa sasa niko fiti baada ya kupata matibabu ya kutosha.

DIMBA: Licha ya kuwa fiti kama unavyosema kipi kinakusibu ambacho kinasababisha usiweze kupata namba ndani ya Yanga tangu mwanzo msimu huu.

Busungu: Ni changamoto tu za mpira kwani benchi la ufundi linajua sababu za kuniweka  jukwaani nibakie kuwa mtazamaji badala ya kucheza. Nipo fiti nafanya mazoezi ya nguvu muda wote lakini sielewi tatizo nini.

DIMBA: Kuna taarifa kuwa vitendo vya utovu wa nidhamu hasa ulevi ndiyo chanzo cha kushuka kwa kiwango chako na kusababisha usielewane na viongozi wa benchi la ufundi na kujikuta ukisugulishwa benchi hili lina ukweli gani?

Busungu: Si kweli, kwani ingekuwa tatizo ni ulevi kama inavyodaiwa mazoezini nisingekuwa naambiwa nafanya vizuri ninachoona sina nyota na kocha msaidizi Juma Mwambusi ambaye ndiye mshauri wa kocha mkuu Hans van der Pluijm.

DIMBA: Kwanini unasema huna nyota, je, ulishawahi kukwaruzana na Mwambusi?

Busungu: Sijawahi kufanya hivyo labda kama nilimkosea nikiwa sijui ni kosa na kama yeye ni mzazi alipaswa kuniambia na si kuniwekea visasi vinavyosababisha kushindwa kupata nafasi katika timu, lakini iwapo nimemkosea natumia nafasi hii kumuomba msamaha.

DIMBA: Msimu huu tangu uanze umeshindwa kucheza mechi hata moja lakini pia haupo pamoja na timu kwanini?

Busungu: Niliamua kuachana na kikosi tangu tuliporejea Zanzibar tulipokwenda kuweka kambi kwa ajili ya mechi dhidi ya Simba, ila ni masuala ambayo tayari tulishayazunguza na uongozi wa juu hivyo sitopenda kuyazungumzia.

DIMBA: Kama mlishayamaliza imekuaje bado haupo na kikosi wakati huu timu ipo katika vita kali ya kutetea taji lake?

Busungu: Ilikuwa niungane na timu mara baada ya wao kurudi kutoka Kagera, lakini niliposikia kocha Hans amejiuzulu mwili na akili yangu vilikufa ganzi hivyo nikajikuta nashindwa kwenda.

DIMBA: Huoni kama utakuwa umepingana na uongozi wako wa juu ambao walikwambia uende ukaungane na timu?

Busungu: Kabla ya kuamua kukaa niliwaeleza juu ya hofu yangu ya kwenda kuwa pamoja na timu ikiwa chini ya Mwambusi, walinambia wanayafanyia kazi masuala yangu lakini baada ya kusikia amerudi nafikiri nitakwenda kuwa pamoja nao baada ya mechi dhidi ya Mbao FC.

DIMBA: Je, ukirudi bado unaimani utapata nafasi ya kucheza?

Busungu: Sina uhakika na hilo kwani nimeshakata tamaa na nina amini mipango na uwezo wangu ulivurugika baada ya kuondoka Mkwassa, kiukweli alikuwa mwalimu asiye na kinyongo na anayependa kuona kila mmoja wetu anaisaidia timu na ndio maana kipindi chake haikuwa rahisi kuona mchezaji anasugua benchi pasipo sababu za msingi hususani kuwa na tatizo la kiafya.

DIMBA: Mwenzako Paul Nonga alipoona hana namba aliamua kuomba kuondoka, je, wewe unasubiri nini kufanya hivyo?

Busungu: Jambo alilofanya Nonga ni jema sana, ila kila jambo lina wakati wake nami muda utafika siku si nyingi.

DIMBA: Ina maana kuwa dirisha dogo likifunguliwa utaomba kuondoka?

Busungu: Kila mchezaji anahitaji kucheza ili aweze kukuza kipaji chake pamoja na kuongezeka thamani, sasa mimi sina nafasi kwanini niendelee kuwepo, ila tusubiri muda ukifika nitaeleza msimamo wangu.

DIMBA: Je, utaomba kutolewa kwa mkopo au utavunja mkataba?

Busungu: Nahitaji kuondoka nikiwa huru kwa maana ya kila mmoja afe na chake.

DIMBA: Kipi unachowashauri wachezaji ambao wanatamani kuzichezea timu kubwa hususani Yanga?

Busungu: Kabla ya kuamua hilo wafikirie mara mbili, lakini pia wanahitajika kuwa wavumilivu ili waweze kuishi.

DIMBA: Tukitoka nje ya Yanga, unafikiri kuondoka kwako na Fullu Maganga pamoja na kocha Bakari Shime ndiko kulikoishusha daraja Mgambo Shooting?

Busungu:  Ni kweli hiyo ni sababu kubwa na iwapo kama kocha Shime akirudi kuifundisha nina hakika itarudi kwenye kiwango chake kwani yule si mtu wa kuyumbishwa.

DIMBA: Je, ni nani ambaye amechangia hadi Watanzania wakafahamu kuna mchezaji anaitwa Busungu na hata Yanga kukuona.

Busungu: Ni kocha Shime, kwangu ni zaidi ya baba, alinilea na kunikemea kama mwanawe pale anapoona nafanya vitu ambavyo vitaharibu mfumo wa maisha yangu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here