Home Makala MALINZI ANASTAHILI KUENDELEA KUWA RAIS WA TFF AMA LA?

MALINZI ANASTAHILI KUENDELEA KUWA RAIS WA TFF AMA LA?

497
0
SHARE

WAKATI chaguzi za soka za mikoa mbalimbali zikiendelea kufanyika nchini kote kwa ajili ya kuwapata viongozi mbalimbali watakaviongoza kwa kipindi kijacho, tayari vuguvugu la uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), utakaofanyika mwakani limeanza kupamba moto.

Wadau mbalimbali wa soka nchini wameanza maandalizi yao kwa ajili ya uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika mwakani, ambapo wapo walioanza kutajwa kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

Kati ya hao, yupo Rais wa sasa, Jamal Malinzi, ambaye ameonyesha nia kubwa ya kusimama tena kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi huo, ingawa kuna baadhi ya majina mengine makubwa yanatajwa.

Hata hivyo, Malinzi ameanza kujiandaa vema akisimama kuitetea nafasi yake ili kuendelea kuisongesha Taasisi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini.

Tangu Malinzi aingie madarakani mwaka 2013, utawala wake umekuwa ukipokea shutuma nyingi kutoka pande mbalimbali za wadau wa soka.

Wengi wa wadau hao wamekuwa wakimkosoa kila mara, huku wengine wakihoji uwezo wake kiuongozi, uadilifu na umakini wake na wasaidizi wake katika shughuli ya usimamizi wa mchezo huu pendwa kuliko yote hapa nchini.

Mambo kama kashfa za rushwa na upangaji matokeo, tuhuma za ukabila, matumizi mabaya ya fedha, ubabe kwa kufungia wapinzani wake na mengine yanayofanana na haya ndiyo ambayo utawala huu umekuwa ukihusishwa nayo.

Ilifikia watu kuona Malinzi na wenzake wameturudisha kipindi cha FAT ya akina Ndolanga na Rage.

Lakini katikati ya haya yote, kuna kitu kiko dhahiri, nacho ni mafanikio ya kisoka katika miaka hii ya TFF chini ya Malinzi kuliko vipindi vingi tu huko nyuma.

Na ili wadau tutende haki, ni lazima tuzungumzie mambo haya kwa nia ya kumpima kimizani badala ya kukosoa tu siku zote.

Wakati watu wakiendelea kumkosoa, Malinzi yeye amejibu kwa vitendo zaidi, ambapo katika utawala wake soka la Tanzania limepata mafanikio kadhaa.

Kwanza ni katika kipindi ambacho Azam FC imeweza kuwa bingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Yanga imekuwa klabu pekee katika eneo la Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la soka barani Afrika, huku ikizitimulia vumbi timu nyingine zote za ukanda huu.

Pia katika kipindi hiki timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’ imeweza kutwaa kibabe ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), huku timu ya vijana wenye umri wa miaka chini ya 17 ‘Serengeti Boys’ ikikaribia kufuzu kushiriki fainali za vijana za CAF.

Aidha, kuna wanaodai kwamba, kwa hivi sasa ushindani ndani ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeendelea kuimarika na kupungua kwa malalamiko dhidi ya waamuzi, huku pia zikianzishwa ligi ya vijana na ile ya wanawake ambazo hazikuwepo.

Ni ukweli, si mafanikio ya maana sana, lakini kwa nchi ambayo tumekuwa tukiambulia patupu karibu kila michuano ya soka tunayoshiriki, angalau kuna kitu kinaonekana, hasa tunapoanza kuwa wababe kwa wanyonge wenzetu wa Cecafa.

Ukiwa kama mdau wa soka nchini na mfuatiliaji mzuri wa masuala hayo, unadhani Malinzi anastahili kuendelea kuisimamia TFF kwa miaka mingine minne ijayo?

Tuma maoni yako, ukianzia na jina lako kamili na mahala ulipo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here