SHARE

Na Joseph Shaluwa

UKITAKA kuoa lazima uwe makini. Ukweli ni kwamba kuna sifa nyingi za mwenzi sahihi. Baadhi ya sifa hizo ni umpende kwa dhati, akupende, akuvutie, awe na tabia njema, akubalike, atoke familia yenye maadili n.k.

Lakini vijana wa sasa huhadaika zaidi na mvuto wa sura na maumbile ya mtu wakifanya kama kipimo kikuu cha anayefaa kuwa mwenzi wa maisha, ni makosa.

Uzuri wa nje pekee si kati ya sifa muhimu zaidi za kumfanya awe na sifa za kuwa mwenzi wako wa maisha. Mapenzi huanzia moyoni, jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako.

Kumbuka kuwa unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana mbinguni na duniani, ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu, si vinginevyo!

Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, hayajaribiwi wala kujaribika! Pia, lazima umchunguze kama penzi lake ni la dhati.

Katika mada zangu mbalimbali nimekuwa nikiainisha sifa za mpenzi mwenye mapenzi ya dhati, lakini kwa kukukumbusha kidogo ni kwamba, anayekupenda huwa mvumilivu, anakusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako, anayekuheshimu na kutambua thamani yako.

Anayetakiwa kuwa mwenzi wako wa maisha lazima awe makini na mwenye akili za kimaisha. Si lazima awe na elimu ya darasani, haijalishi ni mwanamke aliyekulia kijijini au mjini, lakini hapa tunaangalia uwezo wake wa kufikiri.

Hata hivyo, inategemea wewe umepanga kuishi na mwanamke wa aina gani, lakini mwanamke ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa kutosha wa kufikiri na kupambanua mambo.

Mwenye uwezo huu ni yule ambaye ukimwambia una matatizo fulani, anakuwa mstari wa mbele kukusaidia kwa hali na mali. Mtu anayepokea mambo kwa kusikitika, hana maana kwamba anakupenda.

Anatakiwa kukupa mbinu. Lazima uwe na mtu mwenye mbinu. Mwenye uwezo wa kufikiri na kupambanua mambo.
Asiye sahihi utampima hata kwa vitu vidogo tu, si wa kujishughulisha, anaishia kupiga mizinga kila siku!

Asipokuambia kuhusu simu, atasema vocha, atahitaji kununuliwa nguo, pafyumu na vitu vingine vinavyofanana na hivyo. Hawezi kuzungumzia mambo ya maendeleo. Hana mawazo chanya.

Mawazo yake yanaishia kwamba wewe ni kila kitu kwake, akutegemee kwa kila kitu – akuchune. Hawezi kuwa mwenzi sahihi, hata kama ana uzuri wa kiwango gani. Mwanamke wa aina hii unapaswa kumchunguza mapema ili usije ukaoa mzigo!

Suala la uwezo wa kufikiri lina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya sasa, ni bora mkakosa mali lakini mkawa na uwezo wa kufikiri na kutatua matatizo mbalimbali ya kimaisha.

Ni vyema pia ukajiridhisha, ni mwanamke wa ndoto yako? Unatakiwa kujiuliza juu ya uliyotarajia kwake, ni kweli unayapata yote? Hapa kuna vipengele viwili ndani ya hiki kimoja, kabla ya uhusiano na ndani ya uhusiano.

Nikianza na kabla ya uhusiano, hapa namaanisha kwamba, ana sifa zote ambazo ulikuwa unatarajia kwa mpenzi wako ajaye, ambaye ndiye huyo unayetarajia kuingia katika uhusiano naye?

Ni kweli ana kila kitu kinachokuvutia kiasi kwamba hutathubutu kumsaliti? Ukishajiridhisha na hilo, unaweza kuingia katika uhusiano lakini si kwa kiasi kikubwa, hapa namaanisha kwamba, unaingia katika kipindi cha urafiki ambacho huweki kila kitu wazi, hivyo katika kipindi hiki utaweza kujua kama unapata kile ulichotarajia.

Chunguza tabia zake kwa makini katika kipindi hiki, toka naye katika matembezi ya pamoja, huku ukiwa umemweka katika kipimo ambacho hata yeye mwenyewe atakuwa hafahamu.

Lazima mwisho utaweza kugundua kwamba, chaguo lako lilikuwa sahihi au la. Lingine lenye msingi, anatakiwa awe mtu wa kujali.

Hata kama ni mzuri kiasi gani, ana mvuto kiasi gani, anakubalika na marafiki zako kiasi gani, lakini vyote hivyo vinaweza kupoteza maana kama hataonyesha anavyojali thamani yako wewe kama mpenzi wake.

Ninapozungumzia kujali, ninakuwa nimekwenda mbali zaidi, anavyojali familia yako, marafiki na hata wewe mwenyewe! Hutakiwi kuwa na mwanamke ambaye akili yake haiwazi chochote juu ya maisha.

Mwanamke anapaswa kuwa makini, akili ziwe zinafanya kazi sawa sawa na awe na mchango mkubwa wa mawazo kwenye familia. Sifa ya mvuto wake, inaweza kuharibiwa na kukosa uchangamfu na unyenyekevu.

Mwanamke hata kama ni mzuri kwa kiwango gani, akipoteza sifa hizi, uzuri wake ni kama unakuwa umepungua. Kuna suala la uchangamfu pia.

Uchangamfu huu uanzie kwako, asiwe mwanamke mkimya kupitiliza, hali ambayo inaweza kutafsiriwa kwamba anaringa!

Lakini pia, uchangamfu huu anatakiwa auonyeshe hata kwa rafiki zako pamoja na ndugu zako. Mwanamke mwema ni yule mwenye unyenyekevu kwa mumewe pamoja na ndugu zake.

Marafiki, uzuri wa mwanamke hauna maana ya ubora wa kuwa mke. Si kila mwanamke anaweza kuwa mke. Wengine ni wanawake tu. Mchunguze kwa makini kabla ya kufikia uamuzi wa kumwingiza kwenye maisha yako.

Usikose kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA, kipo kwenye hatua za mwisho kabla ya kuingia mitaani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here