SHARE

NA WINFRIDA MTOI

YANGA imeanza kufanya kweli katika hatua za kuanza ujenzi wa kituo chao cha soka kwenye eneo la Kigamboni walilokabidhiwa mwaka jana baada ya Kamati ya Ujenzi na Miundombinu kuanza mchakato, huku ramani ikiwa tayari imepatikana.

Hivi karibuni, kamati hiyo ilitembelea Uwanja wa Azam Complex ambao kwa sasa upo katika marekebisho kupata uzoefu kwa uongozi na kuelewa wanachosema mainjinia wanaouboresha uwanja huo.

Wanajangwani hao wanataka wakiingia katika mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo ambao mchakato wao umeanza, tayari wawe wameanza kuweka mambo sawa ya ujenzi wa uwanja.

Uwanja ambao Yanga wanatarajia kujenga, inasemekana itauzidi hata ule wa watani wao Simba, uliopo Bunju kwa ukubwa.

Akizungumzia lilipofika suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli, alisema wajumbe walikwenda kutembelea Azam FC kujifunza utaratibu wa kutengeneza miundombinu ya viwanja.

Alisema wajumbe hao wa kamati ambao wengi wao wana taaluma ya uinjinia, wameanza mchakato wa ujenzi kwa kufanya maandalizi mbalimbali na utafiti.

“Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi na Miundombinu ya Yanga, walitembelea Uwanja wa Azam Complex kujifunza juu ya miundombinu ya viwanja, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya ujenzi wa uwanja wetu uliopo Kigamboni, Dar es Salaam,” alisema Bumbuli. 

Yanga imekuwa haina uwanja wa mazoezi kwa miaka mingi hususan baada ya kuharibika ule wa Kaunda kutokana na eneo la Jangwani kujaa maji mara nyingi.

Hivyo endapo uwanja huo utakamilika, itaondoa adha ya kukodi viwanja vya mazoezi kama ilivyo kwa Simba ambao sasa wanamiliki uwanja wao, Simba Mo Arena, wenye viwanja viwili vya nyasi bandia na kawaida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here