Home Makala MAN UNITED WAKO ‘SIRIAZ’ NA NEYMAR?

MAN UNITED WAKO ‘SIRIAZ’ NA NEYMAR?

429
0
SHARE

MANCHESTER, England

HABARI kubwa inayopamba vichwa vya habari vya magazeti ya michezo barani Ulaya ni taarifa ya Manchester United kujiandaa kuvunja rekodi ya dunia kwa kumsajili Neymar.

Bila shaka habari hii imewagawa katika pande mbili mashabiki wa soka, wako wanaoamini huenda ikawa kweli na wako wanaoona ni tetesi tu za kuuzia magazeti kama ilivyokuwa kwa Sergio Ramos.

Kweli Jose Mourinho yuko ‘siriaz’ na usajili huu? Makala haya yamejaribu kuchimba kwa undani zaidi kwenye suala hili ili kupata majibu ya kuridhisha.

“Unaweza kutegemea baadhi ya vitu kutoka kwa Ashley Young. Ni mchezaji mzuri lakini hajafika ubora wa Neymar.”

Unaikumbuka kauli hii?

Ilikuwa ni kwenye maandalizi ya msimu wa mwaka 2015, wakati aliyekuwa kocha wa United, Louis va Gaal, alipowachana wachezaji wake kwa kukosa kasi kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kauli hiyo kutoka, Man United wamefanya usajili wa wachezaji wengi kwa lengo la kuboresha safu yao ya ushambuliaji tu.

Wamemsajili Anthony Martial, kinda Marcus Rashford, alipandishwa kikosi cha kwanza. Mwanzoni mwa msimu huu wakawanasa pia Henrikh Mkhitaryan, Paul Pogba na Zlatan Ibrahimovic.

Lakini bado kwa kupima uwezo wa nyota hao, bado hakuna aliyeweza kuingiza ubora uliokuwa unalengwa na Van Gaal na pengine ndiyo sababu iliyofanya kuamua kuvunja benki na kumsajili Neymar.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Hispania, inadaiwa kuwa United wako tayari kutoa Euro 200 (sawa na pauni mil 172) kwa ajili ya kuvunja mkataba wa Neymar.

“Jose Mourinho, binafsi amezungumza na Neymar kumshawishi aachane na Barcelona na kutua Old Trafford.

“Inadaiwa Jose amemshauri Neymar kujiunga na United ni jambo bora kwenye maisha yake ya soka kwa kuwa ataishi bila kivuli cha Lionel Messi na kutengeneza historia yake binafsi.

“Pia Mourinho amezungumza na wakala wa mchezaji na kumwambia kuwa United watalipa Euro milioni 200 yote bila kuhitaji punguzo lolote lakini pia watamfanya Neymar kuwa mchezaji anayelipwa ghali zaidi duniani.”

Hivyo ndivyo ilivyosomeka habari hiyo kwenye magazeti ya Hispania.

Lakini ni kweli United wako tayari kulipa kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo? Na je, Neymar yuko tayari kweli kuachana na Barcelona? Bado maswali haya hayajapatiwa majibu, tuendelee.

United wana ubavu huo wa pesa?

Imeripotiwa kuwa United wako tayari kulipa kiasi cha pauni milioni 172 kwa ajili ya kuvunja mkataba wa Neymar. Ikumbukwe hii ni mara mbili zaidi ya kiasi walicholipa kwa Paul Pogba mwanzoni mwa msimu huu, pauni milioni 89.

Mara ya mwisho usajili ghali wa dunia kuvunjwa kwa kupishana mara mbili zaidi ni mwaka 1968, Juventus walipolipa pauni 500,000 kwa ajili ya Pietro Anastasi na kuizima rekodi ya Roma waliomnunua Montova kwa pauni milioni 250,000.

Bila shaka utakuwa uhamisho utakaoshtua wengi, lakini tusisahau kuwa kuna sababu za msingi zinazoweza kufanya hili litokee.

Kama unatumia kiasi cha pauni milioni 172 kuvunja mkataba, bila shaka unategemea kumpa mchezaji mkataba usiopungua miaka mitano ambao ni sawa na kufanya matumizi ya pauni milioni 34 kwa mwaka.

Hapa sasa United wataanza kuitumia faida ya biashara ya matangazo inayopanda kwa kasi kwenye mchezo wa soka.

Wakimpata Neymar bila shaka watakuwa na mchezaji anayeuzika ‘brand’ na itakuwa rahisi kwao kuingiza matangazo makubwa kupitia jina lake.

Unaweza kuona hili kwa kuufuatilia usajili wa Pogba ulivyokuwa. United walilipa fedha nyingi za usajili lakini baadaye waliingia mikataba mikubwa kuanzia haki za matangazo ya televisheni, wakapiga pesa ndefu na sasa wanakimbizana na Real Madrid kwa utajiri duniani.

Kama mkurugenzi wao wa michezo, Richard Arnold, alivyowahi kusema mwaka jana:

“Sikilizeni, wote mnajua kuwa wachezaji wakubwa ndio wanaotakiwa kucheza kwenye klabu yetu kwa ajili ya kutufanya kuwa bidhaa kubwa sokoni.”

Kwa sababu hii, United wanaweza kujilipua na kumwaga pesa kumsajili Neymar, ambaye tayari anafahamika na kupendwa na watu wengi duniani.

Ni wazi kuwa Neymar atakuwa mchezaji mashuhuri zaidi Premier League na pengine kuwafunika mpaka Messi na Ronaldo, hii ni kutokana na nguvu ya matangazo ya Ligi ya England iliyojiwekea duniani.

Lakini kweli Neymar atapenda kujiunga na Manchester United?

“Premier League ni ligi inayonishangaza sana. Napenda aina yao ya uchezaji na klabu za pale. Na nani anajua siku moja naweza kucheza pale. Nazipenda sana Manchester United, Chelsea, Arsenal na Liverpool, hizi ni timu kubwa ambazo mara zote huwa zinapambana kushinda.

“Pia England kuna makocha wakubwa kama Mourinho na Guardiola, watu ambao kila mchezaji ana ndoto za kufanya nao kazi.”

Alisema haya Neymar wiki iliyopita.

Unaweza kusema kuwa kauli hii inaonyesha kuwepo kwa uwezekano wa nyota huyu kutoka Nou Camp na kutua Old Trafford.

Lakini tunatakiwa kufahamu kuwa Barcelona msimu huu wanapambana kubeba La Liga na Ligi ya Mabingwa huku United wakipambana kuingia ndani ya ‘top 4’, kikwazo cha kwanza kinaanzia hapa.

Hata hivyo, kwa ushawishi wa pesa, United wanaweza kufaidika na uwepo wa Neymar kwenye kikosi chao kutokana na ubora aliokuwa nao.

Kwenye ushindi wa bao 6-1, Barcelona walioupata dhidi ya PSG, ni Neymar ndiye aliyekuwa nyota wa Nou Camp, akiwafunika Messi na Luis Suarez.

Na pia rekodi ya kufunga mabao 51 kwenye michezo 76 akiwa na Brazil, inaweza kuwaondolea mashaka United kuwa Neymar anaweza kung’ara bila uwepo wa nyota wakubwa kwenye kikosi.

Na hakuna muda mwingine wa United kumsajili Neymar zaidi ya huu, unajua kwanini? Mabingwa wa Ufaransa, PSG wameendelea kummezea mate Lionel Messi na endapo wakija kufanikiwa kumnasa ni wazi kuwa Barca watakuwa wazito kumtoa Neymar.

Achana na hayo, tutazame ishu ya mshahara. United wameahidi kumlipa Neymar kiasi cha pauni 415,000 kwa wiki na kumfanya Mbrazil huyu kuwa mchezaji anayelipwa ghali zaidi nchini England, lakini kuwa United kuna faida kubwa zaidi ya mshahara.

Unakumbuka mwaka 2009 wakati Manchester City walipojaribu kumsajili Ricardo Kaka kutoka AC Milan? Walikwenda na maneno mazuri zaidi ya ofa nono ya mshahara

Mkurugenzi wao wa ufundi, Garry Cook, alisema: “Tunaamini kuwa Kaka ni bidhaa kubwa kwenye ramani ya soka, sisi tuko tayari kumsaidia na kumfanya ajitangaze zaidi na zaidi.”

Hii ipo kwa United pia. Ukifika pale unapewa fursa ya kujitengeneza jina lako na kufanya mazungumzo binafsi na makampuni makubwa.

Paul Pogba hivi sasa anapiga pesa za mitandao akiingia dili la kutengeneza ‘emoji’ yake binafsi, hivyo kuendelea kupata fedha nje ya mshahara wake.

Mwaka 2014, makamu wa rais mtendaji wa United, Ed Woodward, alieleza kuwa, “Di Maria alitafutwa mara 12 zaidi mtandaoni alipotua hapa akitokea Real Madrid.

“Radamel Falcao jina lake lilitafutwa mara 10 zaidi tulipomsajili ukilinganisha na alivyosajiliwa na Atletico. Tukumbuke pia Daley Blind, aliiongeza asilimia 50 ya malipo yake na mtandao wa Twitter tulipomsajili kutoka Ajax.”

Barcelona hawako vizuri sana kwenye upande wa matangazo ya kibiashara na ndio maana haikuwa ajabu kuona Januari mwaka huu, United ikirejea kileleni kwa kuingiza mapato ya pauni milioni 515.3 kwa msimu wa 2015-16. Barca walishika nafasi ya pili kwa mapato ya 463.4.

Hivyo Neymar ana fursa ya kukuza zaidi jina lake kibiashara kama atajiunga na Manchester United.

Je, ana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Man United?

Swali zuri na rahisi. Si Martial au Rashford mwenye uwezo wa kumweka Neymar benchi, akicheza kwa kutokea upande wa kushoto.

Kama United wakimpata Neymar, wakawa tena na Mhenrikh Mkhitaryan na Antoine Griezmann, bila shaka watakuwa na safu kali ya ushambuliaji itakayosimama nyuma ya Zlatan Ibrahimovic.

Kwa maelezo hayo, huenda kweli United wako siriaz na usajili huu wa Neymar na kuna sababu za msingi za kisoka na kibiashara zitakazoweza kumfanya Mbrazil huyu atue Old Trafford.

Tusubiri, wakati utakuja na jibu sahihi juu ya habari hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here