SHARE

CLARA ALPHONCE NA EZEKIEL TENDWA         |          


HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba leo mwenyekiti wao Yusuph Manji, atakuwa jukwaani kushuhudia kikosi hicho kikicheza dhidi ya USM Alger.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watawakaribisha Waarabu hao ikiwa ni mfululizo wa michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, hatua ya makundi.

Yanga wapo kundi D katika michuano hiyo wakiwa na pointi moja tu katika michezo minne waliyocheza huku Gor Mahia ya Kenya wakiongoza kwa pointi 8 sawa na USM Alger wanaoshika nafasi ya pili huku Vital’O ya Burundi wakiwa nafasi ya tatu na pointi zao mbili.

Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano wa Yanga, Hussein Nyika, ameweka wazi kuwa juzi usiku walikutana na kiongozi wao huyo na kufanya naye mazungumzo na mwisho akawathibitishia kuwa atakuwa ni moja ya mashabiki wa klabu hiyo watakaohudhuria mchezo huo leo.

“Jana (juzi) tulikuwa na kikao na Mwenyekiti wetu (Manji), tumeongea naye mambo mengi lakini kwa sasa sidhani kama ni muda mwafaka kuyaweka wazi ila ninachoweza kusema ni kuwa atakuwepo kwenye mchezo wa kesho (leo).

“Na leo usiku (jana) atakutana na wachezaji kwa ajili ya chakula cha usiku na kuzungumza nao kwa lengo la kuwapa hamasa ili waweze kufanya vizuri katika mchezo wetu dhidi ya USM Alger,” alisema Nyika.

Alisema mbali na Manji, wanatarajia kuwa na ugeni mzito wa  Mkuu wa majeshi ya Tanzania, Venance Mabeyo, kama  mgeni rasmi kwenye mchezo huo wa kulinda heshima, utakaoanza saa 10 jioni.

 

Manji alijiuzulu Uenyekiti wa Yanga SC Mei mwaka jana, lakini mkutano wa wanachama wa Juni 10, mwaka huu ulimkatalia ombi hilo wakidai bado wanayo imani kubwa na yeye.

Viongozi wa Yanga walifanya jitihada za kukutana naye lakini tangu wakati huo alikuwa kimya na sasa huenda ikawa njia ya bilionea huyo kuamua kurudi upya na kuisaidia timu hiyo ambayo imeyumba kiuchumi.

Mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wana hamu kubwa kumwona mwenyekiti wao huyo, wakitaka kusikia kauli yake juu ya kutengua maamuzi ya kujiuzulu.

Akizungumzia mchezo huo, Msemaji wa Yanga, Dismas Ten, alisema timu yao ipo kamili kwa ajili ya mchezo huo na kwa mujibu wa daktari wao, Edward Bavu, hakuna mchezaji aliye majeruhi hata mmoja hiyo ikimaanisha kuwa wapo tayari kwa mapambano.

Alisema baada ya kambi ya siku 14 mkoani Morogoro, timu yao ilirejea jana kwa ajili ya mchezo huo wakiwa chini ya kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera, ambaye leo kwa mara ya kwanza ataliongoza benchi la ufundi katika mchezo huo.

Yanga ilianza michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 4-0 na U.S.M. Waarabu hao kabla ya kulazimishwa suluhu ya 0-0 na Rayon Sports Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na baadaye kufungwa mfululizo na Gor Mahia, wakianza kupigwa mabao 4-0 nchini Kenya na kukubali tena kipigo cha mabao 3-2 Uwanja wa Taifa.

Wanajangwani hao wanatakiwa kupambana na kushinda ili kujiwekea heshima tu, kwani hata wakishinda michezo yao miwili iliyobakia hawawezi kufikisha pointi nane walizonazo Gor Mahia na Waarabu hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here