Home Michezo Kimataifa MAPENZI NI ZAIDI YA KUAMBIWA UNAPENDWA! – 2

MAPENZI NI ZAIDI YA KUAMBIWA UNAPENDWA! – 2

676
0
SHARE

NA JOSEPH SHALUWA,

THAMANI ya pendo la kweli halipo katika kinywa pekee, matendo
yakizungumza ndiyo hudhihirisha kile kilichopo moyoni. Yapo mambo ya
kujifunza ili kuweza kuwa na uhusiano bora.

Ndiyo mada tunayoijadili hapa ambayo nilianza nayo wiki iliyopita. Ni
muhimu kutambua na kuthamini penzi la kweli la mwenzi wako. Ukilijua
hilo, maana yake utaijua nafasi yako kwa mwenzako na kuisimamia vema.

Usipojitambua hutaona thamani ya mapenzi, hutaona umuhimu wako kwenye ndoa. Muunganiko wenu hautakuwa wa maana kama hutatambua thamani yako.

Lazima mwanamke asimame katika nafasi yake na mwanamume  asimamie
nafasi yake. Kuna baadhi ya watu wakishaingia kwenye ndoa wanaona kila
kitu kimeshaisha. Hawaoni umuhimu wa kufikiria kuwa bora zaidi kwenye
ndoa.

Ndugu zangu, nyumba hujengwa tena hujengwa kwa umakini wa hali ya juu.
Huwezi kumuona mwenzako mpya kama wewe  hujaonyesha upya katika mambo
yako. Mvute mwenzi wako ili akuone kweli unahitaji kuwa mpya, hapo
utatengeneza nafasi kwake ya kubadilika kwenye nyendo zake.

TAFUTA FURAHA YA MWENZAKO

Kati ya mambo yanayoharibu ndoa ni pamoja na kugombana mara kwa mara.
Kuna wengine huwa hawawezi kuzungumza sana, kama umemkosea, ataishia kukwambia mara mbili au tatu, baada ya hapo anaamini umeelewa.

Ikitokea ukajua umekosea na mwenzi wako amekujulisha au ukamuona hana
furaha, ni jukumu lako kuhakikisha furaha yake inarejea tena.
Mpeleleze, jichunguze ni wapi umekosea? Haraka sana unachukua hatua
ya kurekebisha makosa yako. Usiruhusu mwenzako kuwa amenuna muda wote
kwa sababu yako. Tafuta amani yake.

KUWA MWEPESI KUOMBA MSAMAHA

Hakuna kitu kinachoumiza kama mmoja anapokosea na akajua mwenzake
anajua kuwa amekosea halafu aache kulipa uzito tatizo hilo. Binadamu
tumeumbwa na maumivu moyoni. Ikiwa mwenzako amekukosea na akabaki
kimya, maumivu yake huwa mara mbili.

Mwingine anaweza kufikia hatua ya kuzungumza na mwenzake kuhusu tatizo
husika akitarajia mwenzi wake atamsikiliza na pengine kukaa chini na
kujadiliana pamoja lakini inakuwa kinyume chake.

MSISIMKO WA MAHABA

Rafiki zangu, usishangazwe na tatizo la msisimko wa mahaba. Ni
kutokana na makosa ambayo unayafanya kwenye uhusiano wako. Wakati
mwingine, unaweza kuwa chanzo au mwenzi wako akasababisha hilo
kutokea.

Hali hiyo ikitokea, kamwe usiwaze kuhusu kuachana. Achana na fikra za
talaka, si kwamba umemchukia mwenzi wako, si kweli kuwa mapenzi ndiyo
yanakuwa yameisha. Mapenzi yapo moyoni, hivyo kamwe usiwaze kuachana
kunapotokea matatizo ya namna hiyo kwenye uhusiano.

NINI CHA KUFANYA?

Jambo la kwanza kabisa kuliingiza ubongoni mwako ni ufahamu kuwa
tayari kuna tatizo katika ndoa yenu. Tatizo ambalo linahitaji utatuzi
wa haraka.

Katika utatuzi wenyewe, kunawahitaji wote lakini ikitegemea zaidi
upande wako kwa sababu tayari umeshagundua kuna tatizo.

(i) Chunguza tatizo

Lazima ujichunguze, angalia nyumba yako kwa makini. Mchunguze mwenzi
wako, kisha ujue ni wapi kwenye makosa. Kujua chanzo ni mwanzo wa
kuelekea kwenye kutafuta ufumbuzi.

(ii)  Badilika

Inawezekana wewe ndiye uliyekosea, yamkini pia ni mwenzi wako ndiye
mwenye makosa, vyovyote ilivyo, kikubwa cha kuzingatia hapo ni kwamba,
tayari mpo kwenye matatizo ambayo wewe umeshayagundua na upo tayari
kuyasahihisha.

Badilika kifikra. Kama ulikuwa una majibu mabaya kwake, anza kumjibu
vizuri. Hata kama yeye ndiye mwenye makosa, haijalishi maana hapa sasa
unatafuta amani ya nyumba yenu. Mtazame kwa picha tofauti, ondoa fikra
za upungufu wa msisimko kwake.’

Matayarisho ya akili yatakusaidia wakati ukielekea kwenye kutafuta
suluhu ya kudumu ya tatizo lako/lenu.

Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo.

Jiandae kusoma kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA
kitaingia mitaani hivi karibuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here