SHARE

NA NIHZRATH NTANI JNR


KUNA wanadamu wamezaliwa kuja kuwa mashujaa. Hili haliwezi kupingika. Wakati fulani unaweza kufanya jambo kwa maslahi yako, lakini likaja kuwa jambo lenye manufaa kwa jamii nzima.
Hata hivyo, jambo hilo hilo ulilolifanya linaweza kukufanya uwe shujaa kwa upande mmoja na kuonekana adui kwa upande mwingine. Hivi ndivyo wanavyoonekana wanaume hawa wawili.

JE, UMEPATA KUISIKIA SHERIA YA BOSMAN?

Mtu huyu aitwaye Jean Marc Bosman anaweza kuwa mmoja wa wanadamu wanaoweza kutajwa katika historia ya soka duniani.
Bahati mbaya jina la Jean Marc Bosman haliimbwi inavyostahili midomoni mwa mashabiki wengi wa soka duniani.
Marc Bosman hana thamani machoni mwa mashabiki wengi wa soka duniani. Alipata kuwa mwanasoka enzi zake, lakini si kwa kiwango cha juu mno hata apate hiyo thamani?
Jina la Bosman linaweza kuwa likiendelea kuchukiwa na wamiliki wa klabu za soka duniani. Lakini kwa wanasoka wengi, mtu huyu anaonekana ni shujaa miongoni mwao.
Mnamo mwaka 1990, Jean Marc Bosman akiwa na miaka 25 tu wakati huo, mkataba wake na klabu ya RFC Liege ya Ubelgiji ulikuwa umefikia tamati.
Ni wakati huo alipoamua kujisajili na klabu ya Dunkergue ya Ufaransa, akiamini yeye ni mchezaji huru.
Pamoja na kumaliza mkataba, klabu ya RFC Liege ilimzuia kujiunga na klabu yake mpya mpaka walipwe kiasi cha Pauni 500,000 za uhamisho wake.
Kabla ya mwaka 1990, klabu zilikuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu mchezaji pale tu anapomaliza mkataba.
Hakuna mchezaji aliyeruhusiwa kuhama bila kulipiwa ada ya uhamisho. Ni klabu tu ndizo zilikuwa na wajibu wa kuamua kumuacha aondoke bure pale inapotaka kufanya hivyo.
Jambo hili halikumfurahisha sana Marc Bosman.

Katika kupambana na sheria hizi kandamizi, mwanadamu huyu alikuja kufungua kesi katika mahakama ya makosa ya jinai ya Ulaya.
Kesi hii ilikuja kufunguliwa mnamo mwaka 1993 na kupata usajili namba 415/93. Mlalamikaji, Marc Bosman, aliwakilishwa na wanasheria, akiwamo Jean Louis Dupont na mwenzake, Luc Mission.
Washtakiwa katika kesi hii ni klabu ya RFC Liege, Chama cha Soka cha Ubelgiji na Chama cha soka cha Ulaya (UEFA). Bosman aliitaka mahakama itoe haki kwa mchezaji anayemaliza mkataba wake awe huru kujiunga na klabu yoyote bila gharama zozote za uhamisho kwa ridhaa yake, huku pia akizitaka mahakama ziruhusu klabu kuwa na wachezaji wageni zaidi ya watatu. Tofauti na wakati huo, walikuwa wanaruhusiwa watatu tu.
Mpaka kufikia Desemba 15, 1995, mahakama ilimpa ushindi Bosman. Bahati mbaya sheria aliyoipigania haikuweza kumnufaisha.
Alikuwa tayari ameshastaafu soka akiwa na miaka 30 tu. Baada ya kesi hiyo ndipo jina la Bosman lilipoanza kuandikwa vitabuni.

Leo hii watu tunasema kwa sheria za Bosman, basi mchezaji yupo huru kwenda klabu yoyote baada tu ya kumaliza mkataba wake.
Maamuzi ya Bosman yanamuweka katika pande mbili. Upande wa wachezaji, wanamchukulia ni shujaa na upande wa wamiliki wanamuona ni adui.
Kwa wakati huu akiwa na miaka 52 sasa, Jean Marc Bosman angali anajivunia sana kitendo hicho alichokifanya zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kauli ya ‘Nenda zako usingoje shukrani’ inapotimia.

UMEZISIKIA GHARAMA ZA UHAMISHO ZA WACHEZAJI NYAKATI HIZI?

Zinashangaza, zinahuzunisha na mwishowe zinaogopesha. Neymar ametua kunako klabu ya PSG kwa kiasi cha Euro milioni 222. Ni ngumu kuamini hili. Lakini ndivyo ukweli halisi ulivyo.
Sahau kuhusu Neymar. Klabu ya Barcelona baada ya kumuuza Neymar, imetumia kiasi cha pauni milioni 94 kumsainisha Ousmane Dembele kutoka Borrusia Dortmund.
Inashangaza, kwa kiasi kikubwa kilicholipwa kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 20 tu, huku pia akipata kucheza mechi 32 na kufunga mabao 6 tu. Soka linakwenda wapi?
Zikiwa zimebakia siku takribani mbili kabla dirisha la usajili barani Ulaya kufungwa, jina la Kylian Mbappe linaweza kutingisha katika usajili wake kwenda PSG au Real Madrid. Muda utazungumza.

NYUMA YA MATUMIZI HAYA YA FEDHA, YUPO FLORENTINO PEREZ.

Akiwa na miaka 70 hivi sasa, mtu huyu anatambulika kama kiongozi wa klabu ya soka aliye maarufu zaidi duniani. Hakuna shabiki wa soka asiyelifahamu jina la Florentino Perez.
Mwanadamu huyu kama alivyo Jean Marc Bosman wanatajwa kufanya mapinduzi makubwa ya wanasoka. Ni kama anavyochukuliwa Bosman midomoni mwa wacheza soka na wamiliki.
Kabla ya mwaka 2000, gharama za uhamisho wa wanasoka wengi zilikuwa chini ya Euro 45 milioni. Ujio wa Perez klabuni Real Madrid kulikwenda sambamba na umwagaji pesa uliokithiri.
Siku chache tu baada ya kushinda urais wa Real Madrid, alimnunua Luis Figo kutoka Barcelona kwa ada ya Euro milioni 56, ada ambayo ilikuwa rekodi ya dunia kwa wakati huo.
Mwaka mmoja baadaye alikubali kulipa Euro 75 milioni kwa ajili ya Zinedine Zidane kutoka Juventus kwenda Real Madrid. Uhamisho uliokuja kuvunja rekodi ya Luis Figo.
Rekodi ya Dunia ya Zinedine Zidane ilikaa kwa miaka minane na kuja kuvunjwa na Cristiano Ronaldo kwa ada ya Euro 94.4 milioni.
Miaka minne baadaye, yaani mnamo mwaka 2013, Gareth Bale alinunuliwa kwa Euro 100.8 milioni kutoka Tottenham kwenda Real Madrid, ada iliyokuja kuvunja rekodi ya Cristiano Ronaldo.
Uhamisho wa wachezaji wote hawa nyuma yake alikuwapo mwanadamu huyu anayeitwa Florentino Perez. Huyu ndiye sababu ya wachezaji wengi kuhamishwa kwa gharama kubwa nyakati hizi.
Mpaka sasa watu wanaamini kuwa Gareth Bale hakuwa na thamani ya kiasi kilicholipwa kwa ajili yake ukilinganisha na uwezo wake dimbani. Watu wanaweza msamehe kwa Luis Figo, Zidane, Cristiano Ronaldo, lakini si kwa Gareth Bale.
Ndipo pia uhamisho wa Paul Pogba uliokuja kuvunja rekodi ya Bale kutoka Juventus kwenda Manchester United kwa kiasi cha Euro milioni 105 na kuleta mshangao mkubwa na ubishani miongoni mwa mashabiki wengi wa soka duniani. Paul Pogba hakustahili kulipiwa kiasi cha pesa ile ukilinganisha na uwezo wa umahiri wake dimbani.
“Usipoziba ufa utajenga ukuta,” wahenga walipata kunena. Walimruhusu Perez kufanya atakavyo katika soka. Na sasa hakuna budi kukubaliana na hali hii.
Muda tu. Lakini miaka michache ijayo tunaweza kumsikia mtu akihamishwa kwa kiasi cha Euro 500 milioni. Hakuna tutakachokifanya zaidi ya kubakia tukishangaa kama tunavyoshangaa sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here