Home Makala Marcus Rashford Ndiyo alama anayoweza kukumbukwa Van Gaal

Marcus Rashford Ndiyo alama anayoweza kukumbukwa Van Gaal

272
0
SHARE
Marcus Rashford

NA EZEKIEL TENDWA,

BINADAMU hata afanye mazuri kiasi gani, lakini hakosi mabaya yake ambayo atakumbukwa nayo. Vilevile binadamu huyohuyo hata afanye mabaya kiasi gani lazima kuna watakaomkumbuka kwa mazuri hata kama ni machache.

Ni kama Watanzania wengi tunavyoamini kuwa Idd Amin ‘Dada’ ni mtu mbaya sana, lakini wapo wengine wanamuona ni shujaa. Wapo wanaoamini kuwa kifo cha Osama Bin Laden ni halali, lakini wapo ambao mpaka leo wanalaani mauaji yake wakiamini alionewa.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwenye soka, kwamba wapo wachezaji na makocha ambao wanaweza wakafanya kazi nzuri lakini wakajitokeza baadhi wakaponda, pia wapo baadhi yao wanaweza wakafanya vibaya, tena vibaya sana, lakini nyuma yao kuna watu wanaowaunga mkono hata kama si wengi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa mashabiki walio wengi wa Manchester United hawataki kusikia jina la David Moyes likitajwa masikioni mwao, lakini kuna wachache sana ambao watakuambia kocha huyo angepewa muda zaidi angeweza kufanya mambo makubwa ndani ya kikosi hicho.

Ndivyo ilivyo hata kwa Arsenal, ambapo wapo mashabiki kibao wanaona umefika muda wa kocha wao, Arsene Wenger, kuachia ngazi kutokana na kikosi hicho kukosa ubingwa kwa muda mrefu, lakini kama itapigwa kura atapata zake kadhaa za wanaotaka aendelee kufundisha.

Kama ambavyo idadi kubwa ya mashabiki wa United hawataki kabisa kusikia habari za Moyes, hivyo hivyo hawataki jina la Louis Van Gaal, litajwe ingawa yapo mazuri ambayo hata mashabiki hao wamponde kiasi gani watamkumbuka nayo.

Ingawa mashabiki hao wanamlalamikia kocha huyo kwa kushindwa kufanya kile ambacho walikuwa wamekitarajia, lakini ukitaja tu jina la Marcus Rashford, lazima wamkumbuke kwa jinsi alivyomuibua mchezaji huyo.

Rashford licha ya kwamba ana umri mdogo, lakini amekuwa akifanya mambo makubwa uwanjani pale anapopewa nafasi, mfano mzuri ikiwa katika mchezo wa Ligi Kuu nchini England mwishoni mwa wiki iliyopita, Mashetani hao Wekundu walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Hull City.

Wengi walidhani mchezo huo utamalizika kwa suluhu ya 0-0, kwani dakika zilikuwa zinayoyoma, lakini Rashford akatokea huko alikotokea na kufunga bao dakika za lala salama, akiunganisha vizuri krosi ya nahodha wake, Wayne Rooney na kuwafanya kuondoka na pointi tatu muhimu.

Mbali ya kufunga bao hilo, alionyesha uwezo mkubwa kwa dakika ambazo alicheza na kudhihirisha kuwa kama kocha wake wa sasa, Jose Mourinho, ataendelea kumuamini, bila shaka mashabiki wa kikosi hicho watafaidi matunda yake.

Rashford hana mwili mkubwa kama ilivyo kwa akina Didier Drogba, lakini ni mpambanaji, haogopi kukatiza mbele ya msitu wa mabeki wenye maumbo makubwa.

Uwezo wake ndiyo unaowafanya wengi wapige kelele anapowekwa benchi na kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika mchezo huo dhidi ya Hull City, ni wazi atakuwa amemshawishi vya kutosha kocha wake kuendelea kumtumia michezo inayokuja.

Mchezo unaokuja Manchester United watapambana na mahasimu wao wa jiji moja, Manchester City, Uwanja wa Old Trafford ambapo kwa vyovyote Rashford anaweza akapata namba hata kama ni kuingia kipindi cha pili, kwani kazi aliyoifanya mchezo uliopita inatosha kabisa kujitambulisha kwa kocha wake kuwa ni mpambanaji.

Ukweli utaendelea kubakia palepale kwamba hata kama Van Gaal hatakumbukwa kwa mengine, lakini mashabiki wa United watakapomwangalia Rashford na mambo ambayo anayafanya lazima warudishe mioyo yao nyuma na kuangalia nani aliyemtoa chini na kumpandisha juu. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here