SHARE

LONDON, England

TIMU ya Taifa ya England imeanza vizuri harakati zake za kufuzu michuano ya Euro 2020, kwa kuibamiza Jamhuri ya Czech mabao 5-0, katika mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki hii.

Matokeo hayo ni mwendelezo wa kiwango maridhawa kinachooneshwa na timu hiyo tangu ilipoanza kuwa chini ya kocha, Gareth Southgate, ambaye aliwaongoza pia kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia, England walifanikiwa kunyakua zawadi ya mshindi wa tatu, nyuma ya Croatia na mabingwa, Ufaransa,  wakionekana kubadilika na kucheza soka la ushindani zaidi.

Nguvu yao hiyo ilionekana pia katika mchezo wa juzi dhidi ya Czech, uliomalizika kwa nahodha, Harry Kane, kufunga bao la penalti, huku Raheem Sterling akiingia kambani mara tatu.

Kiwango cha Sterling kiliwakuna mashabiki wengi wa England, lakini ni Kane, ambaye alionesha kufurahia mno mabao ya winga huyo wa Man City, kwani amepata msaidizi wa kubeba mzigo wa kufunga mabao uliokuwa ukimwelemea.

Katika kikosi cha wachezaji 25 wa England ambao waliitwa na Southgate, Kane ndiye mwenye mabao mengi kuliko wote (21), akifuatiwa na Sterling (7) ambaye alifikisha idadi hiyo baada ya ‘hat trick’ dhidi ya Czech.

Straika wa Man Utd, Marcus Rashford, yeye alikuwa anashikilia nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi (6) nyuma ya Kane, lakini Sterling amempiku kwa kufikisha mabao saba.

“Nadhani timu yoyote ya taifa inayotaka kuwa imara ni lazima iwe na wachezaji wanne au watano wanaofunga mabao ya kutosha katika msimu mmoja,” alisema Kane.

“England tuna Sterling ambaye anafunga mabao kwenye klabu na timu yake ya taifa, Sancho amekuwa akifanya hivyo kule Borussia Dortmund, pia anasaidia kutoa na asisti.

“Hilo ni jambo muhimu sana, yeyote atakayepangwa kwenye safu ya washambuliaji watatu ni vema akawa na uwezo wa kufunga na kusaidia upatikanaji wa mabao.

“Kwa sasa tunamshuhudia Sterling aliye na kiwango bora kabisa. Rashford pia angetusaidia, lakini kwa bahati mbaya ameumia. Wapo akina Dele Alli na Ross Barkley, pia wana uwezo wa kusukuma mashambulizi na kufunga mabao.

“Jambo zuri zaidi kuna vijana, Callum Hudson-Odoi na Sancho bado wanachipukia, lakini unawaona wanavyocheza kwa kujituma, hawaogopi kukutana na mabeki,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here