Home Makala MASOUD DJUMA: HAO YANGA NA WAJE TU

MASOUD DJUMA: HAO YANGA NA WAJE TU

1739
0
SHARE

NA SALMA MPELI

JUMATANO wiki hii, aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alitangaza kubwaga manyanga kibarua chake cha kuinoa timu hiyo. Mganda huyo aliyeanza kuifundisha Simba Januari mwaka jana, mpaka anaachia ngazi alikuwa chini ya Mcameroon, Joseph Omog.

Mbele ya kamera za vyombo vya habari, Mayanja, alitamka kwa kifupi sababu iliyomsukuma kuachia ngazi kazi hiyo kuwa ni kukabiliwa na matatizo ya kifamilia nyumbani kwao Uganda. Saa chache baada ya Mayanja kuanika uamuzi wake huo aliibuka msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara, kukiri kupokea barua ya kujiuzulu kwa kocha huyo na kwamba wameridhia ombi lake.

Siku iliyofuata Simba kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ilimpokea kocha mbadala wa Mayanja, Mrundi Masoud Djuma, ambaye ni mwalimu wa zamani wa klabu ya Rayon Sport ya Rwanda.

DIMBA limefanya mahojiano na kocha huyo mpya wa Simba kujua mengi kuhusu ujio wake ndani ya kikosi cha timu hiyo kinachokabiliwa na kibarua kizito cha kuwafuta machozi mashabiki wake wenye hamu ya kuona timu hiyo ikitwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

DIMBA: Habari za safari kocha na karibu sana Tanzania.

Djuma: Ahsante nashukuru.

DIMBA: Umeshasaini mkataba na Simba maana naona tayari umeshaanza kazi bila kuchelewa.

DJUMA: Bado sijasaini mkataba, lakini kila kitu kipo sawa, nilishamalizana nao tangu nikiwa nyumbani kwa maana ya mazungumzo ya kimkataba. Wakati wowote nitasaini rasmi.

DIMBA: Mashabiki wa Simba wangependa kujua pengine unatarajia kusaini mkataba wa muda gani?

Djuma: Kwa kuwa nipo Dar es Salaam tayari nadhani hili nitawajulisha mara baada ya kusaini kwani kila kitu nitakiweka wazi. Kikubwa wajue mambo yote ya kimsingi tumeshakubaliana ikiwemo mshahara nitakaolipwa.

DIMBA: Ulianza lini mazungumzo baina yako na klabu ya Simba?

DJUMA: Si muda mrefu sana kama wiki mbili zilizopita.

DIMBA: Ni kiongozi gani alikufuata kwa mazungumzo?

DJUMA: Crescentus Magori na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’.

DIMBA: Je, unaifahamu Simba tangu lini?

DJUMA: Muda mrefu tu, tangu nacheza soka na pia niliwahi kuisikiliza kwenye redio wakati wa mechi zao na Yanga.

DIMBA: Je, unajua ushindani wa Simba na Yanga?

DJUMA: Presha ya mechi ni presha tu, lakini ushindani upo kila sehemu kwani hata nilipokuwa Rwanda ikitokea mechi kati ya Rayon Sport na ARP kunakuwa na ushindani kama wa timu hizo.

DIMBA: Umekuja wakati Simba ipo kwenye maandalizi ya mechi yao dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, ni mechi ngumu na yenye presha kubwa, vipi umejiandaaje na hilo?

DJUMA: Mimi nilikuwa mchezaji na si mara ya kwanza kusikia mechi ya Simba na Yanga. Kwangu naitazama kama mechi ya kawaida sana presha tunajipa wenyewe kiushabiki tu. Nawasubiri hao Yanga kwani tayari nina kila kitu nakijua kuhusu wao na waje tu.

DIMBA: Mara nyingi kocha huwa anapimwa kupitia matokeo ya mechi hiyo, je, ikitokea mmepoteza upo tayari kutimuliwa?

DJUMA: Mpira una matokeo ya aina tatu, kushinda, kutoka sare na kufungwa, mimi sijaja kufanya maajabu yoyote bila kumtegemea Mwenyezi Mungu. Muhimu ni sisi kujipanga kwa kufanya maandalizi ya kisaikolojia kwa wachezaji wetu na wao kuzingatia kile ambacho tutawaelekeza kama benchi la ufundi. Hili la ukame wa mataji naamini tukishirikiana vyema mbona freshi litakwisha.

DIMBA: Ni wachezaji gani wa Tanzania unawafahamu?

DJUMA: Namfahamu Laudit Mavugo na Amis Tambwe ambao ni wachezaji wa Burundi wenye viwango bora wakiwa na uwezo mkubwa wa kufunga.

DIMBA: Umejiandaaje kukabiliana na changamoto?

DJUMA: Kama unafundisha na uliwahi kucheza mpira, hakuna presha, kikubwa ni kufanya kazi kama ambavyo Mungu amekujalia.

DIMBA: Kuna tofauti gani kati ya soka la Tanzania na Burundi?

DJUMA: Utofauti si sana labda uwezo wa kipesa tu, kwani Tanzania wana uwezo mkubwa wa kipesa.

Mbali na kazi ya ukocha, Djuma amewahi kuwa mchezaji wa zamani wa timu za Prince Louis, APR na nyingine za nje ya Rwanda, lakini pia amewahi kuzinoa timu za Rwanda kama Rayon Sport na Inter Club na Inter F za Burundi.

Kocha huyo aliachia ngazi kuifundisha Rayon msimu uliopita baada ya kufanikiwa kuipa timu hiyo taji la Ligi Kuu ya Rwanda kabla ya hivi karibuni kutua nchini na kujiunga na Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here