Home Makala Maswali 10 kwa Arsene Wenger

Maswali 10 kwa Arsene Wenger

585
0
SHARE

LONDON, England

MSIMU mpya, Arsenal ileile. Arsene Wenger ameanza msimu kwa kichapo cha mabao 4-3 kutoka kwa Liverpool, mchezo ukipigwa katika dimba la Emirates. Kichapo hiki kinaonekana kuwaumiza sana mashabiki wa Arsenal, ambapo mpaka sasa yameibuka maswali 10 ambayo wanataka kusikia yakijibiwa na Profesa Wenger.

1 – Kwanini kikosi hakikuwa tayari?

Baada ya fainali za Euro 2016, Arsenal walitarajiwa kuwakosa Mesut Ozil, Olivier Giroud na Laurent Koscielny kwenye pambano dhidi ya Liverpool, waliopewa likizo za mwezi mzima. Likawa pengo kubwa kwa Arsene Wenger.

Kama kuna kauli ya Wenger iliyowaumiza mashabiki wa Arsenal, ni ile aliyoitoa kuwa kikosi chake hakipo fiti. Lakini wiki moja baadaye baada ya kuichapa Manchester City, Wenger aligeuka tena na kusema, ‘tuko tayari.’

Arsenal walitakiwa kuwa tayari, asilimia kubwa ya wachezaji walikuwa na mapumziko marefu, kwa walivyoonekana kwenye pambano la Liver, ni wazi kuwa hawakuwa fiti na hili ni kosa la Wenger.

2 – Kwanini bado haujui pia ni lini kitakuwa tayari?

Jambo la kuogopesha zaidi ni kauli aliyoitoa Wenger baada ya kichapo cha Liverpool, kwa kudai kuwa hajui ni lini timu yake itakuwa tayari kupambana na mikiki mikiki ya Premier League. “Ni lini tutakuwa tayari? Sijui,” alisema Wenger. “Tunatakiwa kuwa tayari kwa sababu wiki ijayo tunacheza na Leicester.” Hapa kuna pointi ya msingi.

Ratiba imekaa kikatili kwa Arsenal, baada ya kucheza na Liverpool, wanatakiwa kusafiri ugenini kupambana na bingwa mtetezi. Wenger alipaswa kuwaandaa vijana wake na shughuli hii ili kuondoa aibu ya kuanza ligi kwa vichapo mfululizo.

3 – Kwanini hili limejirudia tena?

Kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida kwa Arsenal kupoteza pambano la kwanza la Ligi katika uwanja wa nyumbani, huamini?
Huu ulikuwa mwaka wa Liverpool kutumia udhaifu huu wa Arsenal, lakini miezi 12 iliyopita kazi hii ilifanywa na West Ham na miaka mitatu iliyopita The Gunners walipoteza dhidi ya Aston Villa.
Huu ni mwenendo mbaya wa Wenger, lakini haonekani kama amejifunza kitu kwenye vichapo vilivyopita. Mara zote Arsenal walizokuwa wakianza kwa staili ya kufungwa, walipambana na kumaliza kwenye nafasi ya 4, lakini hali ni tofauti msimu huu, wapinzani ni wengi wanaowania nafasi nne za juu.

4 – Kwanini majeruhi hawaishi Arsenal?

Ingawaje kikosi cha Arsenal kilichopoteza pambano dhidi ya Liverpool kilikosa nyota kadhaa, lakini Alexis Sanchez, Mohamed Elneny na Theo Walcott walianza, huku Granit Xhaka na Santi Cazorla wakianzia benchi. Lakini ukweli ni kuwa zaidi ya nusu ya kikosi cha Arsenal ni majeruhi.

Gabriel, Jack Wilshere, Per Mertesacker, Danny Welbeck na Carl Jenkinson wote ni majeruhi na niWilshere pekee ambaye anafahamika atarejea lini. Idadi hii inawaweka Arsenal nyuma ya West Ham kwenye orodha ya klabu za Premier League zenye wachezaji wengi walio majeruhi.
Liverpool wana watano, lakini klabu nyingine zinazopewa nafasi ya kubeba taji Chelsea na Manchester City wana watatu kila mmoja, Manchester United wana majeruhi mmoja na Tottenham hawana mtu aliye nje.

5 – Kwanini hakusajili beki wa kati?

Katika eneo ambalo kikosi cha Arsenal kiliathirika kwa kiwango kikubwa ni safu ya ulinzi– lakini kilichoonekana kufanywa na Wenger ni mchezo wa bahati nasibu.

Kuwapanga Calum Chambers na Rob Holding kama walinzi wa kati dhidi ya Liverpool ilikuwa ni dhambi kubwa ambayo Wenger aliamua kuifanya pale Emirates.
Kwa kipindi chote cha dirisha la usajili Wenger amekuwa akihusishwa na tetesi za kutaka kusajili beki wa kati ili kuja kusaidiana na Laurent Koscielny, hasa kipindi hiki ambacho Per Mertesacker na Gabriel wakiwa majeruhi.

Miongoni mwa waliotajwa sana ni kisiki cha Valencia, Skhodran Mustafi, aliye na thamani ya pauni mil 30, swali linalokuja vichwani, ni kwanini Wenger hakukamilisha usajili huu?

6 – Kwanini hakusajili straika wa maana?

Mbali na kuwa na tatizo la beki, ubovu mwingine wa Arsenal ni eneo la ushambuliaji.
Msimu uliopita Arsenal walifunga mabao 65– idadi sawa na West Ham, waliomaliza kwenye nafasi ya 7.

Lakini inabidi tufahamu kuwa idadi hiyo ilikuwa ndogo kulinganisha na ya msimu wa mwaka juzi. Achana na mambo ya takwimu, ni nani asiyejua kuwa Olivier Giroud si straika wa levo za dunia kiasi cha kutegemewa na klabu kama Arsenal?
Lakini kwanini bado Wenger hafanyi juhudi za kusajili straika mpya? Kilichoshindikana kwa Alexandre Lacazette ni dau la pauni mil 60 lililotakiwa na Lyon, huenda Wenger hakuona sababu ya kutoa pesa hizi kwa mchezaji anayewekwa benchi na Giroud kwenye kikosi cha taifa.

Hii ndiyo iliyofanya Wenger kulazimisha kumtumia Sanchez kama straika wa mbele dhidi ya Liverpool. Licha ya Arsenal kufunga mabao matatu, Sanchez hakufunga hata moja, kwanini timu iendelee kumtegemea kwenye mechi zijazo?

7 – Tangu lini Theo Walcott akawa mpiga penalti?

Lilikuwa jambo la kushangaza sana pale Theo Walcot alipookota mpira na kupiga penalti, tangu lini ameanza kazi hii? Ndiyo maana haikushangaza pia alivyokosa.
Huenda mechi ingebadilika na kumalizika na matokeo mazuri kwa Arsenal kama wangepata penalti ile, kwanini hawakuona umuhimu wake mpaka wakamkabidhi Theo Walcot jukumu lile?

8 – Hivi bajeti yako ya usajili ni kiasi gani mzee?

Kama Wenger ataamua kumuweka kando Walcot na kusajili winga mmoja, beki na straika wa kati, unadhani ni kiasi gani atatumia kwenye usajili wake?
“Kama tukipata watu tunaowahitaji tutatumia kiasi kikubwa cha pesa,” alikaririwa Wenger mwanzoni mwa Julai akiwaeleza mashabiki mipango yake ya usajili ilivyo.

Lakini siku chache baadaye, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ivan Gazidis, aliibuka na kutoa kauli tofauti na Wenger. “Hatuwezi kufanya makosa kwenye dirisha la usajili kwa kumwaga pesa ovyo, hatuko tayari kufanya ushindani wa hela na klabu nyingine kwa sasa”.
Nani mkweli katika hawa? Arsenal waliwahi kutumia pauni mil 40 kwa Ozil na pauni mil 35 kwa Sanchez kama usajili wao mkubwa wa msimu.
Mpaka sasa wameshatoa kiasi cha pauni mil 34 kwa ajili ya Xhaka, ameshamaliza?

9 – Yule Steve Bould anafanya kazi yake sawa sawa?

Kwa kuruhusu mabao manne kwenye mechi moja, tena ya kufungua msimu, bila shaka kikosi cha Wenger kina tatizo kubwa kwenye safu yake ya ulinzi.
Steve Bould anafanya kazi yake ipasavyo? Unamjua huyu? Ni beki mkongwe wa klabu hiyo ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye benchi la ufundi kama kocha wa mabeki.
Tangu achukue nafasi hiyo mwaka 2012 kutoka kwa Pat Rice aliyestaafu, Bould ameishuhudia Arsenal ikiruhusu mabao 36 kwenye msimu miwili, huyu mtu ni sahihi kuendelea kukaa kwenye benchi la ufundi?

10 –Vipi hujafikiria kuondoka sasa?

Mwisho kabisa, swali pekee ambalo mashabiki wa Arsenal wanasubiri majibu yake kwa hamu kubwa ni hili, Babu hujafikiria kustaafu na kutuachia timu?
Kwa miaka yake 66, bila shaka Mfaransa huyu hana muda mrefu tena kwenye maisha yake ya ukocha, lakini mpaka leo Wenger na Gazidis wameendelea kufanya siri kubwa juu ya mabadiliko ya benchi la ufundi, licha ya kuwepo kwa presha kubwa ya mashabiki kuhitaji suala hilo.

Mashabiki wa Arsenal hawaamini kama Wenger ana ubunifu mpya kichwani kwake wa kupambana na kina Jose Mourinho, Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Mauricio Pochettino na Antonio Conte, lakini mwenyewe anajua hili?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here