Home Michezo Kimataifa MATIP NI SHIDA NYINGINE LIVERPOOL

MATIP NI SHIDA NYINGINE LIVERPOOL

518
0
SHARE

LIVERPOOL, England

WAKATI mashabiki wa Majogoo wa Anfield msimu huu wa Ligi Kuu England wakikimwagia sifa kikosi chao kulingana na uwezo wa kiwango cha juu kinachoonyeshwa na nyota wao, hususani katika safu ya ushambuliaji inayoundwa na wakali watatu matata Roberto Fermino, Sadio Mane na Philippe Countinho, lakini pia kuna jembe hatari Joel Matip anayecheza beki wa kati.

Katika mchezo wa ligi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita walipokipiga na Crystal Palace na mchezo kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, Matip alicheza kwa kiwango cha juu sana katika idara ya ulinzi.

Baada ya mchezo huo kumalizika, kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp, aliiambia tovuti ya klabu hiyo: “Matokeo haya kwetu ni kama tumepoteza mchezo, ingawa nimefurahishwa na kiwango cha juu sana kwa mabeki wangu hususani Matip.”

Matip, raia wa Cameroon aliyezaliwa nchini Ujerumani, anafahamu vema jinsi ya kukabiliana na washambuliaji tofauti tofauti wa timu pinzani.

Nani asiyejua makali yake hasa anapokuwa kwenye himaya yake ya ulinzi mbele ya adui yake haswa washambuliaji mahiri?

Matip kwa hivi sasa ndiye anayeufanya ukuta wa Liverpool kusimama imara, ikiwa timu hiyo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ingawa imefungwa mabao 14 tofauti na vinara Chelsea walioruhusu mabao tisa tu kutinga nyavuni kwao, ingawa Tottenham, inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo, nyavu zake zimeguswa mara nane tu.

Ana umbo la kawaida, lakini sifa yake kubwa ni kucheza mipira yote ya juu na ya chini na anatumia akili kwenye kukaba. Kwa kifupi Matip ni mwiba wa kuogopwa na mastraika wakorofi.

Ubora wake huo unaelezwa kuwa hadi kufikia mwisho wa msimamo wa Ligi Kuu ya England ‘EPL’, huenda ukaondoa kabisa wimbi la kuwa miongoni mwa timu nyingi ambazo nyavu zao zinaguswa mara nyingi.

Rekodi zinaonyesha kuwa katika msimu wa 2013/14 Liverpool ama ‘The Reds’ kama wanavyojulikana, walifungwa jumla ya mabao 50, wakiwa mbele kwa idadi ya mabao 13 zaidi Manchester City.

Lakini msimu huu kumeonekana kuna mabadiliko makubwa zaidi kwenye kikosi hicho ambacho tayari kimeshatupia mabao 30, huku ya kufungwa yakiwa ni 14 pekee.

Hata hivyo, uwezo mkubwa wa kumiliki mipira kuanzia kwenye safu ya ushambuliaji kwa akina Sadio Mane, Philippe Coutinho na Roberto Fermino, umeufanya ukuta wao kuwa na utulivu mkubwa kutokana na kutokuwepo kwa presha ya mara kwa mara, kitendo kinachomfanya beki wa kulia, James Milner, kuwa na muda mwingi wa kushambulia.

Matip anayetajwa na wachambuzi wa soka kama moja ya usajili makini za Klopp, akitokea ndani ya klabu ya Schalke ya Ujerumani inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu kama ‘Bundesliga’, amefanikiwa kuingia kwa haraka kwenye mfumo wa Mjerumani mwenzake huyo kwa haraka na taratibu anaanza kuimudu Ligi Kuu England.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, hadi sasa ameshuka dimbani kuichezea klabu yake hiyo michezo 10, huku akiwa amezuia mashambulizi hatari ‘inteception tisa.’

Matip ambaye ni mnyumbulifu zaidi, hakuwemo katika kikosi kilichoruhusu mabao matatu katika ushindi wa 4-3 ambao Liverpool iliupata dhidi ya Arsenal, huku pia akikosekana kwenye kikosi kilichopoteza mechi kwa kufungwa bao 2-0 dhidi ya Burnley.

 

Mfalme wa kucheza kwenye nafasi

Uwezo mkubwa wa Matip anapokuwa uwanjani ni jinsi ya kuwatambua wapinzani wanavyocheza na kuziba nafasi zao. Aliweza kuwamudu vilivyo nyota wa Crsytal Palace chini ya kocha wao, Alan Scot Pardew na kufanikiwa kufanya ‘tackle’ zisizokuwa na madhara.

Umahiri wake huo ulimfanya kuwa bora zaidi katika Ligi ya Bundesliga ambapo ni mara chache sana kumkuta amekumbana na adhabu kutoka kwa mwamuzi, ikiwamo kuonyeshwa kadi ya njano.

Katika jumla ya mechi 274 za ushindani alizocheza hadi sasa, ameonyeshwa kadi 32 pekee, huku kwa beki mwenzake wa mahali hapo Lovren, akiwa na kadi 67 katika michezo 304 aliyoshuka dimbani.

Matip ni mwepesi zaidi kuwa sehemu sahihi kwa wakati akipokonya mipira pamoja na kuzuia mashambulizi.

Kimo chake cha futi sita hewani kwenye idara yake hiyo ya ulinzi humsaidia vilivyo kuweza kuichukua mipira ya juu, sifa ambayo ni ya ziada kwake, huku muunganiko wake na Lovren ukiwafanya makipa wa Liverpool, Simon Mignolet na Loris Karius, kuwa na kazi nyepesi langoni.

 

 

Kipenzi cha Klopp

Licha ya usajili wake huo kutajwa kuwa ni bora zaidi kuwahi kufanywa na Klopp, inaelezwa pia beki huyo ni kipenzi kikubwa cha kocha huyo tangu wakiwa ligi moja ya Bundesliga nchini Ujerumani, Klopp akiongoza Borussia Dortmund kama kocha mkuu, wakati yeye akikipiga katika klabu ya Schalke.

“Klopp kipindi yupo Dortmund aliwahi kuniambia siku moja nitafanya naye kazi sehemu moja akiwa kama kocha wangu na kweli limetimia, nitafanya kila jitihada nisimwangushe, kila siku lazima nijaribu kupiga hatua mbele zaidi,” alisema Matip katika mahojiano maalumu na vyombo vya habari muda mfupi baada ya kusajiliwa Anfield.

 

Kiraka, pasi rula

Matip mwenye uwezo mkubwa kucheza katika safu ya ulinzi bila kubutua ovyo mipira na kuwamudu washambuliaji wenye viwango vya juu, huku pasi nyingi zikiwa fupi fupi za chini zinazofika kwa mlengwa, pia ana uwezo mwingine wa kucheza kama kiungo ikitokea mahitaji ya kocha yanamtaka kufanya hivyo, ambapo amekuwa akipiga pasi za ‘rula.’

 

Anamrahisishia kazi Jordan Henderson

Mapungufu ya Jordan Henderson anayecheza kama kiungo mkabaji ambaye asili yake ni kiungo mshambuliaji, yamekuwa yakizibwa na Matip ambaye mara nyingi amekuwa akisogea juu kidogo nyuma ya Henderson kuhakiki mipira inayoweza kumvuka Muingereza huyo.

Alifanya hivyo dhidi ya Crystal Palace, ambapo alipiga pasi ‘rula’ 14 mahali hapo na kupokea nyingine 18 kutoka kwa nyota mwenzake huyo. Katika mechi hiyo iliyopigwa ndani ya dimba la St Mary, aliipiga jumla ya pasi 84, sahihi zikiwa ni 69.

 

Nje michuano ya Afrika

Taarifa njema kwa Liverpool, wakati wakimkosa staa wao, Sadio Mane, katika safu ya ushambuliaji Januari kutokana na kwenda kuitumikia timu yake ya taifa ya Senegal, kwa upande wa Matip ataendelea kuwepo kikosini hapo.

Hii ni baada ya kuamua kuchagua timu yake ya taifa kuwa Ujerumani alikozaliwa badala ya Cameroon kwenye michuano ya kimataifa.

“Nimempigia Joel simu zaidi ya mara 15 na kumtumia ujumbe wa simu kwa nyakati tofauti lakini hapokei wala kujibu,” alisema kocha wa timu ya taifa ya Cameroon, Hugo Broos, kuthibitisha kuwa hawana mawasiliano.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here