SHARE

NA MWANDISHI WETU

SIKU ya Oktoba mosi, 2016 katika Jiji la London, Arsene Wenger, alikuwa akisherehekea miaka 20 tangu alipoteuliwa kuwa kocha wa Arsenal na jijini Dar es Salaam, Simba na Yanga zilikuwa zikipambana.

Licha ya pambano kumalizika kwa sare ya bao 1-1, yako matukio saba ambayo kwa vyovyote vile lazima yatabaki katika vichwa vya wapenzi wa soka Bongo, kila watakapokuwa wakiukumbuka mchezo wa Simba vs Yanga uliopigwa Oktoba mosi, 2016.

 

Tiketi za elektroniki

Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya soka Tanzania, mashabiki wa soka walianza kuutumia mfumo wa tiketi za elektroniki katika pambano ya Simba na Yanga.

Licha ya kuwa mfumo ulioandaliwa kwa ajili ya kudhibiti wizi wa mapato, lakini changamoto zake zilikuwa kubwa kiasi cha kusababisha vurugu kubwa wakati wa kuingia uwanjani.

Pengine huu ni mfumo bora na wakisasa zaidi, lakini haukutakiwa kutumika Oktoba mosi. Pambano la Simba vs Yanga ni kubwa sana na haikuwa rahisi kwa mashabiki kuelewa namna ya kutumia tiketi hizo.

 

Offside ya Ajib

Moja katika mambo ambayo Martin Saanya atakuwa akimlaumu sana mwamuzi wa pembeni ‘Line One’, Samwel Mpenzu, ni namna alivyomwingiza kwenye lawama ya kulikataa bao la Simba lililofungwa na

Ibrahim Ajib.

Saanya hakuwa kwenye ‘position’ ya kukataa au kukubali goli la Ajib, huwezi kumlaumu moja kwa moja bali mwamuzi wa pembeni, Mpenzu ndiye anatakiwa abebe lawama zote katika hili.

Na ndio maana baada ya mpira kuzama nyavuni aligeuza macho yake na kumtazama, alipoona kibendera kipo juu hakuwa na namna nyingine zaidi ya kukataa bao lile, lakini ukweli lile lilikuwa bao halali na Ajib hakuwa ‘offside’ kama alivyohukumu Mpenzu.

Ukipata bahati ya kuitazama video ya tukio lile bila shaka utakuwa ukijiuliza ni vipi mshika kibendera alilikataa bao lile wakati Ajib alikuwa ‘onside’ kipindi Shiza Kichuya alipopiga pasi ya mwisho.

 

Bao la Tambwe

Hakuna shabiki wa soka Bongo atakayeizungumza Oktoba mosi halafu akaacha kulizungumzia bao la Yanga lililofungwa na Mrundi, Amissi Tambwe.

Ni kweli alifunga na mguu lakini alianza kuushika kwanza kabla ya kujitengenezea nafasi na kufunga.

Hapa huwezi kumlaumu Saanya wala ‘line 2’, Ferdinand Chacha, wakati Tambwe akifunga bao hili. Kwanini? Tambwe alimpa mgongo Chacha na Saanya hakuwa karibu na eneo la tukio.

Mtu pekee aliyeona tukio lile kwa karibu ni beki wa Simba, Novatus Lufunga na kipa wake, Vicent Angban na ndio maana uliona mtafaruku mkubwa baada ya kuingia kwa bao lile.

 

Kadi nyekundu ya Mkude

Jonas Mkude, nguzo muhimu katika kikosi cha Simba msimu huu na ndani ya dakika 25 tu za kipindi cha kwanza alijikuta ameshaingia kwenye kitabu cha Martin Saanya kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.

Taarifa ya Saanya inaeleza kuwa alisukumwa na Mkude wakati wakilumbana kuhusu bao la Yanga na hili ndilo lililomfanya afanye maamuzi ya kutoa kadi nyekundu.

Lakini Mkude mwenyewe alikana kumsukuma Saanya na ameendelea kusisitiza kuwa hakumsukuma na alichokuwa akikifanya yeye kama kiongozi ni kuongea naye kuhusu tukio la Tambwe lilivyokuwa, nani mkweli? Hakuna wakuthibitisha hili na tayari Oktoba mosi imeshapita.

 

Simba kurusha viti

Kukubaliwa kwa bao la Tambwe kisha nahodha wao kupewa kadi nyekundu, hakika haya yalikuwa mambo mawili makubwa yaliyowavuruga zaidi mashabiki maelfu ya Simba waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hayati Nelson Mandela aliwahi kunukuliwa akisema: ‘Ukitaka kujua nguvu ya mnyonge, mpore haki yake’. Baada ya mashabiki wa Simba kuhisi wanaonewa na maamuzi ya refa, uamuzi wa haraka zaidi walioufanya ni kuonyesha hasira zao.

Ghafla mvua ya viti ikaanza, fujo ikatimka na mpira ukalazimika kusimama kwa dakika kadhaa mpaka hali ya amani itakaporejea, Oktoba mosi itakumbukwa zaidi kwa ile mvua ya viti pale Taifa.

 

Mabomu

Sikumbuki ni lini tena nilitazama mpambano wa Simba na Yanga na kukapigwa mabomu na jeshi la kutuliza ghasia kama ilivyokuwa Oktoba mosi.

Hii inaweza kuwa mara ya kwanza na wapenda soka wote tunaomba iwe ni ya mwisho kabisa, hatutarajii tena kuona mpambano mkubwa zaidi nchini ukitawaliwa na vurugu na mabomu namna ile.

Wako walioathirika na tukio lile kwa kuumia na kupoteza mali zao, kimsingi halikuwa tukio zuri na tunaomba Mungu kama ilivyopita Oktoba mosi hii, ipite na tukio hili. Kwaheri Oktoba mosi!

 

Bao la Kichuya ‘Olympic goal’

Naam! Pengine hili linaweza kuwa tukio bora na tamu zaidi Oktoba mosi.

Huku mashabiki wa Simba wakiwa wamepoteza kabisa matumaini ya kupata matokeo dhidi ya wapinzani wao, Shiza Kichuya alionyesha ni kwanini viongozi wa Msimbazi walimpandia gari kumfuata Morogoro.

Akichonga kona safi iliyozama moja kwa moja langoni mwa Yanga na kuisawazishia Simba, bao lililoibua shangwe kubwa kwa mashabiki wa Simba na kuzima kabisa tambo za Yanga.

Kwa miaka mingi zaidi, Shiza Kichuya anaweza kukumbukwa zaidi kwa bao la ‘Olympic goal’ alilofunga kwenye ‘Kariakoo derby.’ Yamefungwa mabao mengi, lakini lile la Kichuya litabaki kwenye kumbukumbu ya Oktoba mosi milele.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here