SHARE
Laudit Mavugo

STRAIKA wa Simba Mrundi, Laudit Mavugo, amesikia kelele za mashabiki wakisifia kiwango chake kisha akacheka kidogo na kutamka maneno ambayo huenda yasiwafurahishe kabisa mashabiki wa timu pinzani na washambuliaji ambao wana ndoto za kuibuka wafungaji bora.

Mavugo ambaye amesajiliwa na Simba kutoka Vital’O ya Burundi, alianza kuonyesha cheche zake kwenye mchezo wa tamasha la Simba Day Agosti 8 mwaka huu alipoonyesha uwezo mkubwa na kufunga bao lililowafanya Wekundu hao wa Msimbazi kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya AFC Leopard ya Kenya.

Mbali na mchezo huo, pia Mavugo alionyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya URA ya Uganda uliochezwa Agosti 14 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Kudhihirisha kuwa Simba hawajamsajili kwa bahati mbaya, alikuwa chachu ya ushindi mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC katika uwanja huo huo, uliomalizika kwa ushindi wa mabao 3-1 Mrundi huyo akifunga bao moja.

Kutokana na uwezo huo katika michezo hiyo mitatu, jina la straika huyo limekuwa gumzo kila kona lakini mwenyewe ameibuka na kuwaambia kuwa bado hajafanya kazi iliyomleta Tanzania na kwamba mashabiki wa kikosi hicho wavute subira kwani mambo mazuri yanakuja.

“Kwanza nashukuru kwa jinsi ninavyopata sapoti kutoka kwa mashabiki wangu, niwaahidi tu kwamba kama Mungu akisaidia wataendelea kufurahia huduma yangu kwani licha ya wao kuona nilichofanya mpaka sasa ni kikubwa, kwangu mimi bado kazi mbichi.

“Sijafikia pale ambapo ninapahitaji, kilichopo tuzidi kuomba uzima kwani kila jambo Mungu ndiye anayelipanga, vinginevyo mashabiki waendelee kutupa sapoti,” alisema.

Akizungumzia mbio za ufungaji bora alisema lengo lake ni kufunga mabao mengi iwezekanavyo, kubwa likiwa kuipa Simba ubingwa na baadaye ndipo atakapoangalia ufungaji bora.

Mavugo anapata jeuri hiyo kwani amefanya mambo makubwa katika ligi ya nchini Burundi, akimaliza kama mfungaji bora alipopachika mabao 32, huku pia akiibuka mfungaji bora michuano ya FA alipofunga mabao saba.

Kauli hizo za Mavugo zinaashiria kuwa mabeki wa timu pinzani itabidi wakaze buti kwelikweli kwani bila kufanya hivyo wanaweza wakajikuta wanawaaibisha makipa wao.

Katika hatua nyingine Rais wa klabu ya Vital’O ya Burundi alikokuwa akichezea straika huyo, Benjamin Bikolimana, amesema wamepokea Sh milioni 80 kutoka klabu ya Simba na wao kiroho safi hawana kinyongo chochote na wamemruhusu kijana wao kwa moyo mweupe kuwatumikia Wana Msimbazi.

“Tuna uhusiano mzuri na Simba tangu zamani hivyo licha ya kutaja kiasi cha Sh milioni 200 ambazo tulizitaka awali, alikuja kiongozi wao mmoja tukakaa naye mezani na kukubali kushusha hadi milioni 80 ambazo wameshalipa, hivyo kwa sasa  hatuna tatizo nao.

“Tumemruhusu kijana wetu kwa moyo mmoja, tunajua huko Tanzania amekuja kufanya kazi, kama atapewa ushirikiano nina imani mashabiki wa Simba watafurahi wenyewe,” alisema.

Simba inatarajia kucheza tena mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi Agosti 27, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here