Home Habari MAVUGO: SIMBA MBONA MTAFURAHI TU

MAVUGO: SIMBA MBONA MTAFURAHI TU

523
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

STRAIKA Mrundi wa Simba, Laudit Mavugo, alicheza kwa dakika 534 katika mechi saba za Ligi Kuu Tanzania Bara, bila kuziona nyavu za timu pinzani, hali iliyozua minong’ono miongoni mwa mashabiki.

Katika mechi hizo ambazo baadhi alimaliza dakika zote tisini na nyingine alitolewa, Mavugo alijitahidi kuhangaika kwa kila hali kusaka mabao bila mafanikio yoyote.

Kwa mara ya mwisho, straika huyo alifunga bao Oktoba 23, mwaka jana katika mechi ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, ambapo Muzamiru Yasin alifunga mabao mawili dakika za 42 na 74, huku yeye akifunga dakika ya 51 kwa mguu wa kulia, akipokea pasi kutoka kwa Mohammed Ibrahim.

Lakini Jumamosi iliyopita, aliwafurahisha tena mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi kwa kufunga bao safi la ‘video’ wakati Simba ikishinda 3-0 dhidi ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji.

Kitendo cha Mavugo kufunga bao hilo kiliwanyanyua wachezaji wote katika benchi la ufundi na kuwafanya kushangilia bao hilo zaidi kuliko yote yaliyofungwa siku hiyo.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Mavugo alisema anafurahi kuifungia timu yake bao na kucheza dakika zote 90 na ana imani kubwa kwamba sasa atafanya vizuri zaidi na kuwafurahisha mashabiki.

Mavugo alisema anamshukuru nyota wa zamani wa Wekundu hao, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye ndiye aliyempa moyo na kumfanya ajione amezaliwa upya katika klabu hiyo.

“Julio aliniambia kuwa mimi ni mchezaji ambaye Simba inanitegemea na ubingwa wa msimu huu upo mikononi mwangu, kwa kweli maneno hayo yalinijenga na kunifanya nijiamini muda wote wa mchezo,” alisema Mavugo.

Alisema ataendelea kumheshimu na kumsikiliza kocha wake pamoja na washauri kama akina Julio, kwa sababu anahisi amebadilisha maisha yake ya soka.

Alisema tangu atue Tanzania, hajawahi kupata mtu na kuzungumza naye maneno muhimu kama hayo na kumfanya ajione yeye ni shujaa kwa miamba hiyo ya soka Tanzania.

“Ukweli maneno ya Julio yamenijenga na kujiona jasiri na sasa naamini nitabadilika na kufunga katika kila mechi ambayo nitapangwa kwenye kikosi cha Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here