SHARE

NA BADI MCHOMOLO

WIKI iliyopita toleo la  13 tuliona jinsi bingwa huyo wa ngumi, Floyd Mayweather, alivyokuwa anafundishwa ngumi peke yake.

Baba wa Mayweather aliamua kufanya hivyo kwa ajili ya kumpa mazoezi maalumu ya kumwandaa ili aje kuwa bora kwenye mchezo huo.

Mipango hiyo ilikuja mara baada ya bingwa huyo kushinda mara mbili katika mapambano yake ya kulipwa.

Baba wa Mayweather, alitumia muda mwingi kumfanyisha mazoezi mtoto wake kwenye mchanga pamoja na maji kwa ajili ya kutafuta pumzi za muda mrefu, jambo ambalo lilimfanya Mayweather kuweza kuhimili mashindano mengi kwa muda mrefu.

Tuachane na hayo yaliyopita wiki ile… sasa tuangalia sehemu ya 14 ambayo inamwelezea bingwa huyo kwamba alifikia hatua kutaka kuachana na mazoezi ya baba yake.

Baba wa bondia huyo aliamua kutumia muda wake mwingi kumuandaa mtoto wake, hivyo alikuwa anampa mazoezi ya nguvu jambo ambalo lilikuwa linampa wakati mgumu bondia huyo na kufikiria maamuzi ya kutaka kuchana na mazoezi ya baba yake.

“Nilidhani baba ataamua kunipa mazoezi mepesi, lakini hali ilikuwa tofauti, hana masihara kwenye mazoezi, kila siku alizidi kuwa mkali.

“Kitendo hicho kilizidi kunichukiza kwa kuwa nilikuwa sijui kama ananifanya nikomae katika mchezo huo.

“Kuna wakati nilikuwa nawakumbuka wajomba zangu ambao walikuwa wananifundisha wakati baba yupo jela, lakini tayari baba alikuwa amechukua jukumu hilo japokuwa kuna wakati wajomba walikuwa wanakuja kunitembelea na kunipa mazoezi mengine.

Mayweather aliongeza kwa kusema, wakati mwingine akifundishwa baada ya muda baba yake anaomba pambano wapigane ili kumuangalia kama atakuwa ameelewa.

Baba wa Mayweather akiwa anapigana na mtoto wake alikuwa anapiga kweli jambo ambalo Mayweather alikuwa halidhanii.

“Wakati nafanya mazoezi ya kupigana na baba nilikuwa najiona kama nipo mazoezini, lakini yeye alikuwa anafanya kweli, anatumia nguvu nyingi kunipiga nikawa nashangaa.

“Hali hiyo ilikuwa inanipa mawazo ya kutaka kurudi kwa wajomba au kuachana na mazoezi ya baba, lakini ukweli ni kwamba alikuwa ananipa mbinu za kuwa mvumilivu kila ninapokutana na mpinzani wangu.

“Nilijaribu kuzungumza na baba na kumwambia kwamba ni bora nikajiunge na kikosi cha wajomba, lakini aliniambia nikirudi huko kiwango changu kitakuwa cha chini kutokana na ukaribu na wanafunzi wengine,” alisema Mayweather.

Miezi mitatu ya mwanzo Mayweather aliweza kuzoea mazoezi ya baba yake pamoja na ile hali ya kufundishwa peke yake.

“Ilibidi nizoee hali hiyo kwa kuwa nilikuwa nayakumbuka maisha niliyotokea na kujua wapi natakiwa kwenda, hivyo nilikuwa mvumilivu pamoja na usikivu wa hali ya juu.

“Hadi kufikia miezi sita nilikuwa ninaona kule ninakoelekea katika tasnia hiyo ya ngumi na mzee alikuwa ananitia moyo kila siku kuwa nitakuwa kuwa bora, nashukuru baada ya muda nikaanza kuamini kuwa naweza kufika mbali kutokana na maendeleo yangu mazoezini pamoja na michezo ya kirafiki,” aliongeza Mayweather.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here