SHARE

NA EZEKIEL TENDWA


SIKU zote binadamu anashauriwa kutokufanya uamuzi wowote akiwa na hasira nyingi, au akiwa mwenye furaha iliyopitiliza, kwani anaweza kujilaumu baada ya maamuzi hayo anayoweza kuyachukua akiwa katika moja ya hali hizo.

Ukiwa na hasira sana unaweza kuchukua maamuzi hata ya kuua, ndiyo maana ushauri ni kwamba subiri kwanza hali hiyo iondoke ndipo ujue nini la kufanya, halikadhalika ukiwa na furaha iliyopitiliza, unaweza kuruhusu jambo lolote litendeke ilimradi kuwaridhisha wanaokuzunguka halafu mwisho wa siku ikaja kukugharimu.

Bila shaka Barcelona wamechukua maamuzi ya hasira. Wameondokewa na mshambuliaji wao matata, Neymar, ambaye ametimkia PSG, na wao wakaamua kumsajili Ousmane Dembele kutoka Borussia Dortmund kwa dau la Pauni milioni 96, ambalo pia linaweza kuongezeka.

Barcelona wanadhani kuwa Dembele anaweza kuziba vema pengo lililoachwa na Neymar, aliyehamia PSG kwa dau la rekodi ya dunia,la  Pauni Milioni 198 na atavaa jezi namba 11 iliyoachwa wazi na Mbrazil huyo aliyeondoka.

Mbali na Dembele, pia bado wapo kwenye mikakati mizito ya kuhakikisha wanainasa saini ya Coutinho, anayekipiga Liverpool, lengo la Barcelona likiwa ni kuwasahaulisha mashabiki wao habari ya Neymar, anayeendelea kuuwasha moto Ligi Kuu nchini Ufaransa, akiwa na kikosi chake hicho kipya.

Wakati mashabiki wa Yanga wakianza kumsahau taratibu Haruna Niyonzima, aliyetimkia Simba, baada ya ujio wa Kabamba Tshishimbi, ambaye moto wake si wa kitoto, kwa upande wa mashabiki wa Barcelona, hawajui cha kufanya.

Barcelona ni kama wameshikwa na kiwewe na sasa wanaonekana kutaka kusajili yeyote aliyepo mbele yao, kwani wakati wengi wakidhani mbadala wa Neymar anaweza kuwa mtu kama Eden Hazard, wenyewe wamekimbilia kumwaga fedha kwa mtu kama Dembele.

Yaani hizo fedha walizozimwaga kwa Dembele na wanazotaka kuwapa pia Liverpool, walitakiwa kuzipeleka pale Stamford Bridge na kuwapa Chelsea, ili wamruhusu Hazard, na hapo hata mashabiki wao wasingelalamika sana, kwani uwezo wa Mholanzi huyo haujatofautiana sana na wa Neymar.

Jaribu mwenyewe kwenda kwenye mtandao (youtube), uanze kupitia namna Dembele, anavyocheza, ukishamaliza, wala usichoke, mtafute tena Coutinho, akiwa na timu yake ya Liverpool, na hata timu ya Taifa ya Brazil, uchunguze uwezo wake kwa umakini, na mwisho pitia uwezo wa Hazard, halafu utajua nani anayefaa kuwa mbadala wa Neymar.

Dembele ni mmoja wa wachezaji wazuri, lakini si wa kumsajili eti awe mbadala wa Neymar. Hata Coutihno ni mzuri sana, anaibeba Liverpool, lakini hata yeye hawezi kuwa mbadala wa Neymar, ni vitu viwili tofauti kabisa. Unayeweza kumsajili ukasema ni mbadala wa Neymar ni Hazard, kwani wawili hao wanakaribiana ucheza wao, vinginevyo ni kudanganyana tu.

Dembele na Coutinho hawana vitu vya ziada kama Hazard, hawana unyumbulifu unaokaribia hata robo kama Neymar, na mtu pekee sahihi kwa wakati huu ni huyo Hazard, kwani anavyo vitu vya ziada, ndiyo maana akikosekana kwenye kikosi cha Chelsea katika mchezo wowote, inaonekana kabisa hayupo, kwani pengo lake halijifichi.

Kama walivyokwenda kupita wachezaji kama David Villa, ndivyo anavyokwenda kupitia Dembele, kwani ni wazi hatakuwa na maisha marefu ndani ya kikosi hicho. Kama haamini amuulize Zlatan Ibrahimovic, ambaye naye alifika pale akakaa muda mfupi akaondoka, halikadhalika kiungo fundi Cesc Fabregas, ambaye aliondoka Arsenal, akiwa moto, akasugulishwa benchi, mwisho wa siku akaamua kuondoka.

Walichotakiwa kukifanya Barcelona, baada ya kuondokewa na Neymar, ni kutuliza akili zao ili kutafuta mtu sahihi, lakini wakaingia sokoni harakaharaka na kumwaga fedha za kutosha kwa Dembele, ambaye bila shaka anaweza akashindwa kuvaa viatu vya Mbrazil huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here