SHARE

SAADA SALIM NA HUSSEIN OMAR,

ASKARI wa Kikosi cha Mbwa waliokuwa mafunzoni katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, jana waliwazuia wachezaji wa Yanga kufanya mazoezi yao kutokana na mafunzo waliyokuwa wakiwapa mbwa wao.

Askari hao waliokuwa na mbwa wapatao sita, waliwasili uwanjani hapo majira ya saa 2:00 asubuhi na kuanza mazoezi katika uwanja huo kwa ajili ya mafunzo kwa wanyama hao.

Gazeti hili liliwasili uwanjani hapo mapema kabla ya askari hao kuwasili na kuwakuta wachezaji wawili tu waliokuwa wametangulia mazoezini ambao ni kipa Ali Mustafa ‘Barthez’ pamoja na Oscar Joshua, ambao walikuwa wakiwasubiri wenzao.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye askari pamoja na mbwa waliwasili uwanjani hapo na kumuomba mtunza vifaa wa wana-Jangwani hao, Mahmoud Omar ‘Mpogoro’, waendelee kufanya mazoezi.

Muda mfupi baadaye, basi la Yanga lililokuwa limewabeba baadhi ya wachezaji, makocha na viongozi wa benchi la ufundi liliwasili, lakini hakuna mchezaji hata mmoja aliyeshuka zaidi ya baadhi ya viongozi.

Lakini habari za ndani zinasema kuwa, wachezaji hao ambao walikuwa ni wachache, hawakushuka kwenye basi ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mgomo wao wa kutofanya mazoezi hadi walipwe mshahara wao wa Novemba.

Chanzo cha ndani kililieleza gazeti hili kuwa, wachezaji wa Yanga walikuwa hawajalipwa mishahara yao ya Novemba na ndiyo maana hawakufanya mazoezi tangu juzi Jumatatu na jana Jumanne.

“Wachezaji hawajalipwa mishahara yao ya Novemba, hawataki kufanya mazoezi na kocha ameshindwa la kufanya,” kilieleza chanzo hicho, ingawa kilikataa jina lake lisitajwe gazetini kwa kuwa si msemaji.

DIMBA Jumatano lilishuhudia uwanjani hapo wakiwepo wachezaji wanne tu ambapo mbali na Barthez na Oscar waliokuja kwa usafiri wao, lakini Haruna Niyonzima na Mzambia Justine Zullu wao walikuja kwa basi la klabu ambalo liliwasili uwanjani hapo saa 2:33.

Hata hivyo, Zullu na Niyonzima hawakushuka kwenye basi, licha ya uongozi wa benchi la ufundi linaloongozwa na George Lwandamina kuwataka wafanye hivyo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here