SHARE
Patrick Kahemele

Na Mwandishi Wetu,

WAKATI straika wa Simba Mrundi, Laudit Mavugo, akimwagwa rasmi na Wekundu wa Msimbazi, Simba, mashabiki wa klabu hiyo juzi walijitokeza kwa wingi kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko Morogoro, kushuhudia mazoezi ya kikosi hicho, huku Mcameroon mpya, Ndjack Anong Guy Serge, akionekana kuwa kivutio zaidi.

Simba imeweka kambi katika Chuo cha Biblia cha Baptist, kilichoko eneo la Bigwa, mkoani Morogoro, kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao, huku ikiwajaribu nyota wake wapya wakiwemo wa kimataifa.

Serge anakaribia kumwaga wino wa kuitumikia klabu hiyo, baada ya kuonyesha vitu adimu huku akimkuna kocha mpya Mcameroon, Joseph Omog na kuwa kivutio kwa mashabiki pia.

Kiungo huyo ameziteka hisia za mashabiki wa Simba baada ya kuonyesha umahiri mkubwa katika utoaji pasi, zikiwamo zile za visigino na chenga za kuufanya umati wa mashabiki waliofika kushuhudia mazoezi hayo kumshangilia kwa nguvu mno.

Ikiwa ana takribani wiki moja tu tangu atue rasmi, Serge ameonyesha umahiri wake pia katika upokeaji wa pasi za juu, kutoa pasi na kupiga mashuti makali.

Simba imebakisha nafasi tano za usajili kwa wachezaji wa kigeni huku ikiwa imewaleta wachezaji kutoka Zimbabwe, Cameroon, Uganda, Ivory Coast na Congo, lakini uongozi wa klabu hiyo umesisitiza kuendelea kuleta nyota wengine wapya kutoka nje.

Jana asubuhi, wachezaji wengine wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), waliwasili kambini humo kwa majaribio na wanaungana na Serge aliyetua wiki iliyopita.

Wakala wa wachezaji hao alithibitisha kuwasili kwa nyota hao ambao mmoja ni kiungo anayeweza kucheza namba nyingi uwanjani, Masanga Masudi Cedric, anayekipiga Sanga Balende ya DR Congo na mwingine ni beki Mayenge Bionik aliyetokea klabu ya FC Lupopo.

Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele, ndiye aliyewapokea wachezaji hao katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, juzi na jana wakapelekwa kuungana na wenzao wanaojifua vikali mkoani Morogoro.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kasim Dewji, alithibitishia uongozi wa klabu hiyo kuleta nyota zaidi kutoka nje ya nchi ingawa alibainisha usajili wao kutegemea na uwezo walionao.

“Kimsingi, sisi tumebakiza nafasi tano za wachezaji wa kigeni, wapo wachezaji walioko kambini lakini bado kocha (Joseph Omog) ametaka kuendelea kuwatazama mazoezini, lakini si hao tu kuna wachezaji wengine watakuja,” alisema Dewji.

Alisema zoezi la kuleta nyota kwa majaribio ni endelevu hadi pale kocha Omog atakaporidhika na kikosi kipya cha Simba anachotaka kuwa nacho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here