Home Habari MCHAWI YANGA HATIMAYE AJULIKANA

MCHAWI YANGA HATIMAYE AJULIKANA

10106
0
SHARE
NA EZEKIEL TENDWA    |  

WAKATI Yanga wakishuka uwanjani leo kuwakabili Mtibwa Sugar, kocha mkuu wa zamani wa kikosi hichom, George Lwandamina, ametajwa kama ndiye chanzo cha kikosi hicho kufanya vibaya katika michezo yao ya hivi karibuni.

Lwandamina, ambaye alikuwa akisaidiana na Shadrack Nsajigwa, aliamua kutimka zake na kujiunga na timu yake ya zamani ya Zesco United ya nchini kwao Zambia.

Licha ya kwamba hata kabla ya kuondoka, kikosi hicho kilikuwa kikikabiliwa na matatizo mengi, likiwamo la ukata, lakini walikuwa wakijikongoja na kupata matokeo mazuri, tofauti na sasa.

Tangu kuondoka kwa Mzambia huyo, kikosi hicho kimecheza michezo sita bila kupata ushindi wowote, hiyo ikiashiria kuwa, kuna namna kocha huyo alikuwa akiishi na wachezaji wake kiasi kwamba walikuwa wakicheza kwa moyo.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wameliambia DIMBA kuwa, Lwandamina alikuwa akiishi nao kama mzazi, huku akiwapa maneno ya faraja ambayo yaliwafanya kupambana ndani ya uwanja, tofauti na sasa.

“Hata wakati Kocha Lwandamina yupo tulikuwa na matatizo ya kutokulipwa mishahara, lakini alikuwa akitukalisha chini na kutuambia tupambane, kwani tunaweza tukaonekana timu nyingine ndani na nje ya nchi tukasajiliwa.

“Yaani tulimchukulia kama mzazi, tofauti na sasa, kwani hakuna aliyeweza kuvaa vizuri viatu vyake, ndiyo maana unakuta hata baadhi wanafika hatua ya kugoma,” alisema mmoja wa wachezaji waandamizi wa kikosi hicho.

Mchezo wa mwisho kwa Lwandamina kuiongoza Yanga ilikuwa ni dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Wanajangwani hao kushinda mabao 2-0.

Katika michezo hiyo sita waliyocheza bila Lwandamina, wamejikuta wakifungwa michezo minne na kutoka sare miwili.

Michezo hiyo waliyotoka sare ni dhidi ya Singida United pamoja na Mbeya City, ambazo zote zilikuwa sare ya kufungana bao 1-1, na michezo waliyofungwa ni dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia mchezo wa Kombe la Shirikisho, wakilala bao 1-0.

Michezo mingine ni dhidi ya Simba, wakifungwa bao 1-0, wakafungwa tena mabao 4-0 dhidi ya USM Alger ya nchini Algeria, mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na pia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Prisons.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya mashabiki wa Yanga wamefikia hatua ya kusema kama Lwandamina angekuwapo wasingeendelea kupata aibu hii wanayoipata kwa sasa.

Wanajangwani hao leo wanashuka Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro, kucheza na Mtibwa Sugar, ukiwa ni mchezo wa saba wakiwa bila Lwandamina, na kila mmoja anasubiri kuona nini kitatokea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here