SHARE

NA JOSEPH SHALUWA,

MAISHA yako yakoje? Unaishi vipi na jirani zako pamoja na wafanyakazi wenzako? Bila shaka jibu yakinifu utakuwa nalo mwenyewe! Unachotakiwa kuzingatia ni kwamba jinsi unavyoendesha maisha yako na wenzako ndivyo taswira ya jinsi ulivyo inavyojionyesha!

Kimsingi unapaswa kuishi na wenzako vizuri, shirikiana nao kwa kila hali katika shida na raha. Haipendezi kama wenzako wanachanga pesa za rambirambi halafu wewe unakwepa, ina maana hutafiwa? Achana na tabia hiyo mbaya isiyo na maana.

Epuka migogoro na wenzako, kama mwenzio amekukosea tumia kauli nzuri kuzungumza naye, ukimwelewesha kosa lake, inaweza kuwa hatua nzuri zaidi kuliko kubwatukiana na kusababisha migongano isiyo ya lazima.

Achana na majigambo, dharau na kujiona wewe ni zaidi ya wenzako, hiyo si tabia njema kwa kuwa binadamu wote ni sawa na tumeumbwa kwa udongo kutokana na upendo wa Mungu wetu. Bila shaka utangulizi huu ni mwafaka kwa ajili ya kuwekana sawa kwa wale wenye tabia hizo.

Mapenzi ni sawa na mchezo wa karata tatu, hata hivyo kama ukiwa makini, hakika mapenzi hayawezi kuwa karata tatu kwako. Tumeshuhudia mara nyingi mtu akiamua kukatisha uhai wake baada ya kuachwa na mpenzi wake, unajua kwanini?

Kwa sababu hakuwa amejiandaa juu ya tukio hilo, amelipokea kwa ukubwa na anajinyima haki yake ambayo ni ya kimsingi ya kuendelea na maisha kama kawaida.

Mambo huwa mrama, baada ya kugundua mpenzi uliye naye hakupendi, hakufikirii na wala hajakupa nafasi katika moyo wake, lakini kumbuka kitu kimoja, mambo haya hutokea ikiwa hukujipanga tangu mwanzo kabla ya kumkaribisha katika moyo wako.

Hatua zifuatazo ni muhimu mno kwako kuzizingatia kabla ya kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya ambaye mategemeo ya baadaye ni kuishi naye katika ndoa takatifu.

TAZAMA MAISHA YAKO YAJAYO

Katika mahusiano ni vizuri ukaanza kwanza kujipa nafasi ya kwanza kabla ya kumpatia huyo ambaye unatarajia awe mwandani wako wa maisha yako yote!

Kosa kubwa linalofanywa na vijana wengi kabla ya kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na mpenzi mpya ni pamoja na kuweka maisha ya kimapenzi katika uwingi.

Ninaposema uwingi ninamaanisha kuwa, unachanganya maisha ya mpenzi wako aliyepita, huyo mpya na maisha yako kama mamoja, jambo ambalo kisaikolojia na mpangilio mzima wa maisha yako yajayo si zuri. Jiweke namba moja, halafu mpenzi wako afuate nyuma yako!

Ukifanya hivyo, itakusaidia kuwa na uamuzi sahihi katika kila ufanyalo na kuwa na uhakika na mambo yako yajayo. Hiyo ina maana kuwa, hata kama mwanaume unayetaka kuanzisha naye uhusiano ana pesa nyingi kiasi gani, lakini usizihesabu kama zenu, bali zake!

Utakapokuwa na mtazamo wa kuangalia maisha yako yajayo, utajiweka katika nafasi nzuri kiakili na kutoruhusu uharibifu wa mwili wako, hasa kama mpenzi huyo alikuwa na nia ya kushiriki na wewe mapenzi kisha kukuacha.

USIMWONGOPEE…

Katika uhusiano na mapenzi, udanganyifu ni moja katika sumu kali sana zitakazoweza kuharibu kabisa mapenzi yenu. Katika kikao chenu cha kwanza, mnapozungumza juu ya matarajio yenu ya baadaye katika uhusiano wenu huo mchanga, hupaswi kabisa kudanganya.

Anapokuuliza juu ya wapenzi wako waliotangulia mweleze ukweli bila kumficha. Ingawa kama ulikuwa na idadi ya wapenzi zaidi ya watano, usimwambie kwa kuwa inawezekana akakuchukulia kama mapepe!

Mwombe naye awe mkweli kwako, usiruhusu uongo kabisa, ni sumu kali sana ya mapenzi. Mweleze athari za uongo katika mapenzi na umtake awe wazi kwa kila kitu kinachotokea katika maisha yake.

Mathalani una tatizo la msisimko wa mapenzi, ni vyema ukimwambia mapema. Pia inawezekana ukikaribia kufika mshindo, unafedheheka au unazimia ni vizuri kumwambia mapema ili aamue kusuka au kunyoa!

ELEZA  HISIA ZAKO

Hapa hutakiwi kuogopa, kwa sababu ndio mhimili wa penzi lenu changa, mwambie mapema kuwa hupendi disko ila unapenda kwenda beach, au mwambie unapenda sana kunywa pombe au hutaki kusikia habari za pombe. Hapo utakuwa umewasilisha hisia zako kwa uwazi.

Bila shaka mpenzi wako mpya, atakujua ulivyo na haitakuwa kazi ngumu kufanya yale unayoyapenda na kuacha yale ambayo anatambua kabisa huyapendi.

Hebu fikiria kidogo kuhusu hili, upo na mpenzi wako mahali fulani, kwenye mfuko wake wa shati ana pakiti zima la sigara, anachokifanya ni kuchomoa moja baada ya nyingine, basi anatoa mimoshi mtindo mmoja!

Ni jambo linalokuudhi, lakini unashindwa kumweleza, hata kama ukimweleza, atalichukuliaje? Bila shaka itakuwa ni matatizo kwa sababu ataona unamharibia starehe yake kama sio kumwingilia maisha yake.

Lakini kama mngekuwa wazi tangu mapema haya yote yasingetokea. Angeelewa wewe unahitaji nini kutoka kwake na yeye anahitaji nini kutoka kwako, ungefahamu hapendi nini naye angejua unachukia nini, huo ndio umuhimu wa kuwa wawazi katika hatua za mwanzo kabisa za uhusiano wenu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here