Home Habari Mechi nne kuipa Simba ubingwa

Mechi nne kuipa Simba ubingwa

458
0
SHARE

kiizaNA SAADA SALIM

WANAODHANI Simba imejiondoa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara hasa baada ya kufungwa na watani zao wa jadi, Yanga mabao 2-0 watakuwa wamekwaa kisiki kwani kocha mkuu wa kikosi hicho Mganda, Jackson Mayanja, amesema anazo mechi nne tu za ubingwa.

Licha ya kwamba Wekundu hao wa Msimbazi wamebakisha michezo 10 kumaliza ligi, Mayanja amesema anaona mechi nne ngumu na kama akivuka salama basi mashabiki wa Simba wajiandae kupokea kombe hilo ambalo wamelikosa kwa misimu mitatu mfululizo.

Bila kung’ata maneno, Mayanja alizitaja timu hizo zinazomuumiza kichwa kuwa Mbeya City ambao watakutana Jumapili hii Uwanja wa Taifa, mchezo dhidi ya Azam FC, Tanzania Prisons pamoja na Mtibwa Sugar.

Amesema anafanya kila linalowezekana kuhakikisha anaibuka na ushindi katika michezo hiyo akianzia na mchezo dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa wiki hii ambapo amekikimbiza kikosi chake Morogoro kujiandaa ipasavyo.

Akizungumzia mchezo huo dhidi ya Mbeya City, Mayanja alisema anaamini atakutana na upinzani mkubwa kutokana na ubora wa Wagonga Nyundo hao lakini ana imani kwamba uwezo wa wachezaji wake utakuwa chachu ya kupata ushindi.

“Mbeya City ni moja ya timu ngumu sana, ubora wao ulianza kuonekana wakati walipopanda Ligi Kuu kwani walimaliza katika nafasi ya tatu, naamini mchezo huo utakuwa mgumu ila naamini vijana wangu watafanya makubwa kama ninavyoendelea kuwapa mbinu za ushindi,” alisema.

Wekundu hao wa Msimbazi wapo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 45 nyuma ya Yanga waliopo kileleni na pointi 46 sawa na Azam waliopo nafasi ya pili, timu hizo zikipishana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

 

Huenda Wekundu hao wa Msimbazi wakakaa kileleni mwishoni mwa wiki hii kama wataibuka na ushindi katika mchezo wao huo dhidi ya Mbeya City kama Yanga watatoka sare ya aina yoyote na Azam Jumamosi.

Pia kama timu hizo moja itaibuka na ushindi kati ya Yanga na Azam na Simba nao wakaibuka na ushindi dhidi ya Wagonga Nyundo hao, basi Wekundu hao wa Msimbazi watashika nafasi ya pili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here