SHARE

NA SALMA MPELI

WAKATI zikitimia siku 67 tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, medali za mshindi wa pili wa ligi hiyo, Simba, zinaendelea kupata kutu katika ofisi za Bodi ya Ligi hiyo (TPLB), baada ya uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi kugomea kuchukua tuzo hizo, kwa madai kuwa hawautambui ubingwa wa Yanga.

Simba waligomea kuvaa medali hizo Mei 20, mwaka huu, siku ambayo ligi hiyo msimu uliopita ilimalizika rasmi, kwa kile kinachodaiwa ni kuendeleza mgomo wao juu ya kuwatambua Yanga kwamba ndiyo mabigwa wa Ligi hiyo.

Akizungumza na DIMBA jana, Mkurugenzi Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura, alisema Simba iliagizwa kuandika barua ya kujieleza kwanini waligomea kuchukua tuzo hizo, lakini hadi sasa bado haweza kutekeleza agizo hilo.

“Tuliwaagiza Simba kuandika barua ya maelezo ya kwanini waligoma kuchukua tuzo hizo, lakini hadi leo bado hawajafanya hivyo, tutakutana kama bodi katika kikao na kujadili jambo hilo na pia kuwataka tena kwa mara nyingine wafanye hivyo na kuwapa muda na wasipotekeleza basi hatua nyingine zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Wambura.

DIMBA lilimtafuta Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo, ambapo alisema kuwa, Bodi ya Ligi haikuwaandikia barua ya kuwataka wao kujibu maelezo yao, hivyo aliwataka wao kufanya hivyo kwanza ili Simba waweze kujibu.

“Hatujapokea barua ya Bodi ya Ligi kutaka sisi tuandike barua ya kujieleza, na wao watakapoanza kutuandikia basi na sisi tutawajibu,” alisema Manara kwa kifupi.

Hatua hiyo ilikuja baada ya uongozi wa Simba kuandika barua kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wakidai haki yao ya kupewa pointi tatu kutoka kwa Kagera Sugar, ambao waliwalalamikia kuwa walimchezesha beki wao, Mohammed Fakhi, ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.

Simba walimkatia rufaa mchezaji huyo na kudai kuwa alichezeshwa kimakosa, kwa kuwa alikuwa na kadi hizo, lakini ushahidi ukaja kuonekana kuwa jambo hilo si kweli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here