Home Makala Messi, Suarez Ni kwanini wameachwa tuzo ya Ulaya

Messi, Suarez Ni kwanini wameachwa tuzo ya Ulaya

349
0
SHARE

Na Markus Mpangala

MAJINA matatu ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya yametolewa. Waliobaki ni Antonio Griezmann (Atletico Madrid), Gareth Bale (Real Madrid) na Cristiano Ronaldo (Real Madrid). Wote hawa wanatoka timu zilizopo jiji la Madrid, nchini Hispania na La Liga.

Kwa kawaida wapo wenye maswali ni kwa nini wachezaji watatu hao wamefika hapo huku manguli kama Lionel Messi na Luis Suarez wameachwa? Ni kwa vipi Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Hispania, Luis Suarez ameachwa?
Imekuwaje Lionel Messi ameachwa safari hii na badala yake kuna maingizo mawili mapya, Gareth Bale na Antonio Griezmann?
Kwa mtazamo wangu, zipo sababu nyingi za wachezaji watatu hao kuwepo hapo walipo. Kwanza Griezmann, Bale na Ronaldo wameshiriki Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka huu na kufika hatua nzuri zaidi kwenye michuano inayohusisha mataifa ya Ulaya.

Lionel Messi na Luis Suarez pia wameshiriki Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini, maarufu kama Copa America. Messi alifanikiwa kufika fainali ya michuano ya Copa Amerika lakini akakosa kombe. Luis Suarez hakufua dafu na Uruguay yake.

Sifa kubwa ya Messi na Suarez msimu uliopita ni kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania. Lakini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa waling’olewa katika hatua ya nusu fainali na Atletico Madrid.

Sidhani kama michuano ya Copa America inatumika kama kigezo cha kuibuka mchezaji bora wa Ulaya. Ronaldo, Bale na Griezmann wanacho kitu walichoongeza kwenye wasifu wao msimu uliopita.
Kwanza, Messi na Suarez wamefungwa na Antonio Griezmann kwa maana aliwatoa kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa katika ngazi ya klabu. Kwa maana hiyo, Griezmann alifika fainali, ingawa alifungwa.

Kusema hivyo ni sawa na kutumia msemo wa wahenga kuwa mshindi huchukua vyote. Ndivyo ilivyokuwa kwa Griezmann dhidi ya Messi na Suarez.

Kwa kuwa Griezmann ametoka Ufaransa ambayo ni taifa lililopo barani Ulaya, bila shaka ni moja ya sababu ya nyongeza iliyomfikisha hapo. Ufaransa ilikuwa mwenyeji wa fainali za Euro 2016, ikachapwa kwenye fainali na Ureno kwa bao 1-0.

Griezmann alikuwa mmoja wa wafungaji bora wa michuano ya Euro mwaka huu, baada ya kuzifumania nyavu mara sita (mabao 6), akiwa amecheza kwa kiwango bora kabisa ambacho kinastahili tuzo.

Gareth Bale naye amepata sifa ya nyongeza kwenye michuano ya Euro ambapo kwa mara ya kwanza waliposhiriki Wales walifika hatua ya nusu fainali kabla ya kufungwa na Ureno.

Lakini jambo jingine ni kwamba Bale ametwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu yake ya Real Madrid. Hii ni sifa ya pili ambayo inamwonyesha kupata mafanikio kuliko washambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi na Suarez.

Kwa upande wake, Suarez alifunga mabao yake 40 na kutengeneza mabao 16. Ronaldo alifunga mabao 35 na kutengeneza mabao 11. Lionel Messi alifunga mabao 26 na kutengeneza mabao 16.

Antonio Griezmann alifunga mabao 22 na kutengeneza mabao matano katika La Liga. Bale amefunga mabao 19 na kutengeneza 10 katika La Liga. Katika Ligi ya Mabingwa Griezmann alifunga mabao 7 na kutengeneza moja.

Ronaldo alikuwa na sifa nyingine ya ziada kutinga fainali ya kutafuta mchezaji bora wa Ulaya. Mreno huyo alipachika mabao 16 na kutengeneza manne kwenye Ligi ya Mabingwa. Ronaldo pia ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Uefa.

Ukifuatilia takwimu zote hizo utapata jibu kuwa Luis Suarez alistahili kuingia kwneye ‘top three’ ya kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya. Lakini utamwekaje wakati alifungwa na Griezmann kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa? Hapo ndipo utakuta ule msemo, mshindi huchukua vyote, ingawaje Suarez anamzidi Girezmann idadi ya mabao ya kufunga Ligi ya Mabingwa. Tofauti ni bao moja tu.

Tofauti na Messi ambaye alizidiwa mno na Griezmann kwenye Ligi ya Mabingwa, Lionel Messi alipachika mabao 6 na kutengeneza moja. Kwenye La Liga Messi amemzidi Griezmann, lakini unapofika kuamua kuchagua mmoja kati yao mwenye msimu mzuri, Griezmann alimzidi Messi ukizingatia alimfunga pia kwenye nusu fainali.

Hapakuwa na njia nyingine ya kuwaacha Griezmann na Bale kwenye mchuano wa tuzo ya Ulaya. Lakini kitu kingine ambacho kimekuwa kikisemwa miaka yote katika tuzo ya Ulaya ni uzawa.
Siyo kubwa, lakini ukiangalia walioteuliwa wote wazawa wa Ulaya (japo huko nyuma washindi wengine walikuwa kutoka mabara tofauti).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here