Home Michezo kitaifa MFARANSA AANZA MAVITU YA KIMATAIFA

MFARANSA AANZA MAVITU YA KIMATAIFA

3296
0
SHARE

NA SAADA SALIM

KAMA utani vile soka la timu ya Simba linaanza kubadilika, ikiwa ni muda  mchache tangu kocha mpya wa timu hiyo, Mfaransa Pierre Lechantre, alipoanza kukisuka kikosi chake baada ya kukabidhiwa majukumu rasmi Januari 23, mwaka.

Kocha huyo anayeshirikiana kwa karibu na msaidizi wake, Masoud Djuma, wamekuwa wakibadili aina za mazoezi mara kwa mara, ambapo kocha Pierre  alisema nia yake ni kukiandaa kikosi hicho kimataifa.

Wekundu hao wa Msimbazi wataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo watacheza dhidi ya Gendarmerie Tnale ya Djibout kati ya Februari 9 hadi 11, mwaka huu na kocha huyo ameweka bayana kuwa mazoezi ya nguvu wanayoyafanya kwa sasa ni kuhakikisha wanafanya maangamizi.

Awali kabla ya kukabidhiwa mikoba rasmi, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Djuma Masoud, alikuwa akitumia mfumo wa 3-5-2, lakini juzi katika mchezo wao dhidi ya Majimaji ambao ni wa kwanza Mfaransa huyo kukalia benchi, walitumia mfumo wa 4-1-3-2.

Mfumo huo ulionekana wazi kueleweka kwa wachezaji kutokana na kucheza kandanda safi na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, hiyo ikimaanisha kuwa kwa sasa Simba wana hazina ya mifumo mingi.

Moja ya mambo ambayo Mfaransa huyo amekuwa akiyasisitiza ni wachezaji wake kuongeza kasi ili kuhakikisha kila timu inayokuja mbele yao wanaishushia kipigo cha maana.

Wakati benchi la ufundi wakifanya yao, kwa upande wa uongozi kigogo mmoja ameliambia DIMBA Jumatano kuwa watashirikiana vizuri kuhakikisha lengo lao la kufanya vizuri kimataifa linatimia.

Katika hatua nyingine, Straika wa kikosi hicho, Emmanuel Okwi, alisema kwa mafunzo na mbinu wanazopewa na kocha wao huyo kwa kushirikiana na msaidizi wake Masoud Djuma, timu hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa na kufika mbali zaidi.

“Kikubwa ni kufuata maelekezo ya kocha wetu, kwani lengo kubwa kwetu ni kuhakikisha tunashinda michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri kimataifa,” alisema.

Simba inayoongoza ligi kuu hadi sasa, itavaana na Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here