Home Habari MGHANA WA AZAM NJE MIEZI TISA

MGHANA WA AZAM NJE MIEZI TISA

6910
0
SHARE

 

NA SAADA SALIM

HII ni taarifa mbaya kwa Azam FC, baada ya kupokea taarifa kutoka Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town nchini Afrika Kusini, kwamba watakosa huduma ya beki wao Mghana, Daniel Amoah aliyegundulika kuwa na tatizo kubwa kwenye goti lake.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema Amoah alikuwa akisikia maumivu kwenye goti, majeraha aliyoyapata miezi miwili iliyopita katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania baada ya kudondokea sakafu nje ya uwanja.

“Baada ya uchunguzi, amegundulika ana tatizo la kukatika mtulinga wa kati wa goti, vilevile amechanika washa ‘meniscus’ ambayo ipo katikati ya goti, pia ameonekana ana sehemu ndogo iliyovunjika katika sehemu ya juu ya mfupa wa ugoko karibu na maungio ya goti,” alisema.

Amoah aliondoka Machi 26, mwaka huu na mchezaji mwenzake, Waziri Junior ambaye naye anakabiliwa na majeraha  wote wakifikia katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town kwa matibabu.

Akimzungumzia Waziri Junior, Mwankemwa alisema: “Waziri naye alikwenda huko kwa ajili ya kupata matibabu na kushauriwa kupumzika kwa siku tano, kwa hiyo ataanza mazoezi ya kwenye sehemu za tifutifu (mchanga) Aprili 5 au 6,” alisema.

Mwankemwa akizungumzia taarifa ya David Mwantika aliyelazwa Muhimbili, alisema mchezaji huyo anaendelea vizuri na huenda leo akapata ruhusa ya kurudi nyumbani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here