Home Uncategorized MIAKA 30 SAFARI YA MUZIKI YA ALLY CHOKI-(45) Arudishwa Twanga kibabe, afanya...

MIAKA 30 SAFARI YA MUZIKI YA ALLY CHOKI-(45) Arudishwa Twanga kibabe, afanya uamuzi mgumu

541
0
SHARE

NA JUMA KASESA

JUMATANO wiki hii katika simulizi ya Safari ya Miaka 30 ya Muziki ya ‘Kamarade’ Ally Choki Mzee wa ‘Farasi’, mwanamuziki huyo aliishia akisimulia namna alivyonasa katika rada za Mkurugenzi wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), marehemu Kepteni John Komba.

Kepteni Komba aliamua kuifanyia umafia menejimenti ya bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ kwa kumpa mkataba kinyemela Choki ili atue TOT na kuiacha bendi hiyo kwenye mataa hatua ambayo ilimchukiza Asha Baraka na kaka yake Baraka Msilwa, hivyo kukoleza bifu la muda mrefu baina ya menejimenti hizo mbili.

Kupitia mkataba huo Kepteni huyo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliwatumia marehemu Hemedi Mpakanjia na Chicago Matelephoni wampe Choki gari aina ya Suzuki ya kutembelea kama kishika ‘uchumba’ kabla ya kusaini mkataba wa mwisho kuanza kuitumikia TOT.

Sasa endelea…

ASET ilichukulia tukio la mimi kunyakuliwa na TOT kama jeraha kubwa kwa wakati ule, kwani bado Twanga Pepeta haikuwa na mwanamuziki mwenye uwezo wa kufunika nyota yangu. Ilikuwa ngumu kwa Twanga kukubali kirahisi niondoke na kuona tena nachukuliwa na mtu ambaye ni adui yao kibiashara ya muziki.

Itakumbukwa bado ASET ilikuwa ikiugulia jeraha la wakati ule TOT ilipowafanyia umafia kwa kumchukua kibabe marehemu Ramadhani Masanja ‘Le General Banza Stone’, ili aende kunogesha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kwenye mchuano mkali dhidi ya vyama vya upinzani.

Baraka Msilwa aliniita ofisini na kunihoji ukweli kama nimesaini TOT na nini msimamo wangu kuhusu kubaki Twanga Pepeta baada ya kuvuja kwa taarifa hizo. Kwakuwa tayari nilikuwa nimeshaichoka bendi hiyo bila kupepesa macho nilimueleza kwa uwazi nataka kuondoka nikachape mzigo TOT ambako wameonyesha kunijali kwa kunipa gari ninalotembelea na pia tumeafikiana wanipe mkataba mnono.

Kipande cha mtu jasho lilimtoka mara baada ya kusikia kauli hiyo ikitoka kwangu, kwani alishtuka na hakuamini kama kweli naweza kufanya uamuzi mgumu kama huo tena kwenda kujiunga na bendi maadui wa TOT. Baraka alilazimika kunyanyua simu na kumtwangia Kepteni Komba kujaribu kupata ukweli wa jambo hilo ambapo alikutana na majibu hayo niliyomwambia.

Alichokifanya Baraka ni kumwambia Komba Choki haondoki TOT kwani ana mkataba na ASET na kushutumu kwanini ameamua kunipa mkataba wakati bado sijamaliza ule nilionao Twanga Pepeta na kumueleza kwamba wamefanya kosa la kisheria.

Menejimenti ya ASET ilitishia kumpandisha kizimbani Komba kwa kuingia mkataba na mwajiriwa wao kinyume na taratibu za kazi huku wakijua fika kufanya hivyo ni kosa.

Komba kwa kujiamini akijua kwamba sina mkataba na ASET alijibu Choki ni mali ya TOT kwani yeye si mjinga kuamua kufanya usajili wake kwa kumpa gari bila kujiridhisha kama kweli bado ni muajiriwa wa bendi hiyo.

Baada ya mjadala na malumbano mafupi kwenye simu Baraka naye alisisitiza Ally Choki haondoki Twanga Pepeta na kama ni suala la kumpa gari basi inaweza kuwa imekula kwa TOT, vinginevyo menejimenti ya pande hizo mbili ikae mezani kutafuta mwafaka kama ataona inafaa.

Kiukweli wakati ule sikuwa na  mkataba na ASET lakini waliamua kukomaa kwamba mimi bado ni mfanyakazi wao halali hatua ambayo binafsi ilinikera lakini sikuwa na la kufanya na itakumbukwa tayari walishaonyesha dharau kwangu kwa kushindwa kuniongeza mkataba muda mrefu.

Menejimenti ya ASET baada ya kuona kama Kepteni Komba na TOT wamewashika pabaya walilazimika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo kwa Baraka Msilwa kunyanyua simu tena na kumuuliza kwamba gari hilo lina thamani ya Sh ngapi ili warudishe fedha ili nisiondoke.

Bifu la pande hizo mbili tayari halikuwa siri tena kwani baadhi vyombo vya habari vililikuza kiasi cha kufanya mashabiki na wadau wa muziki kuelekeza akili zao kwenye mgogoro ili kuona nani atashinda vita hiyo ya mafahari wawili.

Kepteni Komba baada ya kutafakari kwa kina huku akishauriana na watu wake wa karibu Mpakanjia na Chicago Matelephoni, aliamua kuketi mezani na menejimenti ya ASET ili kusaka mwafaka kwani tayari chuki ilikuwa kubwa kwa mashabiki wa TOT na Twanga Pepeta kiasi cha kufanyiana vurugu katika baadhi ya maonyesho.

Komba aliweka sharti ASET irudishe gharama za ununuzi wa gari hilo aina ya Suzuki lenye thamani ya Sh mil.6 na wao kama TOT wako tayari kuachana na Choki iwapo tu fedha hizo zitalipwa mara moja ili waangalie mwanamuziki mwingine atakayeiendeleza bendi yao, kwani kipindi kile ilishaanza kudorora baada ya Banza kuwa naye ameshaondoka.

Lilikuwa jambo jepesi tu kwa Baraka kurudisha kiasi hicho cha fedha kwa makubaliano gari litabaki kuwa mali ya Choki ili mradi tu niendelee kuwepo Twanga.Muafaka ulipatikana kila upande kutekeleza makubaliano ambayo yalifungua ukurasa mpya kwa mimi kubaki Twanga Pepeta.

Sikuwa na furaha na Twanga Pepeta kwani tayari ndoto zangu zilishakuwa kubadili upepo wa maisha kwa aidha kuanzisha bendi yangu au kwenda TOT ambako tayari nilikuwa nimetengewa maslahi bora ya maisha ya muziki. Nilikaa Twanga kwa kipindi cha miezi sita nikiwa sina furaha kabisa nafsi yangu ikiwa imeingia nyongo nyeusi. Kitu kilichonikera ni kwamba nikiwa Twanga nikawa kama mtu ambaye siamini kama awali kutokana na kadhia hiyo ya kutaka kuondoka. Niliumiza kichwa vya kutosha huku nikifanya mipango yangu kwa siri nifanye nini kwani sikuwa na furaha ndani ya bendi hiyo hatimaye siku isiyoliwa kitu nilifanya uamuzi mgumu.

Uamuzi gani mgumu ulifanywa na Choki, usikose kusoma DIMBA siku ya Jumatano kupata mwendelezo wa simulizi hii. Kwa maoni na ushauri 0715-629298.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here