Home Habari MITAMBO IMEWAKA

MITAMBO IMEWAKA

431
0
SHARE

CLARA ALPHONCE NA SALMA MPELI

SIMBA jana ‘iliwasha rasmi mitambo’ yake kuashiria imeiva kwa Ligi Kuu Tanzania, baada ya kuinyuka Rayon Sports ya Rwanda bao 1-0, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba ilishuka dimbani na silaha zake mpya na za zamani kuikabili Rayon, ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa wachezaji wake wapya iliowasajili msimu mpya.

Kabla ya mchezo huo kuanza, kikosi cha Simba kilitambulishwa rasmi kwa mchezaji mmoja mmoja, ambapo nahodha wa timu hiyo, Method Mwanjali, alifungua dimba la utambulisho, huku wachezaji wapya wa kimataifa, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima, wakifunga utambulisho huo kwa shangwe.

Katika mchezo huo, ambao Simba walionyesha kujipanga, huku wakicheza soka la kuvutia, waliweza kuibuka na ushindi wa bao hilo moja lililowekwa nyavuni na Mohammed Ibrahim ‘MO’, kufuatia kazi nzuri ya Okwi, aliyepokea mpira kutoka kwa Kichuya.

Simba iliendelea kucheza soka la kuvutia katika kipindi cha kwanza, huku Okwi akikosa bao dakika ya 21, Bocco naye akakosa dakika ya 22, akishindwa kumalizia mpira wa kona, uliopigwa na Okwi.

Kwa upande wa wapinzani wao Rayon, walikosa nafasi chache, mojawapo ni ile ya kipindi cha kwanza, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Simba, lakini umakini wa kipa Aishi Manula na mabeki wake, vilisaidia kuokoa hatari hiyo.

Kama Bocco na Okwi wangeongeza umakini katika nafasi zao, basi Simba ingeweza kutoka na ushindi wa mabao mengi, kwani walipata nafasi nyingi za wazi na kujikuta wakizipoteza, hivyo kwenda mapumziko wakiwa na bao hilo hilo moja.

Kipindi cha pili kilipoanza, Rayon walianza kucheza soka la kushambulia na kujikuta wakipoteza nafasi zao kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Simba.

Baada ya kipindi cha pili kuanza Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, aliwapumzisha Mohammed Ibrahim, Jamal Mwambeleko, Okwi na James Kotei na kuwaingiza Jonas Mkude, Haruna Niyonzima, Nicholaus Gyan pamoja na Ali Shomari.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuweza kuzaa matunda, kwani hata baada ya mashambulizi ya hapa na pale, Simba ilikosa mabao kadhaa, mojawapo ikiwa ni lile la dakika ya 60, Kichuya aliposhindwa kumalizia kazi nzuri ya Niyonzima.

Niyonzima, ambaye alicheza dakika 45 za pili, baadaye tena aliwatengenezea mastraika nafasi nyingine, ambapo Okwi na Gyan walishindwa kumalizia na hadi mpira unamalizika, Simba ilitoka uwanjani kifua mbele kwa bao 1-0.

DONDOO:

Mwigulu atinga na tisheti nyekundu

Mmoja wa viongozi wa Serikali, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi na shabiki mkubwa wa Yanga, Mwigulu Nchemba, jana alikuwa uwanjani hapo kunogesha tamasha hilo, ambapo kama sehemu ya sapoti yake, aliamua kuvaa jezi nyekundu, huku akiongozana na Waziri mwenzake, Januari Makamba.

Uwanja wafurika

Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tamasha la Simba Day ambalo hufanyika kila mwaka, jana Uwanja wa Taifa ulionekana kujaza idadi kubwa ya watu, waliofika kushuhudia tamasha hilo.

Kwa kawaida, ukiacha mechi ya Simba na Yanga, ambayo inaongoza kwa kujaza idadi kubwa ya watu, Uwanja wa Taifa huwa ni mara chache unajaa katika mechi za kawaida, lakini kwa jana watu walikuwa wengi kiasi kwamba ilibaki sehemu kidogo tu ufurike.

Niyonzima/Okwi wafunika

Wachezaji nyota wa klabu hiyo, Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi walifunika wakati wa utambulisho wa wachezaji.

Msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, ambaye ndiye aliyekuwa akitoa utambulisho, aliwaita wachezaji hao mwishoni na wakati wakiingia umati wa mashabiki uligubikwa na kelele za shangwe.

Tshabalala, Kibadeni wazoa tuzo

Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, jana alikabidhiwa tuzo ya heshima na mashabiki baada ya kuibuka mchezaji bora wa msimu wa klabu, pamoja na mashabiki wake.

Mbali na Tshabalala, pia kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni, naye alipewa tuzo ya heshima kama kocha aliyeipa timu hiyo mafanikio makubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here