Home Makala Mkali wa ‘asisti’ aliyetelekezwa na Guardiola ageuka dili Ulaya

Mkali wa ‘asisti’ aliyetelekezwa na Guardiola ageuka dili Ulaya

2016
0
SHARE

DORTMUND, Ujerumani

MAMBO yanaonekana kwenda sawa kwa kinda wa Borrusia Dortmund, Jadon Sancho, ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa timu pinzani.

Katika michezo 43 aliyocheza msimu huu, nyota huyo wa miaka 19 alitupia mabao 13, huku akitoa pasi za mabao ‘asisti’ 19.

Sancho, ambaye ni raia wa England, alijumuishwa katika kikosi cha timu hiyo kilichotumika kwenye michezo ya Ligi ya Mataifa Ulaya kilichocheza dhidi ya Croatia na Hispania.

Kwa umri wake wa miaka 19, tayari amekuwa kivutio kikubwa kwa timu kubwa Ulaya kama Manchester United, Real Madrid, Bayern Munich, Juventus na Barcelona, ambazo zimeonekana kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya chipukizi huyo.

Hivi karibuni wachezaji wengi raia wa England wamekuwa wakitoka kucheza ligi nyingine tofauti na zamani ilivyozoeleka kwa kiasi kikubwa walitoka ligi ya ndani kuunda kikosi cha timu ya Taifa.

Sancho alifikaje Borrusia Dortmund? Vipi kuhusu maisha yake mengine ya nje ya uwanja, ana mchumba au hana? Vyote hivyo unavipata katika makala haya.

SANCHO NI NANI?

Sancho alizaliwa Machi 25, 2000, nchini England, hakuna taarifa yoyote inayohusisha wazazi wake kama wote ni raia wa England au kuna mchanganyiko.

Tofauti na wengine, Sancho hana taarifa kamili za wakati wake wa utoto zaidi ya kujulikana aliwahi kusoma shule za Harefield Academy na  Middlesex, lakini hata nyota huyo anayekipiga Borrusia Dortmund si mwongeaji kuhusu maisha yake binafsi.

Mpaka anafika miaka saba, Sancho inaaminika alikuwa shabiki mkubwa wa mchezo wa tenisi, lakini miaka mitatu baadaye alibadili maamuzi na kuingia kwenye mchezo wa soka.

CITY YAMWIBA WATFORD

Maisha ya soka ya chipukizi hayo yalianzia katika shule ya kukuzia vipaji ya timu ya Watford, ambayo inasifika kwa kutoa wachezaji mahari kwenye historia ya soka la England.

Alifanikiwa kuonyesha kipaji kikubwa katika shule hiyo na kuwa gumzo kwa timu nyingine ambazo zilionyesha nia ya kuhitaji huduma yake, zikiwamo Manchester United, Chelsea na Arsenal.

Lakini ni Manchester City ambao walifanikiwa kumshawishi na kumvuta katika shule yao ya kukuzia vipaji mwaka 2014.

Inaaminika Manchester City waliwashawishi wazazi wa mchezaji huyo na kuwaahidi kuwafanyia mambo mengi kama wakifanikisha kumpeleka kijana wao ndani ya klabu hiyo.

Sancho alionyesha uwezo mkubwa ndani ya akademi ya Manchester City na kupelekea msimu wa 2015/16 kusaini mkataba wa kuitumikia timu ya wakubwa.

Sancho anatumika vizuri katika nafasi za straika na winga, kwa kasi yake na uwezo wa kumiliki mpira ukionekana kuwa hatari kwa mabeki wa timu pinzani.

Mwaka 2017 alifanikiwa kucheza kwa dakika nne mchezo wa kwanza akiwa na jezi ya wakubwa ya Manchester City, alipoingia kuchukua nafasi ya Raheem Sterling.

Tangu hapo hakufanikiwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha wakubwa mpaka alipoondoka na kuelekea nchini Ujerumani.

DORTMUND YAMVUTA

Klabu ya Borrusia Dortmund ilifanikiwa kupata saini ya Sancho kwa dau la pauni milioni 8, na kumsainisha mkataba wa miaka mitano katika dirisha la usajili la Januari mwaka huu.

Sancho hakuanza Ligi ya Ujerumani vizuri na kuzua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo waliosimuliwa habari zake za kuvutia tangu alipokuwa Manchester City.

Lakini msimu huu kinda huyo ameuanza kwa kasi kubwa na kuandika historia ya kutoa pasi nyingi za mabao ‘asisti’ zaidi ya mchezaji yeyote katika ligi kubwa tano za Ulaya.

TIMU KUBWA ZAMVUTIA KASI

Kutokana na uwezo aliouonyesha Sancho mapema msimu huu, baadhi ya timu zimeonekana kumfuatilia kwa ukaribu zaidi na ikiwezekana kumsajili.

Kubwa zaidi hata Manchester City wanaonekana kuwa tayari kumsajili kwa mara nyingine kiungo huyo aliye kwenye ubora mkubwa hivi sasa.

Pia, Manchester United, Chelsea, Real Madrid, Bayern Munich na Barcelona wapo makini na kupigana vikumbo kwa kinda huyo raia wa England.   

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here