Home Habari MKWARA MZITO YANGA

MKWARA MZITO YANGA

622
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

MKWARA mzito. Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Ngaya de Mbe ya Comoro, Yanga wameibuka na kudai kuwa sasa Simba watafute chaka la kujifichia kwani mara hii hawatatoka salama Uwanja wa Taifa.

Wanajangwani hao ambao wametua jana kutoka Comoro, walifanikiwa kupata ushindi huo, ikiwa ni michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo licha ya kwamba mchezo wa marudiano ni mwishoni mwa wiki hii, wanaonekana zaidi kujipanga kwa ajili ya Simba.

Timu hizo mahasimu zinatarajiwa kukutana Februari 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo tayari tambo kwa pande zote zimeshaanza kutoka kila mmoja akisema ataibuka na ushindi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege  wa Taifa wa Mwalimu Nyerere, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, alisema ushindi wa mabao mengi kutoka kwa wapinzani wao hautafanya wakabweteka na kuona kwamba wamemaliza kazi.

Alisema kwa sasa wanataka kushinda kila mchezo uliopo mbele yao wakianza na huo dhidi ya Ngaya wa marudiano na pia michezo mingine ya ligi kuu ambapo ni dhidi ya Simba hiyo Februari 25.

“Tunataka kushinda kila mchezo uliopo mbele yetu, niseme tu kwamba bado hatujamalizana na hawa Ngaya na hatuwezi kuwadharau isipokuwa tutapambana kuhakikisha tunashinda tena Uwanja wa Taifa,” alisema.

Kwa upande wake nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, licha ya kuzungumzia mchezo huo dhidi ya Ngaya, pia aliwazungumzia Simba na kudai kuwa anawaheshimu ila wanaangalia zaidi ushindi.

“Nawaheshimu Simba ni timu nzuri, ila sitaihofia kwani nimeshakutana nao mara nyingi, hivyo ni mchezo ambao utakuwa wa kuvutia na ushindani mkubwa, kwa jinsi tulivyo nina imani tutashinda,” alisema Cannavaro.

Wakati Mwambusi na Cannavaro wakisema hivyo, idadi kubwa ya mashabiki wao wana imani kuwa watawafunga Simba kwa idadi kubwa ya mabao na wanatamani siku hiyo ifike haraka.

“Tunatamani hiyo siku ifike haraka kwani hicho tulichowafanya hawa Wacomoro tunataka tuwafanye na Simba, bado tunakumbuka yale mabao yao 5-0 na sasa ni zamu ya kuyalipa,” alisema Musa Iddy.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here