SHARE

CATALUNYA, Hispania

SAKATA la Neymar limeendelea kushika kasi baada ya mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi, kuwaambia mabosi wa timu hiyo wafanye kila linalowezekana ili kunasa saini ya winga huyo raia wa Brazil.

Licha ya Barcelona kufanya usajili wa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann bado Messi anaamini Neymar anahitajika ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa Hispania.

Hata hivyo, imegundulika Messi mwenye umri wa miaka 32 amewaambia mabosi wake kuwa kama wanataka asaini mkataba wa kuendelea kuwepo Nou Camp, basi wamsajili Neymar kwanza.

Taarifa zinadai hata baadhi ya wachezaji ndani ya Barcelona wamekuwa wakishinikiza kwa nguvu kusajiliwa kwa winga huyo mwenye umri wa miaka 27.

Mastaa kama Luis Suarez na Gerrard Pique wanatajwa kuwa mstari wa mbele, huku kila mmoja akiamini kuwa Neymar anastahili kusajiliwa kwa mara nyingine tena ndani ya Barcelona.

Mwaka 2013, Neymar alisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 76 na Barcelona kutoka Santos FC ya Brazil lakini miaka minne baadae aliweka rekodi ya usajili kwa kusaini kandarasi ya miaka sita na PSG kwa kiasi cha pauni milioni 196.

Mwandishi wa kituo cha Sky Sport, Graham Hunter, alitoboa siri hiyo huku akidai kuwa Barcelona hawako tayari kumpoteza mshambuliaji huyo raia wa Argentina.

“Messi anacheza katikati ya mambo yote yanayoendelea Barcelona, kila mmoja anasema lake lakini akiwa hana furaha, Nou Camp yote inapata baridi.

“Rais wa Barcelona, Josep Bartomeu alisema kabla hajaondoka mwaka 2021 atahakikisha Messi anasaini mkataba mpya, lakini kwa kinachoendelea inabidi atafakari mara mbili kabla ya kufanya maamuzi.

“Ni kweli Messi amewaambia anamtaka Neymar, usajili wa Griezmann bado haujakidhi mahitaji kwake, anamtaka Mbrazil ambaye walitengeneza utatu wa MSN miaka michache iliyopita.

“Yeye, Suarez na Neymar, licha ya kuwa na tabia tofauti lakini wote ni marafiki wa karibu sana.

“Mara ya mwisho Barcelona walishinda makombe matatu ‘treble’ wakati wanaongozwa na MSN katika idara ya ushambuliaji, licha ya Neymar kuwa kwenye anguko la kiwango chake bado Messi anaamini atakuwa na msaada mkubwa sana,” alisema Hunter.

Imefahamika kuwa klabu ya sasa ya Neymar, PSG wanahitaji fedha taslim kiasi cha pauni milioni 190, bila kujumuishwa mchezaji yoyote kama ambavyo Barcelona wanatajwa kufanya kwa kuwaweka Philippe Coutinho, Ousmane Dembele, Malcom, Samuel Umtiti na Nelson Semedo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here