SHARE

NA MAREGES NYAMAKA

MIPANGO ya Simba kushinda mechi tano mfululizo ardhi nyumbani ya Dar es Salaam ili kutangaza ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi, baada ya kuvuna alama sita Mbeya mbele ya Mbeya City na Tanzania Prisons, imekwama.

Ugumu ulianzia kwa Kagera Sugar waliondeleza ubabe kwa kumtungua Mnyama kabla ya suluhu ya juzi dhidi ya Azam. Maana yake pointi 15 walizokuwa wanazihitaji, tayari nne zimeyeyuka inawafanya kuendelea kupambana.

Miongoni mwa mapungufu ya Simba katika mechi hizo mbili za mwisho ni kushindwa kutumia vizuri mipira ya kona, pamoja na faulo nje kidogo ya boksi ‘free-kick’.

Mara ya mwisho katika matumizi mazuri ya nafasi hizo ilikuwa ni mechi dhidi ya Mbeya City, Jonas Mkude akifunga bao la kusawazisha akimalizia ‘free-kick’ iliyochongwa na Nicolas Gyan pamoja na Meddie Kagere, akimalizia ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Ilikuwa tofauti mechi dhidi ya Azam zaidi ya kona 10 zilizopigwa pamoja na ‘free-kick’ zaidi ya sita hazikuwa na faida, moja kati wachezaji wenye matumizi mazuri ya miguu yao katika hiyo mipira ni Emmanuel Okwi katika mitatu yote aliyopiga hakuwa amefanikiwa.

Weka pembeni mapungufu hayo, nakurejesha nyuma katika michezo mitano ya mwisho, kuna kijana mwili mdogo, Yusufu Mlipili, amemwonyesha kocha wake, Patrick Aussems kuwa miguu yake ni ya thamani kweli kweli.

Katika mechi zote hizo dhidi ya Mbeya City, Tanzania Prisons, KMC, Kagera Sugar na Azam zote Mlipili amecheza kwa utulivu tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, zile faulo zake kwa mastraika zimekuwa adimu sana kuziona.

Huenda kipimo kikubwa zaidi kwa Mlipili mbele ya bosi wake, Aussems, kilikuwa mbele ya Mzambia, Obrey Chirwa wa Azam aliyetembea naye ‘Man-to-man marking’ muda mwingi wa mchezo, lakini pia kwenye ‘Zonal marking’ yenyewe.

Ni ngumu sana hadi ligi inafika tamati Mlipili akiwa kwenye kiwango hicho kumwona akiingia kwenye orodha ya wanaoachwa. Kama timu inamkosa chaguo la kwanza tangu msimu unaanza  Pascal Wawa kwa muda wa wiki nne na Mlipili anaonyesha kilichobora, unathubutu vipi kumweka kwenye mstari mwekundu?

Bahati nzuri ubora huo unaonekana katika wakati muhimu zaidi ambao timu inahitaji ubingwa ndani ya mechi chache zilizosalia. Kuruhusu mabao matatu katika mechi tano, nidhamu ya mchezo vinachagiza namna alivyokamaa kumudu presha za kuchezea timu kubwa.

Maboresho maradufu ya kikosi bora msimu ujao kama alivyowahi kuweka wazi bilionea kijana, mwekezaji wa timu, Mohamed Dewji, huenda umefanya kundi kubwa la wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi mara chache kujituma kwa asilimia zote 100.

Mlipili amefanya hivyo, anaujua uzito wa jezi ya Simba hasa uwepo wa kupata nafasi ya kucheza michuano mikubwa ya kimataifa. Kabla ya hivi sasa aliweza kuwazuia mastraika wa Al Masry  Kombe la Shirikisho ugenini chini ya  Pierre Lechantre.

Iilikuwa ni suala la muda tu msimu huu kuaminika mbele ya Mbeligiji, Patrick Aussems ambaye baada ya Erasto, Juuko Murushid, Pascal Wawa, Paul Bukaba, chaguo la mwisho alikuwa yeye Mlipili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here