SHARE

NA WINFRIDA MTOI

SUALA la kufungashiwa virago kwa kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems, linazidi kuchukua sura mpya kila kukicha kutokana na kuendelea kuonekana akikinoa kikosi hicho tangu taarifa za kuondolewa kwake zilipovuja.

Ni muda mrefu tetesi za kung’olewa kocha huyo raia wa Ubelgiji aliyeipa Simba mafanikio makubwa msimu uliopita, zimekuwa zikichukua nafasi sehemu mbalimbali, huku baadhi ya viongozi wa ndani wa klabu hiyo kukiri kuwepo kwa mpango huo.

Ishu hiyo ilipamba moto baada ya wiki iliyopita Aussems alipoondoka ghafla ikidaiwa kuwa alikwenda kufanya mazungumzo na klabu ya Polokwane ya Afrika Kusini.

Kitendo cha kocha huyo kuondoka kwa kuwashtukiza mabosi wake akidai alipata dharura, imezidi kuchochea moto safari yake ya kuondoka Msimbazi kwa sababu inadaiwa waajiri wake hawakuridhishwa na jinsi alivyoondoka, akiaga akiwa tayari yupo uwanja wa ndege.

Kwa taaarifa zilizopo, tayari Aussems amekabidhiwa barua ya kusitisha ajira yake huku akiwekewa kikao cha kujieleza, kwanini aliondoka bila kuaga kwa utaratibu unaotakiwa.

Lakini jana zimeibuka taarifa mpya zinazokinzana na kocha huyo ambazo zinadai bado Mbelgiji huyo ataendelea kuwepo Msimbazi hadi mkataba wake utakapofikia tamati.

DIMBA Jumatano limepata taarifa kwamba kuna mvutano juu ya kuachana na kocha huyo, ikidaiwa kuwa kinachombeba Aussems ni mafanikio aliyoyapata na kikosi hicho na jinsi timu inavyoendelea kufanya vizuri, huku wapenzi wa timu hiyo wakitaka abaki hadi watakapokutana na watani zao Yanga Januari 4 mwakani.

Ni wazi kuwa benchi lote la ufundi la Simba halina uhakika wa maisha yao ndani ya timu hiyo, kutokana na kila mmoja kuitwa na Ofisa Mtendaji wa Klabu hiyo (CEO), Senzo Mazingiza, kujieleza kwa wakati wake.

Hadi jana taarifa zilizolifikia DIMBA Jumatano, zinasema kulikuwa na vikao vizito na CEO huyo pamoja na watendaji mbalimbali wa klabu ajenda ikiwa ni kujadili uamuzi gani ufanyike, hususan baada ya kudaiwa kuwa Aussems ameomba radhi kwa kile alichokifanya.

“Kama Aussems atafukuzwa, basi hadi mwisho wa mwezi huu kocha mpya wa Simba atakuwa amejulikana, lakini pia kuna uwezekano akaendelea kuwepo,” kilisema chanzo hicho.

Mazingiza amekuwa akikaririwa akisema, Aussems bado ni kocha wa Simba na kwamba hawana mpango wa kuachana naye kwa sasa.

Licha ya Mazingiza kutoa kauli hiyo, lakini ukweli ni kwamba mwenye uamuzi wa mwisho, kumuondoa Aussems ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ ambaye ndiye mwekezaji wa klabu hiyo.

Hiyo inatokana na baadhi ya matukio aliyowahi kuyafanya, katika kipindi cha usajili, ambayo mengi hayakuhitaji kujadiliwa na viongozi wenzake.

Mfano ni kipindi cha usajili ambacho MO amekuwa akibeba jukumu la kugharamia kwa kiasi chochote mchezaji ambaye Wanasimba wanahitaji kumuona kikosini mwao.

Hata hivyo kocha Aussems mwenyewe ameeleza kukerwa na taarifa hizi zinazosambaa juu yake, akidai kwamba ni za uzushi huku akisisitiza kwamba yeye bado yupo katika klabu hiyo na siku atakapoondoka haitakuwa na kificho kama alivyokuja. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here