SHARE

NA SAADA SALIM


 

WACHEZAJI wa Simba wamejikuta wakioga minoti kutoka kwa mfanyabiashara na mwanachama maarufu wa timu hiyo, Mohammed Dewji (MO), kutokana na jinsi wanavyoiletea heshima klabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kwamba, Mo pamoja na baadhi ya matajiri wengine ndani ya Simba, wamekuwa wakivutiwa na uwezo wa kikosi pamoja na matokeo wanayoyapata kwa sasa.

Kubwa zaidi walilovutiwa nalo ni baada ya timu yao kuifunga Yanga bao 1-0, hali iliyopelekea vigogo hao kuamua kuchangishana ili kuwafuta jasho wachezaji wao hao.

Licha ya kiasi hicho cha fedha kutowekwa wazi, baadhi ya wachezaji wamelithibitishia DIMBA Jumatano kuwa wamevuta fedha za kutosha kutoka kwa viongozi wao hao na wameahidi kuhakikisha wanaendelea kufanya kweli.

“Kwa sasa vigogo wetu wanatujali sana, wamekuwa wakitupa motisha pale tunapopata matokeo mazuri, hata juzi tu wametupa kifuta jasho baada ya kuwafunga Yanga na sisi tumewaahidi kupambanaa kuhakikisha tunatwaa ubingwa bila kufungwa,” alisema mmoja wa wachezaji nyota wa kikosi hicho.

Naye Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema wamekutana na wachezaji wake na kupanga mikakati yao ambayo hata hivyo hakutaka kuiweka wazi.

“Ni kweli mara kwa mara tunakutana na wachezaji na kuweka mikakati, siwezi kukwambia ni mikakati gani lakini nitoe wito kwa mashabiki wetu kuwa tupo vizuri kuhakikisha tunatwaa ubingwa bila kufungwa,” alisema.

Kikosi cha Simba kimeendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Boko na kinatarajia kuondoka kesho kwenda Singida kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya wenyeji Singida United.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here